LAPF

LAPF
LAPF

Jumanne, 12 Oktoba 2010

Morogoro Jazz Band

Mwaka 1944 ni mwaka muhimu katika historia ya muziki wa Morogoro na Tanzania kwa ujumla. Katika mwaka huo ndipo ilipozaliwa Morogoro Jazz Band , na  katika  kijiji cha Kingolwira alizaliwa Mbaraka Mwinshehe Mwaluka. Kati ya wanachama waanzilishi wa Morogoro Jazz Band walikuweko Makala Kindamile, Joseph Thomas, Seif Ally, Daudi Ally na Shaaban Mwambe. Bendi wakati huo ilikuwa ikipiga vyombo visivyotumia umeme kama magitaa, mandolin, ukulele, banjo na ngoma za kiasili. Ndoto za wakati huo ilikuwa ni kuwa kama Dar es Salaam Jazz Band, bendi iliyokuwa juu wakati huo, Bendi hii ilipofanya ziara Morogoro, na kuja na gitaa la umeme na baadae kuja kufanya ziara nyingine wakiwa wameongeza trumpet na saxaphone ilileta changamoto kubwa kwa Morogoro Jazz nayo kujitahidi kupata vyombo hivyo. Na kweli walifanya chini juu mpaka nao wakapata vyombo hivyo. Katika miaka ya mwanzo wa uhai wa bendi hiyo Salum Abdallah pia alipitia katika bendi hiyo, japo Salum Abdallah hujulikana zaidi kwa utunzi na uimbaji lakini pia alikuwa akipiga trumpet na mandolin, Salum alihama na kwenda kuanzisha bendi yake ya Lapaloma ambayo baadae ikaja kuwa Cuban Marimba.

                                         Morogoro Jazz Kazini
Mbaraka Mwinshehe alianza kushiriki katika maonyesho ya Morogoro Jazz tangu akiwa shule, wakati huo alipenda kupiga sana filimbi katika mtindo wa ‘kwela’, mtindo huu ulitoka Afrika ya Kusini ukiwa na wapulizaji maarufu kama Spokes Mashiyan, na ulipendwa sana na vijana haswa wa shule na makundi mengi ya jiving yalikuweko katika shule za sekondari. Hivyo alishiriki akiwa mpigaji wa filimbi wakati wa wikiendi. Siku moja kwenye mwaka 1965, wakati wanamuziki wa Morogoro Jazz wakiwa wamepumzika nje ya klabu yao Mbaraka alipita akiwa na begi kubwa walipomuuliza anaenda wapi muda ule ambao anatakiwa kuwa shule, aliwaambia kuwa hataki tena shule anaenda Dar es Salaam kutafuta maisha , walimsihi alale pale klabuni kwanza awaze hatima yake. Kesho yake wanamuziki walishangaa kumkuta Mbaraka akifanya mazoezi ya gitaa kwani walikuwa wakimfahamu kama mpiga filimbi, kwa kuwa walikuwa na shida ya mpiga rhythm walimsihi aache safari ya Dar na abaki kwenye bendi kama mpiga rhythm, akakubali. Wakati huo ni wapiga trumpet, saxaphone na solo gitaa pekee waliokuwa wanalipwa kwa mwezi,wengine wote walipata posho kidogo kila lilipopigwa dansi.  Siku moja walialikwa Dar Es Salaam kwa ajili ya mashindano na Kilwa Jazz, kabla ya kuondoka Mbaraka aligoma kwenda kwa kuwa alikuwa halipwi, wazee wa bendi wakakubali kumlipa shilingi 120 kwa mwezi, mpiga solo ambaye alikuwa akilipwa sh150 akagoma kwenda Dar kwa kutetea kuwa mpiga rhythm hastahili malipo, hivyo Mbaraka akasema angepiga pia solo, bendi ikaenda Dar ikiwa na mashaka kwani Kilwa Jazz Band wakati huo ilikuwa ni tishio, na wao walikuwa wakienda bila mpiga solo. Mbaraka alilipiga vizuri sana solo katika mashindano hayo na bendi ikashinda. Akapandishwa mshara hadi shilingi 250 ambazo zilikuwa ni kiwango cha juu sana, na kuanzia hapo mpaka alipoacha bendi na kwenda kuanzisha bendi yake Super Volcano, Mbaraka akawa mpiga solo wa Morogoro Jazz Band.

Maoni 8 :

Bila jina alisema ...

John
Asante kwa kutupa kumbukumbu muhimu sana ktk tasnia ya muziki. Kikubwa kwa kupitia blog hii tafadhali nijulishe mimi na baadhi ya wadau kwa kupitia historia hii ndefu ya mafanikio ya moro jazz, ni nini SIRI YA UMOJA WA WANA KILIMANJARO BAND kulinganisha na wana moro jazz kwa maana ya mshikamano wa muda mrefu na mafanikio,ukilinganisha na muziki wa makundi ya sasa ambayo bado yanaonekana imara lakini chini ya mkeka kuna mambo mengi

moses gasana alisema ...

Kaka Kitime ahsante sana kwa habari hizi za marehemu Mbaraka. Utupatie habari zaidi za maisha yake na hata safari yake ya Nairobi ilivyokuwa mpaka mauti yake, please mukulu
Moses Gasana

Mzee wa Changamoto alisema ...

Tumewasili.

Bila jina alisema ...

Mbaraka alikuwa Lwambo wetu Watanzania. Sikiliza Mashemeji Wangapi, moja ya vibao vyake vya mwisho alivyovirekodi kabla ya kifo chake mwaka 1979, katika http://www.youtube.com/watch?v=FPenKz3-_ns

Bila jina alisema ...

Mbaraka RIP. We will never forget you.

Bila jina alisema ...

Mbaraka aliwasha moto maonyesho ya Expo 70 ya kimataifa yaliyofanyika Japan na aliporudi alitoa ule wimbo wa kueleza safari yao. Siyakumbuki maneno yake isipokuwa "Sayonara Japan..." Hata mimi nimekuwa frustrated kama mdau mmoja aliyecomment katika stori ya Salim Abdala kwa kuzunguka kutafuta nyimbo za Moro Jazz.

Bila jina alisema ...

MWINSHEHE RIP, TUMEZALIWA HATUJAKUKUTA ILA TUMEKULIA KWENYE MUZIKI WAKO, AHSANTE KWA HILO. YOU WERE THE SPECIAL ONE (ADIMU).
AHSANTE KITIME KWA STORI YA MWINSHEHE. ULISEMA "KILA SIKU SHIDA SHIDA MPAKA SIKU YA MWISHO..." HAKIKA ULINENA KWA HILO. MUNGU AKUREHEMU, THANKS AGAIN AND AGAIN FOR THE MUSIC.

Bila jina alisema ...

Nawashukuru Ndugu zangu kwa kumkumbuka Marehemu, Kipawa alichokuwa nacho Marehermu Mbaraka ni wachache sana ulimwenguni wanao barikiwa hivyo Mimi Tangu utoto wangu miaka hiyo ya sitini na sabini Mbara ndiye aliye kuwa nyota yangu ki muziki na hata Leo Naishi Nje ya Afrika lakini DVD yangu kwenye gari utasikia tu sauti za wanan muziki wangu nilio sikiza enzi hizo kule kwetu Mombasa Kenya akina moro. volcano, jamhuri, segere matata saboso na kadhalika ahsanteni nashukuru kujua kuwa siko peke yangu..Mwinshehe hoye Daima!!!!!Its one voice that will ring till the end of my days