Ijumaa, 21 Oktoba 2016

MAZISHI YA MZEE KUNGUBAYA

MWANAMUZIKI mkongwe ambaye alipata umaarufu kutokana na wimbo wake Salam za Wagonjwa amezikwa leo katika makaburi ya kifamilia Njeteni Kwembe. Msiba huo ulihudhuria na watu wengi wakiwemo majirani, ndugu, wanamuziki na wapenzi wa muziki wa Mzee Kungubaya.Tatu itakuwa siku ya Jumamosi 22/10/2016.
Jeneza likiwa nje ya nyumba ya marehemu

Mwanamuziki Mjusi Shemboza akiongea na mmoja wa watoto wa marehemu Mzee Kungubaya
Mjusi Shemboza akiwa na Mtendaji Mkuu wa COSOTA wa zamani Mzee Mtetewaunga

Msafara wa kuelekea makaburiniMazishi ya Mzee Kungubaya

Alhamisi, 20 Oktoba 2016

BURIANI OMARY KUNGUBAYA

kungubaya
Mzee Omari Kungubaya akipiga gitaa siku ya mkesha wa msiba wa Dr. Remmy Ongala
MZEE Omari Kungubaya ambaye atakumbukwa kwa wimbo wake Salam za wagonjwa, wimbo uliokuwa ukiashiria kuanza na kuisha kwa kipindi cha salamu za wagonjwa kupitia Radio Tanzania kwa miaka mingi amefariki leo mchana baada ya afya yake kuwa si nzuri kwa muda mrefu. Msiba wake uko nyumbani kwake Njeteni, Mbezi ya Kimara Habari zaidi tutawaleteeni Mungu amlaze pema peponi

Ijumaa, 7 Oktoba 2016

BURIANI SALOME KIWAYA


Picha iliyopigwa Uingereza wakati Salome alipoenda huko na Shikamoo Jazz Band. Toka Kushoto Marehemu Salome Kiwaya, Marehemu Papa Wemba, na Marehemu Bi Kidude Mungu awalaze pema.
Kwa masikitiko makubwa nimepokea taarifa za msiba wa Mama Salome Kiwaya, mwanamuziki mkongwe. Taarifa zilinifikia kuwa Salome amefariki katika ajali ya gari iliyotokea Dodoma sehemu za Meriwa. Nilimfahamu Salome kwa mara ya kwanza mwaka 1987, wakati nikiwa bendi ya Tancut Almasi Orchestra, tulipopiga kambi Dodoma Hotel kwa muda wa miezi mitatu, tukitoa burudani kwanza kwa wajumbe wa mkutano wa Kizota, kisha wenyeji wa mji wa Dodoma. Katika kufahamiana  kipindi hicho, tuliweza hata  kupiga wimbo wake mmoja ulioitwa Tuhina, uliokuwa ukiimbwa na Kasaloo Kyanga na Kyanga Songa, ambao nao ni marehemu. Siku moja nilipita mtaani Dodoma na kununua kanda za muziki wa Salome, nilizipenda sana nyimbo zake na nikamuahidi kuwa ningejitahidi kuzipeleka kwa watu wenye uwezo wa kuendeleza kazi zile. Nilizipeleka kanda kwa Ronnie Graham, Mscotch mmoja mwenye upenzi na uelewa mkubwa wa muziki wa Kiafrika na hasa rumba, na huyu Mscotch ndie aliyewezesha kuanzishwa kwa bendi ya Shikamoo Jazz Band. Baada ya kuzisikia nyimbo zile akaamua kuwa Salome asindikizane na bendi ya Shikamoo kwenye ziara yao ya Uingereza kama muimbaji wa kike. Salome alienda Uingereza na aliporudi ndipo alipoanza kununa vyombo na kuunda kundi la Saki Stars, ikiwa ni kifupi cha Salome Kiwaya Stars. Mume wake Mzee Kiwaya nae ni msanii maarufu aliyekuwa kiongozi wa kikundi cha Utamaduni cha CDA miaka hiyo ya 80. Kuanzia hapo nimekuwa karibu sana na Salome, miaka ya 90 wakati nikiwa Mwenyekiti wa CHAMUDATA, Salome ndie alikuwa mwenyekiti wa chama hicho katika mkoa wa Dodoma baada ya mkutano mkubwa wa wanamuziki uliofanyika mwezi June 1998, kule Bagamoyo, ambapo wanamuziki 265 waliweza kukusanyika pamoja na kukaa siku nne katika mji wa Bagamoyo wakifanya warsha za fani mbalimbali za muziki. Katika miaka ya karibuni Salome alishughulika na sanaa ya urembo akiwa wakala wa Miss Tanzania kwa kanda ya Kati na kuweza kutoa MIss Tanzania mmoja, baadae aliingia katika siasa na kufikia kuwa Mwenyekiti wa UWT wa Mkoa wa Dodoma, lakini aliendelea na muziki katika maisha yake yote.

Mungu Amlaze Pema Salome Kwaya. Ucheshi wako hatutausahau. 
JOHN KITIME

Alhamisi, 22 Septemba 2016

TANGA MJI ULIKOANZA MUZIKI WA DANSI


Wiki hii nilipata bahati ya kutembelea mji wa Tanga, mji ambao  sifa zake zilianza kusikika kuanzia enzi za utawala wa Wajerumani, jiji ambalo shule ya kwanza ya serikali ilijengwa hapa enzi hizo hizo za utawala wa Wajerumani, jiji ambalo liliendelea kukua sana kutokana na kilimo cha katani na hivyo kukusanya vijana toka kila kona ya nchi kuja kutafuta kazi katika mashamba makubwa ya katani wakati huo. Tanga mji ambao kutokana na uwingi wa vijana wakati huo, shughuli za burudani ya muziki nazo zilifikia kiwango cha juu kuliko sehemu nyingi Tanzania.
Ukizungumzia historia ya muziki wa dansi, huwezi kukwepa kuzungumzia Tanga, kwani historia inatueleza kuwa kabla ya kuanza vikundi vya muziki wa dansi kulianzishwa klabu za kucheza dansi. Klabu hizo zikitumia muziki wa santuri, wanachama wake walicheza na hata kushindana kucheza muziki kwa mitindo mbali mbali ya kigeni ikiwemo waltz, tango, chacha, rumba na kadhalika. Klabu za kwanza nchini zilianzia Tanga. Kulikuwa na klabu kama Young Noverty miaka michache baada ya vita ya kwanza ya dunia, wakati huo nchi ya Tanganyika ikiwa bado changa kabisa. Mtindo huu wa vilabu vya dansi ulienea na baadae kuingia Dar es Salaam na miji mingine iliyokuwa imeshaanza wakati huo. Vilabu hivi ndivyo baadae vikaanzisha vikundi vya kwanza vya muziki wa dansi. Hata majina ya vikundi hivyo vya kwanza yalihusiana na klabu za burudani za wakati huo. Kulikuwa na vikundi kama Coast Social Orchestra, Dar es Salaam Social Orchestra na kadhalika.  Hivyo mji wa Tanga ulikuwa katika ndoto za vijana enzi hizo. Kwa vile vijana wengi walikusanyika katika jiji hili nchi, kulianzishwa pia klabu ambazo zilikuwa kwa ajili ya vijana waliokuwa wakitoka kabila moja. Klabu hizo zikiwa na nia ya wananchama wao kusaidiana katika shida na raha, na vilabu hivi pia vilikuwa ni sehemu muhimu katika kutoa burudani kwa vijana waliotoka sehemu moja. Kati ya klabu hizi kulikuweko na klabu iliyoitwa Young Nyamwezi, kama jina lake lilivyo ilikuwa ni klabu ya vijana kutoka Unyamwezini. Hatimae mwaka 1955 klabu hii ilianzisha bendi yake iliyoitwa Young Nyamwezi Band, bendi hii ilikuja kukua na baada ya Uhuru ilibadili jina na kuitwa Jamhuri Jazz Band. Hakika kwa vijana waliokuwa wapenzi wa muziki miaka ya 60 na 70 ilikuwa lazima uifahamu Jamhuri Jazz Band, muziki wake, au kwa lugha ya enzi zile, ‘vibao’ vyake vilijulikana Afrika ya Mashariki nzima. Bendi hii ilikuwa ikibadili mitindo ya upigaji wake na kupiga katika mitindo ya ‘Toyota’ na hatimae ‘Dondola’. Aliyekuja kumiliki bendi hii, ambayo wapenzi wake pia waliita JJB alikuwa Joseph Bagabuje,  kulikuwa hata maelezo wakati fulani kuwa JJB ilikuwa kifupi cha Joseph Jazz Band na si Jamhuri Jazz band. Kama ilivyokuwa kawaida ya bendi za wakati ule Jamhuri Jazz Band ilisafiri sana na kufanya maonyesho katika kila kona ya nchi yetu, jambo hilo pamoja na kuwa bendi hii ilirekodi na kutoa santuri kupitia kampuni za kurekodi za Kenya na pia kurekodi nyimbo zake katika radio ya Taifa uliifanya bendi hii kuwa maarufu sana. Upigaji wa aina ya pekee wa gitaa la rhythm wa bendi hii, ambao uligunduliwa na Harrison Siwale, maarufu kwa jina la Sachmo, uliigwa na wapiga magitaa ya rhythm wengi nchini. Uimbaji wa kutumia waimbaji wawili tu, uliopendelewa na bendi za Tanga wakati huo ikiwemo bendi nyingine maarufu wakati huo, Atomic jazz Band, ulikuwa ni wa aina yake pia. Jamhuri Jazz Band pia ndio kilikuwa chanzo cha bendi maarufu ya Simba wa Nyika na bendi zilizozaliwa baada ya hapo. Nilibahatika kukutana mtu aliyekuweko siku ya kwanza ya safari ya kuja kuzaliwa kwa Simba wa Nyika, hakika ni hadithi yake ilikuwa ya kusisimua. Inasemekana kuwa siku hiyo Jamhuri Jazz Band ilikuwa imekodishwa kwa ajili ya kupiga kwenye harusi kule Muheza. Wanamuziki walikuwa wakilazimika kukusanyika katika jengo la klabu lililokuwa Barabara ya 15 ili kupata usafiri wa kwenda  Muheza. Siku hiyo wanamuziki wengine walikusanyika lakini George na Wilson Peter, Luza Elian a wengine wachache hawakuonekana, baada ya upelelezi mfupi ikajulikana kuwa wamejificha au wameondoka mjini Tanga, hivyo ikalazimika kutafuta wanamuziki viraka wa haraka haraka kuweza kufanikisha onyesho la siku hiyo, msimuliaji alinambia kuwa japo yeye hakuwa mwanamuziki bali shabiki tu wa bendi aliweza kupanda jukwaani na kuimba katika harusi hiyo, hali haikuwa mbaya kwani alijitokeza mteja mwingine akitaka bendi ikapige kwenye harusi yake pia, lakini ombi lake lilikataliwa kwani wanamuziki walijua kuwa hawakuwa kwenye kiwango chao. Na baada ya hapo kikaanza kipindi kigumu kwa Jamhuri Jazz Band kujitahidi kurudisha hadhi na ubora wa bendi, na pia ikaanza safari iliyokuja kubadili historia ya muziki wa dansi Afrika mashariki kwa vijana hawa waliotoroka kuelekea Arusha ambako walianzisha Arusha Jazz Band na hatimae kuvuka mpaka na kuingia Kenya ambako walianzisha Simba wa Nyika ambayo  mafanikio yake yanatingisha hisia za wapenzi wa muziki wa dansi mpaka leo.


Jumanne, 13 Septemba 2016

JAMHURI JAZZ BAND


Kwa mara ya kwanza niliwaona 'Live', Jamhuri Jazz Band wakipiga katika ukumbi wa Community Centre Iringa, ukumbi maarufu kwa wenyeji wakati huo kwa jina la Olofea senta (Welfare Centre). Ni vigumu kuelezea jinsi nilivyokuwa najisikia kwani nilikuwa sidhani kama kutakuja kuweko na wanamuziki wanapiga vizuri namna ile. Lakini katika wote mpiga rythm guitar Harison Siwale, aliyejulikana kwa jina la Satchmo, alikuwa na anabakia kuwa mpiga gitaa aliyenifurahisha kuliko wote. Kwanza alikuwa na staili ya peke yake, na mpaka leo nikisikiliza nyimbo zake kama vile Blandina, Mganga no 1, Maria bembeleza mwana au Ewe ndege, nabaki kusifia kuwa huyu bwana alikuwa na kipaji cha pekee. Kuna rafiki yangu aliwahi kumuuliza wakati ule huwa anapataje mawazo ya kupiga gitaa lake kwa staili ile? alijibu kuwa huwa anajaribu kupiga sauti za viumbe mbalimbali wa porini katika gitaa lake.
Wanamuziki waliokuwa katika bendi ya Mkwawa High School,  Manji, Sewando, Danford Mpumilwa, Askofu Kakobe watakumbuka jinsi walivyoweza kupata nafasi ya kupiga pamoja na bendi hii kila ilipokuja Iringa mjini, maana hizo ndiyo zilikuwa taratibu wakati huo lazima bendi kubwa ikija, wanamuziki wadogo huomba Kijiko, na kama unaweza kuimba au kupiga vizuri unaachiwa nafasi ili muhusika akatafute mpenzi. Bendi ikifika katika mji, kama mji ule una bendi basi nao watapata nafasi ya kushirikiana na wageni.  Bendi hii ilianza kwenye miaka ya 50 ikiwa ikijulikana kama Yanga Nyamwezi Band, Kiukweli ilikuwa ni Young Nyamwezi Band, bendi iliyokuwa imetengenezwa kwa ajili ya Vijana toka Tabora waliokuja kukata mkonge katika mashamba ya mkonge yaliyokuweko Tanga miaka hiyo. Na baada ya Uhuru ikajulikana kama Jamhuri Jazz Band, kifupi JJB japo kifupi hicho baadae kilidaiwa kuwa kilikuwa kifupi cha jina mwenye bendi Joseph Bagabuje. Wakati wa uhai wa Jamhuri Jazz bendi Tanga kulikuwa kuna waka moto kwa vikundi maarufu katika Afrika ya Mashariki kuwa vyote katika mji huo. Atomic Jazz, Amboni Jazz, Lucky Star, Black Star. Kwa vyovyote Tanga ulikuwa mji wa starehe wakati huo, hasa ukikumbuka kuwa kulikuweko na bendi nyingine ambazo hazikuwa maarufu labda kutokana na aina ya muziki zilizokuwa zinapiga. Kama vile ile bendi ya Magoa The Love Bugs ambayo ndiyo hatimae ilikuja kuwa The Revolutions na sasa Kilimanjaro Band
Mbaruku Hamisi,Abdallah Hatibu, Zuheni Mhando

Eliah John, Alloyce Kagila, Musa Mustafa

Yusuf Mhando, Joseph Bagabuje, Rajabu Khalfani


George Peter, Harrison Siwale, Wilson Peter

Ijumaa, 9 Septemba 2016

HASSAN SHAW MPIGA KINANDA MKONGWE

Shaw Hassan Shaw
Kwa wapenzi wa Vijana Jazz wanakumbuka vile vipande vya kinanda vilivyokuwa vikianzisha zile nyimbo mbili alizokuwa akiimba Kida Waziri, Penzi Haligawanyiki na Shingo feni, mpigaji wake alikuwa Shaw Hassan Shaw Rwamboh. Mwanamuziki huyu alizaliwa tarehe 25 September 1959, Dar Es Salaam. Alianza kujifunza kupiga gitaa na wenzie kando ya Ziwa Tanganyika huko Kigoma, wakitumia magitaa ya tajiri mmoja aliyekuwa na meli ya uvuvi. Alipokuja Dar es Salaam akakutana na mwanamuziki Zahir Ally Zorro, Zahir ndiye aliyeboresha upigaji wake wa gitaa kiasi cha kukubaliwa na Patrick Balisidya kupiga gitaa la rythm katika bendi yake ya pili PAMA Band, chini ya Afro70.
Hassan Shaw wa kwanza kulia aliyenyoosha mkono. Mwendeshaji wa blog hii John Kitime wa kwanza aliyesimama kushoto. Hapa wakiwa Stadium Morogoro.
Ni chini ya malezi ya Patrick alipojifunza kupiga Keybords (Kinanda). Baada ya hapo aliacha muziki na kujiunga na Dar Technical College. Lakini 1980 alijiunga na Vijana Jazz kama mpiga Keyboards, alishirikiana na wanamuziki wengi lakini wengi kwa mapenzi ya Mungu,  wametangulia mbele ya haki. Baadhi ya waliobaki kati ya aliyokuwa nao wakati huo ni John Kitime, Kida Waziri, Saad Ally Mnara, Hamisi Mirambo, Huluka Uvuruge, Hassan Dalali, Hamza Kalala na Rashid Pembe. Mwaka 1990 alijiunga na Orchestra Safari Sound, chini ya Maalim Muhidin Gurumo (MJOMBA), na Marehemu Abel Baltazar, hapa alikutana na wanamuziki kama Benno Villa Anthony na Mhina Panduka (Toto Tundu) .Aliacha bendi baada ya miezi sita tu, mwenyewe anasema, ‘….kutokana na muhusika kutozingatia mkataba wangu…’. Alihamia Zanzibar na kujiunga na bendi iliyokuwa ikipiga Mawimbini Hotel, hakukaa sana kwani Washirika Tanzania Stars walimwita. Hapa akakutana na mwalimu wake wa gitaa Zahir Ally, Ally Choki, Musemba wa Minyugu,Tofi Mvambe, Abdul Salvador na wengine, ilitokea kutoelewana baina ya wanamuziki na yeye kama kiongozi wa bendi ilibidi aachie ngazi kuepusha bendi kuzidi kujichanganya. Baada ya hapo Kanku Kelly ambaye ni mume wa dada wa mke wake alimuita ajiunge na Kilimanjaro Connection Band. Anasema Kanku alimvumilia sana kwa kuwa alikuwa hajawahi kufanya kazi ya kukopi nyimbo za wanamuziki wengine wakubwa duniani, hatimae akaweza kujiendeleza na kuweza kumudu kupiga vitu vikubwa, bendi hii ya Kanku  ilikua inazunguka kwa kupiga muziki hotel mbalimbali katika nchi za Malaysia, Singapore, Indonesia, Thailand na Japan jambo ambalo lilifanya aone kila kitu ni kigeni kila alipokwenda. Katika bendi hiyo alishirikiana na akina Kanku Kelly, Mafumu Bilal, Maneno Uvuruge, Burhan Adinan, Shomari Fabrice, Bob Sija, Fally Mbutu, Raysure boy, Delphin Mununga na Kinguti System. Baadaye Shaw, Kinguti na Burhan Muba waliamua kuanzisha kundi dogo wakitumia sequencer keyboards na kumuaga Kanku Kelly. Group hili lilijiita Jambo Survivors Band, bendi ambayo itakumbukwa  kwa ule wimbo Maprosoo ulioimbwa na MlasiFeruzi ambao uliokuwa katika album ya MAPROSOO.
Mlasi feruzi
Baada ya hapo bendi ikaanza kuzunguka nchi mbalimbali ikipiga katika mahotelini. Wameshapita Oman , Fujairah, U.A.E, Singapore, Malaysia na sasa wapo Thailand. Shaw anasema wanamuziki ambao hatawasahau kwa kuwa wamemfikisha alipo ni Zahir Ally Zorro, Marehem Patrick Balisdya, Waziri Ally, Kinguti System, Burhan Muba na Kanku Kelly. Kituko ambacho hawezi kusahau ni nchini Malasyia wakati akiwa na Kanku Kelly na ikiwa ni mara ya kwanza kwake kupiga muziki akiwa amezungukwa na watu weupe watupu. Anasema nyimbo zote zilipotea kichwani akawa hakumbuki hata nyimbo moja aliyokuwa kafanyia mazoezi

Jumatano, 7 Septemba 2016

WESTERN JAZZ BAND MOJA YA BENDI ILIYOKUWA MAARUFU TANZANIA

Mzee Iddi Nhende ndiye aliyepata wazo la kuanzisha bendi maarufu ya Western Jazz. Iddi Nhende alianza muziki akiwa bado mdogo katika bendi ya shule alipokuwa Primary huko Nzega, mwaka 1944 alijiunga na Tabora Boys Secondary na hapa akajiunga na Brass Band ya shule ambapo alikuwa mpigaji wa Cornet. Alimaliza shule na kuja Dar es Salaam kujiunga na Chuo cha Afya, Sewa Haji Medical Training Center. Baada ya kumaliza mafunzo akaajiriwa Bohari ya madawa na kisha mwaka 1957 alihamishiwa Muhimbili. Upenzi wake wa muziki ulimfanya mwaka huohuo ajiunge na Rufiji Jazz Band kama mpiga trumpet, bendi hii wakati huo ilikuwa ikifanya maonyesho yake Minazini Community Centre iliyokuwa eneo linaloitwa siku hizi Mchikichini na pia walikuwa wakipiga muziki katika ukumbi wa Arnatougro.
Kutokana na miji kuwa ndio ilikuwa inaanza, watu wengi kutoka maeneo mbalimbali walihamia mijini na kujaribu kutafuta wenzao waliotoka sehemu moja na kuwa na vikundi vya kusaidiana au kuwaunganisha, watu wa sehemu mbalimbali walianzisha bendi wakazipa majina ya wanakotoka, hivyo waanzilishi wa Rufiji Jazz walitoka Rufiji, na ndivyo ilivyokuwa kwa Kilwa Jazz, Ulanga jazz na kadhalika. Hivyo Iddi Nhende aliyekuwa ametoka Nzega akaamua kuanzisha bendi ya watu kutoka Magharibi, kwa kuwa nchi ilikuwa imegawanywa katika majimbo, yakiweko majimbo kama Northern Province, Southern Highlands Province, Western Province na kwa vile Nhende alitoka Western province akaanzisha Western Jazz Band 1959. Akanunua vyombo aina ya Grampian toka duka la Souza Junior duka la vyombo vya muziki lililokuwepo mtaa wa Mkwepu. Aliweza kupata fedha baada ya kuuza ng’ombe kadhaa wa mamake. Wakati huo katika bendi za aina yake ni Dar es Salaam Jazz Band peke yake waliokuwa na magitaa ya umeme, hivyo Nhende akawa na kazi ya kuwatafuta wapigaji ambapo alimfuata mpiga gitaa la umeme wa kwanza Haus Dibonde(Msukuma), aliyekuwa anapigia Dar es Salaam Jazz Band(hii ilikuwa chini ya Mzee Muba), baada ya hapo akawapata wanamuziki wengine kutoka Ulanga Jazz Band, wakati huo chombo cha banjo kilikuwa muhimu hivyo akamtafuta mpiga banjo toka Cuban Marimba tawi la Dar es Salaam. Cuban Marimba wakati huo ilikuwa na tawi Dar Es Salaam lililokuwa chini ya Mzee Mwaipungu. Mwaka mmoja baadae alipata transfer ya kwenda Morogoro, hivyo huku nyuma alilazimika kuongeza wasanii ili kuimarisha bendi wakati hayupo. Akampata David Makwaya mwimbaji, na Ally Rashid(huyu ameacha muziki karibuni akiwa Msondo), mpiga Saxaphone toka Zanzibar. Bahati mbaya yule mpiga gitaa Haus akapata kichaa katika mazingira yaliyohusishwa na ushirikina kutokana na ushindani wa bendi uliokuwepo. Hivyo basi walifuatwa wanamuziki watatu toka Tabora Jazz, wanamuziki hao walikuwa wametoka pamoja katika bendi iliyokuwa na makazi Mwanza ikiitwa Kimbo Twist Band na wakahamia Tabora Jazz, na kutoka hapo wakachukuliwa na Western Jazz. Wanamuziki hao walikuwa
Rashid Hanzuruni, Kassim Mponda na Omary Kayanda. Baada ya kazi nzuri sana, Hanzuruni Nae akarukwa na akili katika mazingira yale ya yule mpiga solo wa kwanza akalazimika kurudishwa Tabora ambako alikaa mpaka mauti yake. Wema Abdallah akachukua nafasi ya mpiga solo katika bendi ya Western. Tatizo la kinidhamu lilifanya Wema aondolewe Western, na mpigaji mwingine mzuri sana Shamba Abbdallah akachukua nafasi, solo la huyu bwana linasikika kwenye nyimbo ka Rosa na kadhalika.
Hall la nyumbani la Western Jazz lilikuwa Alexander Hall, ambalo lilikuja kuwa hall la DDC Kariakoo. Western walinunua drums baada ya Kilwa Jazz kununua drums na kuzipitisha kwao kuwaringia. Walinunua toka kwa bendi moja ya Wagoa iliyoitwa De Mello Brothers. Western walirekodi santuri kadhaa chini ya mkataba waliyousaini na lebo ya Phillips ya Kenya. Hatimae Western na mtindo wao wa Saboso walitoweka katika anga za muziki miaka ya mwisho ya sabini. Kati ya nyimbo zao nyingi ni hizi hapa; Rosa, Vigelegele, Jela ya Mapenzi, Helena no 1 na 2.