LAPF

LAPF
LAPF

Alhamisi, 14 Oktoba 2010

Salum Abdallah na Cuban Marimba


 Salum Abdallah Yazidu-SAY

 Kushoto-Kibwana Seif, kulia Salum Abdallah. 


Cuban Marimba Band
Morogoro, moja ya miji iliyokuwa maarufu kwa burudani katika miaka ya hamsini, sitini na sabini. Watu walitoka Dar es Salaam na kufuata week end Morogoro. Hali yake ya hewa, na kuwepo kwa bendi mbili maarufu zilizokuwa na uwezo mkubwa zilifanya wafanyakazi watake kupangwa kituo cha Morogoro. Kati ya hizo bendi mbili, ilkuweko Cuban Marimba Band. Bendi hii ilikuwa ndoto ya mwanamuziki Salum Abdallah Yazidu, maarufu kama SAY. Salum Abdallah alizaliwa tarehe 5 Mei, mwaka 1928. Baba yake alikuwa mwarabu na mama yake mwenyeji wa Morogoro.. Alisoma mpaka darasa la sita pale Msamvu na akachaguliwa kuendelea na shule Dar es Salaam , maana wakati ule ililazimika kuja Dar es Salaam ili kuendelea na masomo baada ya hapo.  Pamoja na kufaulu huko baba yake aliamua abakie nyumbani kumsaidia katika shughuli za biashara. Katika kipindi hiki Salum alianza kuonyesha kupenda kwake muziki. Alifurahia sana santuri kutoka Cuba zilizokuwa maarufu kwa kuitwa kwa namba zake. Gv1, GV2, GV3 na kadhalika. Pamoja na baba yake kutokupenda aina ya muziki aliokuwa anaupenda mwanawe, aliona ni heri amnunulie gramafon ya kupigia hizo santuri. Haukupita muda mrefu Salum alitoroka kwao ili aende Cuba kujifunza muziki. Alitoroka hadi Mombasa ili apande meli kwenda Cuba, ilikuwa mwaka 1945 kulikuwa bado na vuguvugu la vita ya pili ya dunia na safari yake ikaishia Mombasa.  Baba yake alimrudisha Morogoro, akamfungulia mgahawa ili atulie , lakini Salumu alikuwa kishapata mzuka wa muziki na akawa ameanza kuhudhuria madansi na kupendezwa sana na vifaa vya Dar Es Salaam Jazz Band, wakati huo yeye na wenzie walikuwa wameanzisha kikundi ambacho kilikuwa na vyombo vya kuchonga na ngoma za kiasili wenyewe wakikiita bendi na kuipa jina, La Paloma, hili lilikuwa jina la wimbo mmoja katika santuri za GV, nyimbo hii ni nzuri kiasi cha kwamba mpaka leo bado inapigwa duniani kote, na hata kurekodiwa na wanamuziki mbalimbali akiwemo Elvis Presley aliyeingia katika anga za muziki baadae sana.  La Paloma , ilikuwa na viongozi kama Juma Said-Rais ,Abubakar Hussein- Mweka hazina, Ramadhan Salum-Katibu Mkuu, Ali Waziri –Naibu Katibu Mkuu, Salum Abdallah –Band Master.
Katika kuiona Dar Es Salaam Jazz Band, hamu ya kuwa na vyombo kama vya Dar Jazz ilikuwa kubwa kiasi cha Salum kuuza kwa siri nyumba moja wapo ya baba yake na kununua vyombo kama vya Dar Es Salaam Jazz band. Mwaka 1948 La Paloma ikawa bendi rasmi. Viongozi wake walikuwa Salum Abdallah-Kiongozi, Abubakar Hussein-Mweka Hazina, Juma Ndehele-Katibu, wanamuziki walikuwa Kibwana Seif, Juma Kilaza, Ligongo,Mgembe,Juma Kondo,Nzige, Daulinge. Kundi hili mwaka 1952 likajipa jina la Cuban Marimba Jazz Band. Kundi lilianza kuwa maarufu kiasi cha kuwa mwaka huohuo kampuni ya santuri ya Mzuri Records walikuja mpaka Morogoro kurekodi nyimbo za bendi hii.  Bendi iliendelea na umaarufu mkubwa mpaka kwenye miaka ya 70. Salum Abdallah alifariki katika ajali ya gari, ambapo taa za gari lake zilizimika ghafla akiwa katika mwendo na gari lake likatoka nje ya barabara na kumtupa nje akapasuka kibofu na kufariki siku hiyo. Ilikuwa tarehe 19 Novemba 1965.
(Picha kwa hisani ya Jumaa R. R. Mkabarah)

Maoni 14 :

Webmaster Kalley A.P alisema ...

Kwa kweli JK hii Historia ya Salum Abdalla nimeipenda sana ukizingatia hata mimi namkubali kwa vibao vyake vikali vilivyokuwa vikileta ushindani na Moro Jazz chini ya Mbaraka Mwinshehe na kufanya kuwa kama Simba na Yanga. Pia nakumbuka uliwahi kusema kwamba Salum Abdalla aliwahi kupigia Moro Jazz.

Sebastian Ritte alisema ...

What a great story...sad ending with damn car accident to those Morogoro legends!

Nadabi alisema ...

Natamani vibao vyake maarufu kama wangu ngaiye ngoma iko hukuuuuu,shemeji shemeji huku mwazima taaaaaaa...wanawakeee..tanzaniaaaa etc
He was great bana!

Bila jina alisema ...

Msikilize SAY katika linki hii:
http://www.youtube.com/watch?v=edgPJr1y5vg&feature=related

Bila jina alisema ...

Hii blog mbona inasuasua tangu ihamie hapa kutoka mwakitime.blogspot.com? Naona ni wiki sasa hakuna kilichobadilika humu na wachangiaji ni wachache mno. Kulikoni?

Bila jina alisema ...

Japo ni kazi kubwa kutafuta ama kuandika mada, bila shaka wachangiaji hawakuvutiwa na mada yenyewe. Tumpe nafasi huenda akaja na JAMBO JIPYA NA ZURI SANA

Perez alisema ...

Mpenzi wangu utaniponza,
Mpenzi wangu utaniponza we,
Mpenzi wangu utaniponza mama kwa mambo unayoyafanya.

Mpenzi watuchonganisha,
Mimi na yule ni rafiki,
Wewe watugombanisha ee mpenzi utaniumiza.

Wajaribu kunidanganya,
Wanambia yule Mungu mwana,
Kumbe pambeni ni wako bwana ee mpenzi utaniumiza.

Kule ulisema yule kaka,
Kumbe mafuta ulinipaka,
Pembeni huwa hekaheka ee na vitanda kuvunjika.

Shemeji shemeji huku mwazima taa………….
Shemeji shemeji huku mwazima taa………..

Shemeji shemeji huku mwazima taa mama,

Shemeji shemeji huku mwazima taa…..

Ushemeji wa Urongo mmie sitaki,

Shemeji shemeji hukumwazima taa…….

Huyu ni shemeji yako mwazimia nini taa,

Shemeji shemeji huku mwazima taa…….

Muna singizia ati luku imekwisha(Hii anaongezeaga KITIME hii),

Shemeji ahemeji huku mwazima taa…….

Yaani! We acha tu

Bila jina alisema ...

Hii ni kwikwi sii bure

emu-three alisema ...

Tunashukuru kwa kutupa hazina hizi, na hazina kama hizi zilikuwa zimefukiwa, na wewe umefanya jitihada ya kuzifukua na kuziweka hewani ili zilete thamani yake. Tunashukuru sana sana.
Kwa nyongeza tu kama inawezekana, basi kila ukitoa historia ya mmojawapo weka wimbo wake, sijui kama unaweza kuingiza yotube..nk, ili usome huku unaisikia kazi yake!
Hongera kwa mabadiliko na muonekano mpya.

Bila jina alisema ...

Mwaka 1965, nilkuwa shule ya msingi. Lakini nakumbuka nilipotoka shule (probably siku ya pili baada ya msiba) nakumbuka nilimwona mama mmoja jirani yetu analia. Nakumbuka niliambiwa kuwa alikuwa analia kwa kuwa Salim Abdallah amefariki dunia. Pia nakumbuka kuwa baada ya hapo nyimbo zake zilikuwa zinapigwa sana Radio Tanzania (k.m. Wanawake Tanzania, Shemeji shemeji huku wazima taa, Mheshimiwa JK Nyerere TANU imemaliza ukoloni, Ngoma iko huku...). Tragically, genius mwingine Mmorogoro mwenzake Salim Abdalla, yaani Mbaraka Mwinshehe, alifariki dunia takriban miaka 13 baadaye katika ajali ya gari Kenya. Gone but not forgotten. Hatutawasahau.

Bila jina alisema ...

John, Nakumbuka ule wimbo wa Salim Abdala "Hapo zamani tulipata taabu sana---" [maneno yake nimeyasahau lakini ulikuwa wimbo wa kukisifu chama cha tanu] SAY alitumia mtindo wa uimbaji wa 'country' uitwao 'yodelling'. Kwa maoni yangu katika 60's na 70's fani ya uimbaji Afrika Mashariki ilikuwa ni sanaa hasa na wanamuziki walikuwa wanajaribu mitindo mingi sana [Afro-Latino, Country, western, rock, soul, blues, nyimbo na staili za uimbaji wa asili wa jamii zetu za jadi, kwela n.k.] tofauti na sasa ambapo staili ni tatu tu, R n' B, Rap na ndomoloo.

Bila jina alisema ...

Perez, huo wimbo "Shemeji shemeji huku wazima taa" ninayo katika CD ya wanamuziki mbalimbali wa TZ wa miaka ya 1960s. Cha ajabu ni kuwa CD hiyo nilinunua ughaibuni (UK). Hapa TZ nimetafuta sana CD au kanda za miaka hiyo za Salim Abdallah, Western Jazz, Dar Jazz, Kilwa Jazz, Kiko Kids, Moro Jazz bila mafanikio. Kila nikiuliza naambiwa niende Radio Tanzania (TBC). Je kuna duka lolote hapa Dar ambako naweza kununua CD/kanda hizo????? Jimmy.

Bila jina alisema ...

JK, Kama sikosei, Juma Kilaza alikuwa mjombaake (au binamu upande wa mama?) Salim Abdala, na yeye ndio alichukua uongozi wa Cuban Marimba baada ya kifo cha SA. Wakati huo mimi nilikuwa Primary school kwa hivyo vitu vingi sana nimevisahau. Kama kuna mtu anaweza kutukumbusha. Pili, nakumbuka kulikuwa na kitabu cha maisha ya SA katika miaka ya 70 ambacho, kama sikosei, jaladani kilikuwa na picha hiyo ya kwanza hapa juu. Tatu, ingelikuwa vyema kama BAMUTA lingekuwa na mradi wa kutoa vitabu kuhusu maisha ya wasanii wa zamani kama vile Hanzuruni, Michael Enoch, Ahmed Kipande, Mbaraka Mwinshehe Daudi Makwaia, Patrick Balisidya, n.k. kabla vyanzo vya kumbukumbu havijatoweka. Kwa kiasi kikubwa Shaaban Robert amechangia kuweka kumbukumbu ya Siti binti Sadi hai kupitia kitabu chake 'Wasifu wa Siti binti Saada'.

Bila jina alisema ...

Story nzuri sana na nimuhimu vijana kujua historia ya muziki Nchini kwamba ni kubwa na ndefu yenye mizizi mirefu. Tanzania ilikuwa na muziki wake na bado inagundua muziki wake. Ubunifu bado upo katika damu ya wajukuu wa wakongwe hao. Je nachouliza kulikoni haturudii miziki hii na kuikarabati katika style za sasa ili ziuzike. Hili linafanywa na vizazi vyote duniani kama namna ya kuvienzi vizazi vilivyopita na pia namna na ku-reintroduce muziki huo kwa vizazi vya sasa. Kinachotokea ni muziki huo kupigwa kwa kuigwa (maranyingi kwa ubora wa hali ya chini sana- kiasi kwamba iwapo wakongwe hao watafufuka wanaweza kupiga marufuku bendi hizo zisiupige tena muziki wao)na bendi za usiku ambao hauwafikii wananchi wengi kama vile ungepatikana katika radio, tv, video nk.
Mkongwe hebusaidia hapo tufanyenye hapa? Natamani ningekuwa najua kupiga muziki kama wewe/nyie hilo ningelifanya kwa ukweli kabisa!!!