LAPF

LAPF
LAPF

Ijumaa, 29 Oktoba 2010

Muziki wa Taarab

Taarab ina historia ndefu katika muziki wa Tanzania kama ulivyokuwa muziki wa dansi. Wapenzi wa taarbu wa zamani waliiweka taarabu katika vyanzo kama Taarab ya Tanga, Taarab ya Dar es Salaam,Taarab ya Zanzibar na Taarab ya Mombasa. Taarab ya Zanzibar wakati huo ilikuwa ni ile yenye kundi kubwa la wanamuziki, kwa kufuata mfumo wa muziki huo kama ulivyokuwa ukipigwa huko Misri. Historia inatueleza kuwa Sultan  Sayyid Barghash wa Zanzibar kwenye mwaka 1870, alipeleka wanamuziki wake wawili kwenda Misri kupata taaluma ya upigaji wa Taarab , na waliporudi ndipo mwaka 1905 wakaanzisha klab ya Ikwaan Safaa, kundi ambalo pamoja na kupitia misukosuko mingi ya kisanii na hata kisiasa, lipo mpaka leo. Na muziki wa kundi hili na makundi mengine yalifuata aina hii ya muziki kwa muda mrefu, ulikuwa unajumuisha kundi kubwa la wanamuziki wenye vifaa mbalimbali kitaalam wanaweza kuitwa orchestra.  Taarab ya Dar es Salaam haikupishana sana na ile ya Zanzibar wakati huo, hapa Dar kukiwa na vikundi kama Egyptian Musical Club na Alwatan Musical Club vilivyoanza tangu kwenye miaka ya 30. Mombasa ilijulikana sana kwa aina yake ya Taarab iliyofanywa maarufu na akina Juma Bhalo waliokuja na upigaji ulioiga mipigo ya muziki wa kihindi, uliopata umaarifi kutokana na sinema za kihindi. Ukisikiliza nyimbo maarufu za Juma Bhalo kama Pete, utasikia uimbaji upigaji na upangaji zauti unaofanana sana na muziki wa kihindi. Taarab ya Tanga kwa kweli ndio ilistahili kuitwa modern taarab, taarab hii ndio ilikuwa ya kwanza kuanza kuingiza vifaa ambavyo vilikuwa vigeni katika taarabu, magitaa, akodian , na mipigo ya ngoma za kiasili, na pia vikundi vya Tanga vilikuwa vidogo vikiwa na washirika wa wastani wa watu kumi na mbili. Kazi za Black Star na Lucky Star wengi tunazijua na waimbaji wake maarufu kama Bi Shakila, Hasmahani sauti zao zilitawala anga ya muziki huu katika miaka ya sabini..
Katika anga za leo kuna vikundi vingi vinavyotangaza vinapiga muziki wa taarabu, jambo ambalo limepingwa na wengi kuwa kinachopigwa pigwa sasa si taarabu, kuna hata waliofikia kusema kwa vyovyote vile kinachoitwa  mipasho hakina uhusiano wowote na taarab!!

Alhamisi, 14 Oktoba 2010

Salum Abdallah na Cuban Marimba


 Salum Abdallah Yazidu-SAY

 Kushoto-Kibwana Seif, kulia Salum Abdallah. 


Cuban Marimba Band
Morogoro, moja ya miji iliyokuwa maarufu kwa burudani katika miaka ya hamsini, sitini na sabini. Watu walitoka Dar es Salaam na kufuata week end Morogoro. Hali yake ya hewa, na kuwepo kwa bendi mbili maarufu zilizokuwa na uwezo mkubwa zilifanya wafanyakazi watake kupangwa kituo cha Morogoro. Kati ya hizo bendi mbili, ilkuweko Cuban Marimba Band. Bendi hii ilikuwa ndoto ya mwanamuziki Salum Abdallah Yazidu, maarufu kama SAY. Salum Abdallah alizaliwa tarehe 5 Mei, mwaka 1928. Baba yake alikuwa mwarabu na mama yake mwenyeji wa Morogoro.. Alisoma mpaka darasa la sita pale Msamvu na akachaguliwa kuendelea na shule Dar es Salaam , maana wakati ule ililazimika kuja Dar es Salaam ili kuendelea na masomo baada ya hapo.  Pamoja na kufaulu huko baba yake aliamua abakie nyumbani kumsaidia katika shughuli za biashara. Katika kipindi hiki Salum alianza kuonyesha kupenda kwake muziki. Alifurahia sana santuri kutoka Cuba zilizokuwa maarufu kwa kuitwa kwa namba zake. Gv1, GV2, GV3 na kadhalika. Pamoja na baba yake kutokupenda aina ya muziki aliokuwa anaupenda mwanawe, aliona ni heri amnunulie gramafon ya kupigia hizo santuri. Haukupita muda mrefu Salum alitoroka kwao ili aende Cuba kujifunza muziki. Alitoroka hadi Mombasa ili apande meli kwenda Cuba, ilikuwa mwaka 1945 kulikuwa bado na vuguvugu la vita ya pili ya dunia na safari yake ikaishia Mombasa.  Baba yake alimrudisha Morogoro, akamfungulia mgahawa ili atulie , lakini Salumu alikuwa kishapata mzuka wa muziki na akawa ameanza kuhudhuria madansi na kupendezwa sana na vifaa vya Dar Es Salaam Jazz Band, wakati huo yeye na wenzie walikuwa wameanzisha kikundi ambacho kilikuwa na vyombo vya kuchonga na ngoma za kiasili wenyewe wakikiita bendi na kuipa jina, La Paloma, hili lilikuwa jina la wimbo mmoja katika santuri za GV, nyimbo hii ni nzuri kiasi cha kwamba mpaka leo bado inapigwa duniani kote, na hata kurekodiwa na wanamuziki mbalimbali akiwemo Elvis Presley aliyeingia katika anga za muziki baadae sana.  La Paloma , ilikuwa na viongozi kama Juma Said-Rais ,Abubakar Hussein- Mweka hazina, Ramadhan Salum-Katibu Mkuu, Ali Waziri –Naibu Katibu Mkuu, Salum Abdallah –Band Master.
Katika kuiona Dar Es Salaam Jazz Band, hamu ya kuwa na vyombo kama vya Dar Jazz ilikuwa kubwa kiasi cha Salum kuuza kwa siri nyumba moja wapo ya baba yake na kununua vyombo kama vya Dar Es Salaam Jazz band. Mwaka 1948 La Paloma ikawa bendi rasmi. Viongozi wake walikuwa Salum Abdallah-Kiongozi, Abubakar Hussein-Mweka Hazina, Juma Ndehele-Katibu, wanamuziki walikuwa Kibwana Seif, Juma Kilaza, Ligongo,Mgembe,Juma Kondo,Nzige, Daulinge. Kundi hili mwaka 1952 likajipa jina la Cuban Marimba Jazz Band. Kundi lilianza kuwa maarufu kiasi cha kuwa mwaka huohuo kampuni ya santuri ya Mzuri Records walikuja mpaka Morogoro kurekodi nyimbo za bendi hii.  Bendi iliendelea na umaarufu mkubwa mpaka kwenye miaka ya 70. Salum Abdallah alifariki katika ajali ya gari, ambapo taa za gari lake zilizimika ghafla akiwa katika mwendo na gari lake likatoka nje ya barabara na kumtupa nje akapasuka kibofu na kufariki siku hiyo. Ilikuwa tarehe 19 Novemba 1965.
(Picha kwa hisani ya Jumaa R. R. Mkabarah)

Jumanne, 12 Oktoba 2010

Morogoro Jazz Band

Mwaka 1944 ni mwaka muhimu katika historia ya muziki wa Morogoro na Tanzania kwa ujumla. Katika mwaka huo ndipo ilipozaliwa Morogoro Jazz Band , na  katika  kijiji cha Kingolwira alizaliwa Mbaraka Mwinshehe Mwaluka. Kati ya wanachama waanzilishi wa Morogoro Jazz Band walikuweko Makala Kindamile, Joseph Thomas, Seif Ally, Daudi Ally na Shaaban Mwambe. Bendi wakati huo ilikuwa ikipiga vyombo visivyotumia umeme kama magitaa, mandolin, ukulele, banjo na ngoma za kiasili. Ndoto za wakati huo ilikuwa ni kuwa kama Dar es Salaam Jazz Band, bendi iliyokuwa juu wakati huo, Bendi hii ilipofanya ziara Morogoro, na kuja na gitaa la umeme na baadae kuja kufanya ziara nyingine wakiwa wameongeza trumpet na saxaphone ilileta changamoto kubwa kwa Morogoro Jazz nayo kujitahidi kupata vyombo hivyo. Na kweli walifanya chini juu mpaka nao wakapata vyombo hivyo. Katika miaka ya mwanzo wa uhai wa bendi hiyo Salum Abdallah pia alipitia katika bendi hiyo, japo Salum Abdallah hujulikana zaidi kwa utunzi na uimbaji lakini pia alikuwa akipiga trumpet na mandolin, Salum alihama na kwenda kuanzisha bendi yake ya Lapaloma ambayo baadae ikaja kuwa Cuban Marimba.

                                         Morogoro Jazz Kazini
Mbaraka Mwinshehe alianza kushiriki katika maonyesho ya Morogoro Jazz tangu akiwa shule, wakati huo alipenda kupiga sana filimbi katika mtindo wa ‘kwela’, mtindo huu ulitoka Afrika ya Kusini ukiwa na wapulizaji maarufu kama Spokes Mashiyan, na ulipendwa sana na vijana haswa wa shule na makundi mengi ya jiving yalikuweko katika shule za sekondari. Hivyo alishiriki akiwa mpigaji wa filimbi wakati wa wikiendi. Siku moja kwenye mwaka 1965, wakati wanamuziki wa Morogoro Jazz wakiwa wamepumzika nje ya klabu yao Mbaraka alipita akiwa na begi kubwa walipomuuliza anaenda wapi muda ule ambao anatakiwa kuwa shule, aliwaambia kuwa hataki tena shule anaenda Dar es Salaam kutafuta maisha , walimsihi alale pale klabuni kwanza awaze hatima yake. Kesho yake wanamuziki walishangaa kumkuta Mbaraka akifanya mazoezi ya gitaa kwani walikuwa wakimfahamu kama mpiga filimbi, kwa kuwa walikuwa na shida ya mpiga rhythm walimsihi aache safari ya Dar na abaki kwenye bendi kama mpiga rhythm, akakubali. Wakati huo ni wapiga trumpet, saxaphone na solo gitaa pekee waliokuwa wanalipwa kwa mwezi,wengine wote walipata posho kidogo kila lilipopigwa dansi.  Siku moja walialikwa Dar Es Salaam kwa ajili ya mashindano na Kilwa Jazz, kabla ya kuondoka Mbaraka aligoma kwenda kwa kuwa alikuwa halipwi, wazee wa bendi wakakubali kumlipa shilingi 120 kwa mwezi, mpiga solo ambaye alikuwa akilipwa sh150 akagoma kwenda Dar kwa kutetea kuwa mpiga rhythm hastahili malipo, hivyo Mbaraka akasema angepiga pia solo, bendi ikaenda Dar ikiwa na mashaka kwani Kilwa Jazz Band wakati huo ilikuwa ni tishio, na wao walikuwa wakienda bila mpiga solo. Mbaraka alilipiga vizuri sana solo katika mashindano hayo na bendi ikashinda. Akapandishwa mshara hadi shilingi 250 ambazo zilikuwa ni kiwango cha juu sana, na kuanzia hapo mpaka alipoacha bendi na kwenda kuanzisha bendi yake Super Volcano, Mbaraka akawa mpiga solo wa Morogoro Jazz Band.

Jumatatu, 11 Oktoba 2010

Matangazo ya Magazeti


Matangazo ya bendi za muziki zamani yalikuwa na vituko vyake katika upangaji na pia maelezo yake. Magazeti maarufu kwa matangazo yalikuwa ni Uhuru ambalo lilikuwa gazeti la kila siku na magazeti ya kila wiki kama Mzalendo, Mfanyakazi, Heko na kadhalika. Pichani  ni matangazo ya Bendi ya OSS wakati huo wakiwa na mtindo wa Masantula Ngoma ya Mpwita, kama  tangazo linavyoonyesha kikosi hicho kilikuwa na Ngalula na Frida wakiwa kwenye kucheza show, Mottoo mpiga tumba, King Kiki kwenye uimbaji, Otrishi mpiga rhythm, Kalala Mbwebwe na Kabeya Badu waimbaji, Hatibu Iteytey katika kupuliza saxophone. Pembeni kuna tangazo la Kyauri Voice wakiwa na mtindo wa Katakata mwendo wa jongoo, wanamuziki wakiwemo Mbwana Cocks kwenye gitaa, na Belela Kabaa kwenye bezi. Vijana Jazz watoto wa nyumbani, hapa tunawaona Hassan Shaw kwenye kinanda. Hili jina ‘Watoto wa nyumbani’ lilikuja kutokana na kuweko na ushindani mkubwa kati ya bendi za kikongo wakati huo na zile zenye wanamuziki waKitanzania watupu, kama unakumbuka Vijana Jazz walitunga hata wimbo kuwananga wenzao waliokuwa wakijichubua na kusuka nywele ……oo ni mwanaume gani anapaka wanja, naomba ujirekebishe, ohh ni mwanaume gani anasuka nywele, naomba ujirekebishe, oo ni mwanaume gani ana paka Ambi…... UDA Jazz na mtindo wa Bayankata , enzi za John Kijiko kwenye  solo, Chipembele(Bob Chipe) kwenye drums, Forty kwenye rhythm. Na Juwata Jazz wakikuletea Msondo ngoma Magoma Kitakita.

Ijumaa, 8 Oktoba 2010

The Upanga Story - The Strokers

The Strokers, hili lilikuwa kundi jingine la wanamuziki wa Upanga. The Strokers lilikuwa na awamu mbili, ya kwanza ilikuwa na wanamuziki akina Donald Max, David Max, Harry Chopeta, Vincet Chopeta, Pino Makame na Ochiwa na Freddy Lukindo. Awamu ya pili ya kundi hili ilikuwa na Sajula Lukindo,Onesmo Kibira,Innocent Galinoma,Ben Galinoma, Denis Pad,Francis Kasambala,Vicent na Harry Chopeta, Ally Mwarabu, Sabri Mmanga na wengineo. Pichani ni awamu ya kwanza ya Strokers. Waliosimama, Pino Makame, Freddie Lukindo, David Max. Waliokaa (?),Harry Chopeta, Vincet Chotepa.

Upanga Story extra

Picha hii ina maana nyingi kwa wapenzi wa Groove Makers. Hapa ni wakali wawili wa GrooveMakers wakiwa katika mazoezi ya Karate. Hakuna zawadi kwa kuwataja japo itakuwa vizuri kupata taarifa ya kipindi hiki

Jumatatu, 4 Oktoba 2010

Intimate Rhumba

Mwishoni mwa miaka ya themanini, lilitengenezwa kundi lililokusanya wanamuziki mahiri wa Kitanzania na Kikongo na kuunda bendi iliyoitwa Intimate Rhumba, kundi hili halikukaa muda mrefu wala halikuweza kurekodi. Baadhi ya wanamuziki waliokuwemo katika kundi hili wanaimani kuwa  bendi yao iliuwawa kwa kutumia uchawi. Wana amini walionekana ni tishio mno kwa kundi lililokuwa na ukaribu nao la Ndekule na hivyo kufanyiwa ulozi na kuvunjika. Pichani ni Intimate Rhumba wakiwa jukwaani kati yao wa kwanza kushoto Mawazo Hunja, watatu Kabeya Badu, King Kiki, mwisho na Joseph Mulenga

Ijumaa, 1 Oktoba 2010

Sikujua kama utabadilika - Simba wa Nyika


Wengi tunaufahamu wimbo Sikujua Kama Utabadilika, wenye maneno yafuatayo....
Ohhh Sikujua kama utabadilika
Ohhh Ulimwengu kweli una mambo mengi
Baki salama oo kuonana nawe ni majaliwa
Chorus
Utalia utalia ooo usinione, Mombasa mbali, Kakamega mbaali......................
Wimbo huu ulitungwa na Wilson Peter kama kijembe, baada ya mpiga rythm wa Simba Wa Nyika, Prof. Omar Shaaban kwenye mwaka 1978 kuondoka na karibu kundi zima la Simba wa Nyika na kwenda kuanzisha Les Wanyika ambao nao waliokuja na vibao vikali sana katika album yao ya Sina Makosa.
Western Jazz Band

Mzee Iddi Nhende ndiye aliyepata wazo la kuanzisha bendi maarufu ya Western Jazz. Iddi Nhende alianza muziki akiwa bado mdogo katika bendi ya shule alipokuwa Primary huko Nzega, mwaka 1944 alijiunga na Tabora Boys Secondary na hapa akajiunga na Brass Band ya shule ambapo alikuwa mpigaji wa Cornet. Alimaliza shule na kuja Dar es Salaam kujiunga na Chuo cha Afya, Sewa Haji Medical Training Center. Baada ya kumaliza mafunzo akaajiriwa Bohari ya madawa na kisha mwaka 1957 alihamishiwa Muhimbili. Upenzi wake wa muziki ulimfanya mwaka huohuo ajiunge na Rufiji Jazz Band kama mpiga trumpet, bendi hii wakati huo ilikuwa ikifanya maonyesho yake Minazini Community Centre iliyokuwa eneo linaloitwa siku hizi Mchikichini na pia walikuwa wakipiga muziki katika ukumbi wa Arnatougro.
Kutokana na miji kuwa ndio ilikuwa inaanza, watu wengi kutoka maeneo mbalimbali walihamia mijini na kujaribu kutafuta wenzao waliotoka sehemu moja na kuwa na vikundi vya kusaidiana au kuwaunganisha, watu wa sehemu mbalimbali walianzisha bendi wakazipa majina ya wanakotoka, hivyo waanzilishi wa Rufiji Jazz walitoka Rufiji, na ndivyo ilivyokuwa kwa Kilwa Jazz, Ulanga jazz na kadhalika. Hivyo Iddi Nhende aliyekuwa ametoka Nzega akaamua kuanzisha bendi ya watu kutoka Magharibi, kwa kuwa nchi ilikuwa imegawanywa katika majimbo, yakiweko majimbo kama Northern Province, Southern Highlands Province, Western Province na kwa vile Nhende alitoka Western province akaanzisha Western Jazz Band 1959. Akanunua vyombo aina ya Grampian toka duka la Souza Junior duka la vyombo vya muziki lililokuwepo mtaa wa Mkwepu. Aliweza kupata fedha baada ya kuuza ng’ombe kadhaa wa mamake. Wakati huo katika bendi za aina yake ni Dar es Salaam Jazz Band peke yake waliokuwa na magitaa ya umeme, hivyo Nhende akawa na kazi ya kuwatafuta wapigaji ambapo alimfuata mpiga gitaa la umeme wa kwanza Haus Dibonde(Msukuma), aliyekuwa anapigia Dar es Salaam Jazz Band(hii ilikuwa chini ya Mzee Muba), baada ya hapo akawapata wanamuziki wengine kutoka Ulanga Jazz Band, wakati huo chombo cha banjo kilikuwa muhimu hivyo akamtafuta mpiga banjo toka Cuban Marimba tawi la Dar es Salaam. Cuban Marimba wakati huo ilikuwa na tawi Dar Es Salaam lililokuwa chini ya Mzee Mwaipungu. Mwaka mmoja baadae alipata transfer ya kwenda Morogoro, hivyo huku nyuma alilazimika kuongeza wasanii ili kuimarisha bendi wakati hayupo. Akampata David Makwaya mwimbaji, na Ally Rashid(huyu ameacha muziki karibuni akiwa Msondo), mpiga Saxaphone toka Zanzibar. Bahati mbaya yule mpiga gitaa Haus akapata kichaa katika mazingira yaliyohusishwa na ushirikina kutokana na ushindani wa bendi uliokuwepo. Hivyo basi walifuatwa wanamuziki watatu toka Tabora Jazz, wanamuziki hao walikuwa wametoka pamoja katika bendi iliyokuwa na makazi Mwanza ikiitwa Kimbo Twist Band na wakahamia Tabora Jazz, na kutoka hapo wakachukuliwa na Western Jazz. Wanamuziki hao walikuwa
Rashid Hanzuruni, Kassim Mponda na Omary Kayanda. Baada ya kazi nzuri sana, Hanzuruni Nae akarukwa na akili katika mazingira yale ya yule mpiga solo wa kwanza akalazimika kurudishwa Tabora ambako alikaa mpaka mauti yake. Wema Abdallah akachukua nafasi ya mpiga solo katika bendi ya Western. Tatizo la kinidhamu lilifanya Wema aondolewe Western, na mpigaji mwingine mzuri sana Shamba Abbdallah akachukua nafasi, solo la huyu bwana linasikika kwenye nyimbo ka Rosa na kadhalika.
Hall la nyumbani la Western Jazz lilikuwa Alexander Hall, ambalo lilikuja kuwa hall la DDC Kariakoo. Western walinunua drums baada ya Kilwa Jazz kununua drums na kuzipitisha kwao kuwaringia. Walinunua toka kwa bendi moja ya Wagoa iliyoitwa De Mello Brothers. Western walirekodi santuri kadhaa chini ya mkataba waliyousaini na lebo ya Phillips ya Kenya. Hatimae Western na mtindo wao wa Saboso walitoweka katika anga za muziki miaka ya mwisho ya sabini. Kati ya nyimbo zao nyingi ni hizi hapa; Rosa, Vigelegele, Jela ya Mapenzi, Helena no 1 na 2.

Maneno Uvuruge 2


Katika kipindi ambapo Maneno Uvuruge alikuwa akipigia Super Rainbow ndipo Eddy Sheggy na Emma Mkello walipojiunga, hawa hukumbukwa sana kwenye bendi hii kwa ajili ya ule wimbo Milima Ya Kwetu, pia nae Banza Tax akajiunga kipindi hiki. Na kule Mabibo bendi ya Mambo Bado ilipata msukosuko na kuvunjika kwa mara ya kwanza na hivyo wanamuziki wake Juma Choka mpiga drums, Lodji Mselewa na Nana Njige pia wakajiunga na kundi na Super Rainbow, lakini hawakukaa sana Assossa aliweza kuifufua tena Mambo Bado na wote wakarudi wakifuatana na Maneno Uvuruge. Lakini tayari bendi ilikuwa iko katika hali mbaya kwani Assossa aliacha tena akiwa katika harakati ya kuunda bendi mpya na Mambo Bado ikafa rasmi. Juma Choka akamtaarifu Maneno kuwa Urafiki Jazz kuna nafasi ya kazi na hapo akenda na kusailiwa na Ngulimba wa Ngulimba, Marehemu Mzee Juma Mrisho, Urafiki nayo ilikuwa katika siku zake za mwisho lakini bado yule mpiga solo mahiri Michael Vicent alikuweko. Kipindi hiki pia waliingia Mohamed Gota gota na Hussein Jumbe. Maneno Uvuruge sasa alianza kufahamika kwa wanamuziki wengine kuwa ana uwezo mkubwa na bendi zikaanza kumsaka, na kuanzia hapo amekuwa hatafuti kazi bali anatafutwa. Bendi ya kwanza kumchukua ilikuwa ni Maquis, alichukuliwa ili awe mpiga gitaa la rhythm, aliwakuta wapiga rhythm wawili, huko, Mbwana Cox na Makuka. Akawa mwanamuziki wa Maquis wakati huo wapiga solo wa bendi hiyo walikuwa ni Nguza Viking, na Mzee Lubaba.
Mwanamuziki Belly Kankonde akakutana na Marehemu Mzee Mwendapole na kuamua kuipa uhai bendi ya Afrisongoma. Kankonde akawashawishi wanamuziki wenzie wanne wa Maquis, Maneno Uvuruge (guitar),Kiniki Kieto(mwimbaji), Comson Mkomwa(saxophone) na Keppy Kiombile(bass) wakahamia Afrisongoma. Maneno hakukaa muda mrefu kwani Nguza alimfuata yeye na Comson na kuwarudisha Maquis , na kwa kuwa walikuwa wamekwishapokea fedha za Mzee Mwendapole kesi ilifika polisi na ikalazimu Maquis warudishe fedha hiyo. Lovy Longomba alijiunga na Maquis nae hakukaa muda mrefu Mwendapole akamshawishi akaunde upya kundi la Afrisongoma ambalo katika awamu ya kwanza liliishia kurekodi mara moja na kutokuwa na maendeleo. Lovy pia tena akamuondoa Maneno na kuhamia nae Afrisongoma.
Wakati huo Mosesengo Fan Fan yule mpiga gitaa mahiri aliyetoka kwa Franco na kupigia Matimila na Makassy alikuwa amehamia Uingereza na akawa amemtaka Kiniki Kieto awashawishi Maneno Uvuruge, Keppy Kiombile, na Vivi Kapaya wamfuate,lakini mpango huo uliishia kwa Kiniki na Vivi kuendelea na Fanfan wakati Maneno na Keppy wakahamia Afrisongoma wakiwa na Lovy. Wanamuziki kadhaa walihamia Afriso wakati huo wakiwemo Kalamazoo, na Mzee Mponda ambae baada ya kutoka Msondo alikuwa kapita Sikinde na akatua Afrisongoma. Na hapo ndipo msondo wakamchukua Maneno kwa mara ya kwanza. Alikaa kwa muda na rafiki zake akina Benno Vila Anthony wakaweza kumshawishi ahamie Sikinde. Baada ya muda si mrefu Nguza akamfuata ili kumshawishi ajiunge na Orchestra Sambulumaa. Ilikuwa ni ushawishi wa Skassy Kasambula na Emmanuel Mpangala aliyekuwa mkurugenzi wa bendi ndio ulioweza kumfanya Maneno ahamie Sambulumaa (itaendelea………) (Pichani...Keppy Kiombile Bass, Maneno Uvuruge Rythm, Makuka Second solo, Juma Choka Drums, Lubaba Solo....)

Maneno Uvuruge

Maneno Uvuruge ni moja ya wanamuziki waliotoka katika familia ya wanamuziki ya ukoo wa Uvuruge. Kaka zake Jumanne, Stamili, na Huluka ni kati ya wapiga magitaa walioheshimika sana katika jamii ya wanamuziki wa bendi Tanzania.
Jumanne Uvuruge ambae alikuwa mkubwa wa akina Uvuruge wote, ndie aliyetunga kibao maarufu cha Georgina, kilichopigwa na Safari Trippers na kuimbwa na Marijani Rajabu. Siku zake za mwisho za maisha Jumanne alikuwa anajishughulisha na kupata riziki yake kwa kuzunguka katika mabaa mbalimbali na gitaa na kupiga maombi mbalimbali ya wanywaji, na kisha kuhama na kuelekea baa nyingine. Hayakuwa maisha rahisi.
Maneno Uvuruge hana kumbukumbu ya jinsi gani Jumanne alijifunza gitaa, lakini anajuwa kuwa Stamili alifundishwa na Jumanne. Anakumbuka zaidi jinsi Huluka alivyojifunza kwani ndie alikuwa kaka yake waliefuatana kuzaliwa. Huluka alijifunza gitaa kwa kuanza kuchonga gitaa lake mwenyewe, aliiba mishipi ya kuvulia ya baba yake na ndio zikawa nyuzi za gitaa lake, siku babake alipogundua wizi huo alivunja vunja gitaa na kumkataza asiguse mishipi yake tena, lakini akamwelekeza inakonunuliwa, Huluka alitafuta pesa na kwenda kununua mishipi na kuendelea na gitaa lake la kopo. Wakati huo Huluka alikuwa anasoma, naye Maneno akaanza hamu ya kutaka kujua kupiga gitaa akawa anaiba gitaa la kaka yake kila alipoenda shule, ilikuwa ni ugomvi kila alipokata nyuzi kwani alikuwa bado anajifunza. Jumanne na Stamili wakaanza rasmi kumfundisha gitaa Huluka nae akalijua vizuri sana. Si muda mrefu baadae nae akaanza rasmi kumfundisha mdogo wake. Maneno anasema wimbo wa kwanza kakake kumfundisha ni ile rhythm ya wimbo Novelle Geneation wa Orchestra Lipualipua, wimbo huu ulikuwa ni kipimo muhimu kwa wapiga rythm enzi hizo. Freddy Benjamin ndie aliyemshauri kujiunga na Bendi. Alimkaribisha UDA Jazz ambako alikuwa akiimbia na pamoja na kuweza kupiga gitaa alifanyiwa mizengwe na mpiga rhythm aliyekuweko na ambae pia alikuwa katibu wa bendi. Freddy alimuombea kazi Super Rainbow iliyokuwa na makao yake makuu pale Sunlight Bar Mwananyamala B. Na hapo akakutana na wanamuziki kama Hatibu Iteytey, Nuzi Ndoli, Rocky, Mzee Bebe, Akina Eddy Sheggy walikuwa bado hawajajiunga na bendi hii wakati huo.(Picha ya juu akiwa na Mohamed Shaweji, ya chini akiwa na Mawazo Hunja)

Kassim Mponda

Kassim Mponda alikuwa mmoja ya wapiga gitaa mahiri hapa Tanzania. Kama unakumbuka wimbo utunzi wa Kakere, wa Sogea Karibu uliopigwa na JUWATA ambao pia ulipambwa na kinanda cha Waziri Ally aka Kissinger, basi lile ndio solo la Kassim Mponda. Kwa kifupi alianzia Nyanyembe Jazz, akahamia Tabora Jazz,na kupitia Police Jazz Band Wana Vangavanga, Safari Trippers ,mbapo alihama na wenzie na kuanzisha Dar International, kisha akahamia Msondo, akapitia Shikamoo Jazz, hatimae mwanae akamnunulia vyombo akanzisha bendi yake mwenyewe Afriswezi. Mpaka mauti yake mwezi June 2002. Wanaoikumbuka Police Jazz, imekuwa nayo ni Band ya miaka mingi ambayo wanamuziki wengi maarufu walipitia huko,ni muhimu kuja kuongelea bendi za majeshi na mchango wake katika muziki wa Tanzania.

Kuanzishwa kwa Mlimani Park Orchestra

Sababu ya Mlimani Park kuzaliwa ikiwa imeundwa na kundi kubwa la wanamuziki kutoka Dar International ilitokea kwa bahati sana. Kwa maelezo ya mwanamuziki aliyekuwepo wakati huo, hadithi nzima ilitokana na bendi ya Dar International kukodishwa na Chuo Cha Ardhi katika sherehe yao ya kuwaaga wanachuo wazamani na kukaribisha wapya. Chuo cha Ardhi kilikodi ukumbi wa Mlimani Park kwa ajili ya shughuli hiyo. Wakati huohuo utawala wa Mlimani Park ulikuwa mbioni kutengeneza bendi baada ya kumalizika mkataba wa Orchestra Fukafuka katika ukumbi huo. Tchimanga Assossa ambaye alikuwa amekuja na Bendi ya Fukafuka alibaki nchini na alikuwa katika hatua za mwisho za kwenda kufuata wanamuziki wengine kutoka Kongo kwa ajili ya ukumbi huo. Hivyo basi Dar International wakati huo ndio wakivuma na nyimbo kama Magreti walianza kuporomosha muziki chini ya kiongozi wao Abel Balthazal. Uongozi wa Mlimani Park ulipigwa butwaa na muziki wa hawa jamaa, Abel aliitwa pembeni na kuulizwa bendi iko chini ya mkataba wa nani? Na je, wanamuziki wangeweza kukubali kuajiriwa na na Mlimani Park wakati huo ikiendeshwa na TTTS? Kwa vile Dar International ilikuwa ya mtu binafsi na hawakuwa na ajira yoyote ya kudumu katika bendi hiyo, haraka sana wanamuziki walikubali wazo hilo. Kesho yake viongozi wa Dar International walienda kukutana na viongozi wa ukumbi wa Mlimani Park, na wakakubaliana kuazisha kambi ya bendi mpya palepale katika ukumbi wa Mlimani. Haikuwa taabu maana vyombo vilivyonunuliwa wakati wa mkataba wa Orchestra Fukafuka vilikuwa mali ya Mlimani Park kwa hiyo bendi ilianza kwa Abel kusisitiza kupata wanamuziki kama Muhidin Gurumo,ikumbukwe kuwa ni huyu Abel ndiye aliyeisuka Dar International baada ya kuwachukua wanamuziki wote wa Safari Trippers kundi zima wakati huo, Kassim mponda, Joseph Bernard, Marijan Rajabu, Ben Peti, Zito Mbunda,Bito Elias na wengine kasoro Christian Kazinduki na kutoka Tanzania Stars ya Maggot walitoka Joseph Mulenga, George Kessy , Haruna Lwali na wengineo. Na kwa staili hiyohiyo skwadi nzima ya Dar International ikageuka kuwa Mlimani Park. Muda mfupi kabla la hili ugomvi mkubwa ulikuwa umetokea Dar International kati ya Marijani Rajabu na Abel Balthazar katika ubishi kuhusu tungo aliyoleta Marijani ambayo Balthazar alidai kuwa ni ya Tabu Ley kwa hiyo akatunge tena, jambo lililoleta kushikana mashati, na kusababisha Marijani kusimamishwa kazi. Wakati yuko benchi ndipo mpango mzima wa kuhamia Mlimani ulifanyika hivyo mwenye vyombo alilazimika kumfwata tena Marijani na kumwomba aunde bendi upya, na ndipo Super Bomboka ikaundwa.
Mlimani Park ikaanza ikiwa na Tchimanga Assossa ambaye safari ya kwenda kutafuta wanamuziki Kongo ikawa imekwisha. Na mchango wa kudumu wa Assossa wakati huo ni utunzi wa ule wimbo Gama.

The Upanga Story-Autographs

Utamaduni wa Autograph ulikuwa maarufu sana kwa vijana wa enzi hizo, kwa bahati tuu niliweza kupata kurasa chache za Autograph za vijana wa Upanga sitayataja majina ya wahusika kwa sababu nyingi sana chini ni maelezo yaliyokuwa kwenye autograph hizo, ukizisoma zina eleza mengi kuhusu hali ya wakati huo;
Drink: Coke
Food: Ugali
Clothes:boo-ga-loo
Singers: James Brown
Showbiz Personalities:Guliano Gemma
Records: The Chicken
Girl: "X"
Boy:Groove Maker
Place: Mchikichi
Best Ambition: Music (Drumer)

Drink: Babycham
Food: Tambi + Rice
Clothes: Pecos(bell-bottom)
Singers: James Brown, Clarence Carter,Otis Redding
Showbiz Personalities:Sidney Poitier,Elvis Presley,Franco Nero
Records: If I ruled the world,Thats how strong my love is, Take time to know her,
Girl: The one who loves me
Boy:Groove Maker
Place: Soulville Upanga
Best Ambition: Secret Agent

Drink: Fanta
Food: Chapati
Clothes:boo-ga-loo
Singers: Percy Sledge,James Brown
Showbiz Personalities:Fernando Sancho, Lee Marvin
Records: Take time to know her, Sex Machine Blue Transistor Radio
Girl: Fikirini
Boy:Groove Maker
Place: Soulville Upanga
Best Ambition: Electrician

UPANGA NI ENEO MUHIMU KATIKA HISTORIA YA MUZIKI WA TANZANIA


Upanga ni eneo muhimu sana katika historia ya muziki Tanzania. Hata katika miaka ya karibuni kulizuka kilichoitwa East Coast, muungano fulani wa wasanii wa Bongoflava toka maeneo ya Upanga, hii haikuwa mara ya kwanza kwa Upanga kuwa na wanamuziki waliotingisha mji. Enzi hizo za muziki wa soul, vijana wa Upanga walilipa eneo hili la mji jina la Soulville.Kwenye kona ya barabara ya Mindu na United Nations, nyumbani kwa familia ya Jengo, hapo ndipo palikuwa mahala pa mazoezi pa kundi lile la Groove Makers. Baadhi ya wanamuziki wa kundi hili walikuwa Mohamed Maharage, Joseph Jengo, Emmanuel Jengo, Herbert Lukindo, Willy Makame, na mpiga Drums ambae mpaka leo yupo katika anga za muziki Jeff. Kipindi hiki kilikuwa ni wakati wa muziki wa soul na kundi hili lilikuwa kundi la ubora wa juu wakati huo. Upanga ilikuwa na kundi jingine The Strokers, hili lilikuwa na awamu mbili, awamu ya kwanza ilikuwa na wanamuziki akina Donald Max, David Max, Harry Chopeta, Vincet Chopeta, Pino Makame na Ochiwa na Freddy Lukindo.

Awamu ya pili ya kundi hili lilkuwa na Sajula Lukindo,Onesmo Kibira,Innocent Galinoma,Ben Galinoma, Denis Pad,Francis Kasambala,Vicent na Harry Chopeta, Ally Mwarabu, Sabri Mmanga na wengineo. Barlocks ni Bendi nyingine i
liyochipukia Upanga, jina la Barlockslilitokana na kuweko kwa kundi laBarkeys ambalo leo linaitwa Tanzanites.Barlocks walikuwa wakitumia vyombo vya Barkeys kwani kwa wakati huo bendi hizi zilikuwa kama mkubwa na mdogo. Barlocks hiyo ya awamu ya kwanza ilikuwa na wanamuziki akina Jimmy Jumba,Pimbi Sokoine, huyu alipewa jina la utani Pimbi kutokana na kuwa mrefu sana, Said Mbonde kaka yake Amina Mbonde mwanamuziki mwingine muimbaji,Sajula Lukindo, Abraham. Kulikuweko na makundi mengine mengi hapo Upanga, kamaWhite HorseAquarius hapa walikuweko producer maarufu Hendrico Figueredo, Joe Ball,Joel De Souza, Mark De Souza,Roy Figueredo, Yustus Pereira,Mike De Souza. Baadhi ya wanamuziki wake walienda na kuungana na wengine Arusha na kuvuma sana na kundi la Crimson Rage, baadae wakarudi Dar na kujiita Strange. Baadhi ya kumbi walizokuwa wakipiga zilikuwa DI, Marine,Gymkhana,Maggot, St Joseph na kwenye shule mbalimbali. 
(Picha ya juu-Emmanuel 'Emmy' Jengo, Joseph 'Joe' Jengo, Herbert 'Herby' Lukindo. Kati-Jeff 'Funky' nyuma yake ni Willy Makame. Picha ya chini Willy Makame)

Marijani Rajabu

Marijani Rajabu kwa vyovyote ni mmoja wa wanamuziki ambao wametoa mchango mkubwa katika ulimwengu huu wa muziki. Japo ni miaka mingi toka mauti yake yalipomfika, bado nyimbo zake zinapigwa na wanamuziki mbalimbali majukwaani na hata kurudiwa kurekodiwa tena. Marijani alizaliwa maeneo ya Kariakoo mwaka 1954. Mama yake alikuwa mama wa nyumbani wakati baba yake alikuwa na shughuli za uchapishaji. Maisha yake ya utoto yalikuwa ya kawaida ila alikuwa kipenda sana uimbaji wa Tabu Ley na mwimbaji mmoja wa Guinea Sorry Kandia. Alilelewa vizuri kwa misingi ya dini ya Kiislam kwa hivyo alihudhuria mafunzo ya dini utotoni kama inavyotakiwa. Akiwa na umri wa miaka 18 hivi, alijiunga na STC Jazz, ikiwa chini ya mpiga gitaa maarufu wakati huo Raphael Sabuni, kabla ya hapo bendi hii ilikuwa unajulikana kama The Jets. Katika bendi hii Marijani aliweza kutoka nje ya Tanzania kwa mara ya kwanza ambapo alikwenda Nairobi na kurekodi nyimbo zilizotoka katika label ya Phillips. Mwaka 1972 Marijani alihamia bendi ya Safari Trippers. Hapa ndipo ubora wake ulifunguka haswa na kuweza kuinyanyua Safari Trippers kuwa moja ya bendi maarufu za wakati huo. Waliweza kutoa vibao vilivyopendwa mfululizo na kuweza kuzunguka nchi nzima. Vibao kama Rosa nenda shule, Georgina,Mkuki moyoni, viliweza kuuza zaidi ya nakala 10000 za santuri na hivyo kuwezesha bendi kuwa na vyombo vyake vizuri. Bendi wakati huo ikiwa na wanahisa wanne, ambao kwa bahati mbaya wakati bendi ndio iko juu, wakakosa kuelewana na ukawa ndio mwisho wa bendi hiyo. Miezi michache baadae Marijani na wenzie waliibukia Dar International. Pia huku kulikuwa na wanamuziki wazuri na haraka bendi ilipata umaarufu wa hali ya juu kwa vibao vyake kama Zuena na Mwanameka. kutokana na hali wakati huo bendi ilirekodi vibao hivi RTD na kuambulia sh 2500/- tu. Kilichosikitisha zaidi ni kuwa nyimbo zao tisa ziliuzwa kwa kampuni ya Polygram bila ridhaa yao. Kati ya mwaka 1979 na 1986 bendi ilipiga karibu kila wilaya nchi hii na kufurahisha sana watu na mtindo wao wa Super Bomboka. Uchakavu wa vyombo hatimae mwaka huo 1986, ukamaliza mbio za bendi hii. Kwa miezi michache Marijani akashiriki katika lile kundi kubwa la wanamuziki 57 waliotengeneza Tanzania All Stars, kundi hili lilirekodi vibao vinne ambavyo si rahisi kwa bendi zilizopo sasa kufikia ubora wake kimuziki. Marijani alipitia Mwenge Jazz kw muda mfupi, na kukaa kama mwaka mmoja Kurugenzi Jazz ya Arusha, kisha akajaribu kuanzisha kundi lake la Africulture na mtindo wa Mahepe lakini kwa ukosefu wa vyombo mambo hayakuwa mazuri. Kufiki1992 hali ya Marijani ilikuwa ngumu akiishi kwa kuuza kanda zake ili aweze kuishi.Pamoja na nyimbo nyingi, za kuimbia Chama tawala na serikali, na hata tungo yake Mwanameka kutumiwa katika mtihani wa kidato cha Nne. Rajabu Marijani hajawahi kukumbukwa rasmi kama mmoja wa wasanii bora Afrika ya Mashariki

Blog Mpya ya haki za wasanii Tanzania

Nimekuwa napewa changamoto kubwa kuhusu namna ya kusaidia wasanii wenzangu katika mapambano yao ya kupata haki kutokana na kazi zao mbalimbali walizorekodi au kushiriki. Hivyo basi nimeanzisha blog inayoitwa Wasanii wa Tanzania na Haki Zao ambapo patakuwa jukwaa la kutoa elimu kuhusu haki kama vile Hakimiliki, mikataba ya kazi mbalimbali, pia sehemu ya kupeana maoni na taarifa mbalimbali kuhusu biashara nataratibu nzima za shughuli za sanaa hapa nchini Tanzania. Nategemea wadau mtaweza kuchangia maoni na kuitangaza ili iwe kweli chombo muhimu kwa wasanii wa Tanzania.

Kinguti System

Ramadhan Maulid Kinguti maarufu kama Kinguti System ni mzaliwa Ujiji, Kigoma. 
Bendi yake ya kwanza ilikuwa Super Kibissa ya Kigoma.Super kibissa ni bendi iliyoanziswa 1968 na Kinguti akajiunga nayo mwaka 1977. Wakati huo kiongozi wa bendi alikuwa Mlolwa Mussa Mahango ambaye alikuwa ni binamu yake Kinguti. Bendi ilikuwa mali ya watu watatu, Gollo Saidi, Haruna Mahepe, n Maulidi. Kinguti alitunga nyimbo kadhaa katika bendi hii kwa mfano-Kazi ni uhai, Mapenzi tabu,na Zaina. Mwaka 1979 alichukuliwa na Ahmed Sululu ambae alikua katibu wa Dodoma International na kuhamia Dodoma, ililazimika Dodoma International wamchukue kujaza nafasi ya Shaaban Dede ambaye alikuwa kahama Dodoma International na kuhamia JUWATA. Katika bendi hiyo alikutana kwa mara ya kwanza na mpiga gitaa mahiri Kassim Rashid. Baada ya hapo alihamia Orchestra Makassy ambapo wakati huo walikuweko wanamuziki akina Marehemu Masiya Raddi ambaye alifariki kwa kukanyagwa na daladala, Doctor Remmy, Andy Swebe, Keppy Kiombile, John Kitime, Issa Nundu, Kyanga Songa, Choyo Godjero na wengineo, pia alikuweko Mzee Aimala Mbutu kwenye solo, na Kassim Mganga kwenye rhythm. 1986 alijiunga Afrisso ngoma chini ya Lovy Longomba, hapa alitunga nyimbo sita, Pesa ni maua, Amana mpenzi, Estah Usituchonganishe, waimbaji wakati huo walikuwa Kinguti, Lovy na Anania Ngoliga,kwenye solo alikuweko mzee Kassim Mponda, na rhythm Maneno Uvuruge, Kwa muda mfupi alikuwa DDC Mlimani Park, na hapa akatunga kile kibao maarufu Visa vya mwenye nyumba, ambapo aliimba na Hassan Bitchuka, Francis Lubua,Hussein Jumbe na Benno Villa. Mwaka 1989 alikuwa moja ya wanamuziki waanzilishi wa Bicco Sound, wakiwa na Mafumu Bilali, Asia Darwesh, Andy Swebe, Mzee Aimala Mbutu, walitikisa na vibao kama Muuza chips, Leyla, Magreth maggie, Kitambaa cha kichwa, Nyumba ya kifahari, na nyingine nyingi tu. 1999 alijiunga na kilimanjaro Connection, alikaa bendi hii na Kanku Kelly kwa miaka miwili kisha kuanzisha bendi na akina Hassan Shaw The Jambo Survivors ambayo yupo mpaka leo 

Vijana Jazz enzi za Ngapulila


Kati ya awamu nyingi za Vijana Jazz Band moja iliyoleta changamoto na furaha ni ile awamu ya nyimbo , Ngapulila, Ogopa Tapeli, Adza. Pichani baadhi wa wanamuziki wa wakati huo. Picha ya kwanz a juu- Mzee Joseph Nyerere akiwa na Kulwa Milonge na Hamis Mnyupe, picha ya pili wapiga trumpet marehemu Chondoma, Hamis Mnyupe, na Kulwa Milonge. Picha ya chini ni kundi zima la Vijana Jazz wakiwa na Mheshmiwa Seif Khatib, hapa wanaonekana akina Shaaban Dogodogo, Hemed Maneti,Shaaban Wanted, Abou Semhando na wengine wengi.Kama unavyoona alama za x wengi hawapo tena nasi duniani.Shaw Hassan Shaw


Kwa wapenzi wa Vijana Jazz wanakumbuka vile vipande vya keyboards vilivyokuwa vikianzisha zile nyimbo mbili alizokuwa akiimba Kida Waziri, Penzi Haligawanyiki na Shingo feni, mpigaji wake alikuwa Shaw Hassan Shaw Rwamboh. Mwanamuziki huyu alizaliwa
tarehe 25/sept/1959, Dar Es Salaam. Alianza kujifunza kupiga gitaa na wenzie kando ya Ziwa Tanganyika huko Kigoma, wakitumia magitaa ya tajiri mmoja aliyekuwa na meli ya uvuvi. Aliporudi Dar es Salaam akakutana na mwanamuziki Zahir Ally Zorro, Zahir ndiye aliyeboresha upigaji wake wa gitaa kiasi cha kukubaliwa na Patrick Balisidya kupiga gitaa la rythm katika bendi yake ya pili PAMA Band, chini ya Afro70.
Ni chini ya malezi ya Patrick alipojifunza kupiga Keybords (Kinanda). Baada ya hapo aliacha muziki na kujiunga na Dar Technical College. Lakini 1980 alijiunga na Vijana Jazz kama mpiga Keyboards, alishirikiana na wanamuziki wengi lakini wengi pia wametangulia mbele ya haki. Waliobaki kati ya aliyokuwa nao wakati huo ni John Kitime, Abuu Semhando, Kida Waziri, Saad Ally Mnara, Hamisi Mirambo, Hassan Dalali, Hamza Kalala na Rashid Pembe. Mwaka 1990 alijiunga na Orchestra Safari Sound, chini ya Maalim Muhidin Gurumo (MJOMBA), na Marehemu Abel Baltazar , hapa alikutana na wanamuziki kama Benno Villa Anthony na Mhina Panduka (Toto Tundu) .Aliacha bendi baada ya miezi sita tu, mwenyewe anasema, ‘….kutokana na muhusika kutozingatia mkataba wangu…’. Alihamia Zanzibar na kujiunga na bendi iliyokuwa ikipiga Mawimbini Hotel, hakukaa sana kwani Washirika Tanzania Stars walimwita. Hapa akakutana na Zahir Ally, Ally Choki Rwambow, Musemba wa Minyugu,Tofi Mvambe, Abdul Salvador na wengine, ilitokea kutoelewana baina ya wanamuziki na yeye kama kiongozi wa bendi ilibidi aachie ngazi kuepusha bendi kuzidi kujichanganya. Baada ya hapo Kanku Kelly ambaye ni mume wa dada wa mke wake alimuita ajiunge na Kilimanjaro Connection Band. Anasema Kanku alimvumilia sana kwa kuwa alikuwa hajawahi kufanya kazi ya kukopi nyimbo za wanamuziki wengine wakubwa duniani, pili hii bendi ilikua inazunguka kwa kupiga muziki hotel mbalimbali Malaysia,Singapore, Indonesia,Thailand na Japan jambo ambalo lilifanya aone kila kitu ni kigeni. Katika bendi hiyo alishirikiana na akina Kanku Kelly, Mafumu Bilal, Maneno Uvuruge, Burhan Adinan, Shomari Fabrice, Bob Sija, Fally Mbutu, Raysure boy,Delphin Mununga na Kinguti System. Baadaye Shaw, Kinguti na Burhan Muba waliamua kuanzisha kundi dogo wakitumia sequencer keyboards na kumuaga Kanku Kelly. Group hiyo ilijiita Jambo Survivors Band, itakumbukwa kwa ule wimbo Maprosoo uliokuwa katika album ya MAPROSOO. Baada ya hapo bendi ikaanza kuzunguka nchi mbalimbali ikipiga katika mahotelini. Wameshapita Oman , Fujairah, U.A.E, Singapore, Malaysia na sasa wapo Thailand. Shaw anasema wanamuziki ambao hatawasahau kwa kuwa wamemfikisha alipo ni Zahir Ally Zorro, Marehem Patrick Balisdya, Waziri Ally, Kinguti System, Burhan Muba na Kanku Kelly. Kituko ambacho hawezi kusahau ni nchini Malasyia akiwa na Kanku Kelly kwa mara ya kwanza kupiga muziki akiwa amezungukwa na watu weupe Anasema nyimbo zote zilipotea kichwani akawa hakumbuki hata nyimbo moja.
(Picha ya juu Burhan Muba, Kinguti System ,Hassan Shaw, ya chini ni Vijana Jazz, Hassan Shaw wa mwisho kulia)