LAPF

LAPF
LAPF

Ijumaa, 1 Oktoba 2010

Kuanzishwa kwa Mlimani Park Orchestra

Sababu ya Mlimani Park kuzaliwa ikiwa imeundwa na kundi kubwa la wanamuziki kutoka Dar International ilitokea kwa bahati sana. Kwa maelezo ya mwanamuziki aliyekuwepo wakati huo, hadithi nzima ilitokana na bendi ya Dar International kukodishwa na Chuo Cha Ardhi katika sherehe yao ya kuwaaga wanachuo wazamani na kukaribisha wapya. Chuo cha Ardhi kilikodi ukumbi wa Mlimani Park kwa ajili ya shughuli hiyo. Wakati huohuo utawala wa Mlimani Park ulikuwa mbioni kutengeneza bendi baada ya kumalizika mkataba wa Orchestra Fukafuka katika ukumbi huo. Tchimanga Assossa ambaye alikuwa amekuja na Bendi ya Fukafuka alibaki nchini na alikuwa katika hatua za mwisho za kwenda kufuata wanamuziki wengine kutoka Kongo kwa ajili ya ukumbi huo. Hivyo basi Dar International wakati huo ndio wakivuma na nyimbo kama Magreti walianza kuporomosha muziki chini ya kiongozi wao Abel Balthazal. Uongozi wa Mlimani Park ulipigwa butwaa na muziki wa hawa jamaa, Abel aliitwa pembeni na kuulizwa bendi iko chini ya mkataba wa nani? Na je, wanamuziki wangeweza kukubali kuajiriwa na na Mlimani Park wakati huo ikiendeshwa na TTTS? Kwa vile Dar International ilikuwa ya mtu binafsi na hawakuwa na ajira yoyote ya kudumu katika bendi hiyo, haraka sana wanamuziki walikubali wazo hilo. Kesho yake viongozi wa Dar International walienda kukutana na viongozi wa ukumbi wa Mlimani Park, na wakakubaliana kuazisha kambi ya bendi mpya palepale katika ukumbi wa Mlimani. Haikuwa taabu maana vyombo vilivyonunuliwa wakati wa mkataba wa Orchestra Fukafuka vilikuwa mali ya Mlimani Park kwa hiyo bendi ilianza kwa Abel kusisitiza kupata wanamuziki kama Muhidin Gurumo,ikumbukwe kuwa ni huyu Abel ndiye aliyeisuka Dar International baada ya kuwachukua wanamuziki wote wa Safari Trippers kundi zima wakati huo, Kassim mponda, Joseph Bernard, Marijan Rajabu, Ben Peti, Zito Mbunda,Bito Elias na wengine kasoro Christian Kazinduki na kutoka Tanzania Stars ya Maggot walitoka Joseph Mulenga, George Kessy , Haruna Lwali na wengineo. Na kwa staili hiyohiyo skwadi nzima ya Dar International ikageuka kuwa Mlimani Park. Muda mfupi kabla la hili ugomvi mkubwa ulikuwa umetokea Dar International kati ya Marijani Rajabu na Abel Balthazar katika ubishi kuhusu tungo aliyoleta Marijani ambayo Balthazar alidai kuwa ni ya Tabu Ley kwa hiyo akatunge tena, jambo lililoleta kushikana mashati, na kusababisha Marijani kusimamishwa kazi. Wakati yuko benchi ndipo mpango mzima wa kuhamia Mlimani ulifanyika hivyo mwenye vyombo alilazimika kumfwata tena Marijani na kumwomba aunde bendi upya, na ndipo Super Bomboka ikaundwa.
Mlimani Park ikaanza ikiwa na Tchimanga Assossa ambaye safari ya kwenda kutafuta wanamuziki Kongo ikawa imekwisha. Na mchango wa kudumu wa Assossa wakati huo ni utunzi wa ule wimbo Gama.

Maoni 2 :

Bila jina alisema ...

Kamanda Kitime hii band kubwa sana, pls tunaomba uongeze historia ya ngide ngoma ya ukae

hamissi delgado alisema ...

miaka imepita ingi sana kwa hiyo kama ninakosea mtanisameh. Ninavyokumbuka mimi, Mponda na Ben Peti pia walikataa kwenda Mlimani Park. Hawa marehemu wote walikuwa rafiki zangu kwa hiyo nadhani niko sawa. Ben Peti ndio alikuwa mtunzi wa Magreti mama, tukiwa jobless corner Sikukuu/Agrey