LAPF

LAPF
LAPF

Jumamosi, 23 Julai 2011

Baada ya mazoezi ya takriban miezi miwili hatimae wanamuziki wakongwe walifanya onyesho lao ambalo lilikumbwa na mikasa ya dakika za mwisho ambayo ingekuwa si ukubwa dawa kungekuwa hakuna onyesho.

Baadhi ya mambo yaliyojitokeza siku ya mwisho ni kupatikana kwa taarifa kuwa vyombo ambavyo vilikuwa vitumike katika onyesho ambavyo ni vile alivyotumia Shaggy kule Mwanza, vilipata shoti kubwa  ya umeme na kuharibika kwa hiyo havikuweza kutumika. Harakati ya kutafuta vyombo vingine ilifanyika na kuweza kupatikana kwa ufadhili wa Makumbusho Entertaiment katika dakika za mwisho.  Jukwaa ambalo lilikuwa litumike ikapatikana taarifa kuwa limepelekwa Tanga kwenye onyesho huko, na hivyo siku ya mwisho kuanza kutafutwa jukwaa. Pamoja na kuweza kufanikisha kupata vitu mbadala, tatizo la kukosa umeme wa TANESCO lilileta changa moto nyingine. Kupata generator kubwa kutosha kuweza kusukuma vyombo vyote na zile taa za rangi, ilikuwa ni mtihani, hivyo kulazimika kuwa na generator mbili ambazo moja ilitumika kwa taa na nyingine kwa vyombo, kwa kuwa generator hazikuwa na nguvu ikalazimika kutumia robo tu ya vyombo, tukitegemea kuwa TANESCO wangerudisha umeme saa tano usiku, la kuvunda halina ubani, TANESCO wamerudisha umeme sa nane na nusu usiku dakika chache baada ya onyesho kwisha, hivyo muziki kutokuwa na ubora uliostahili.


Kwa upande wa wanamuziki waliokuweko walikuwa Juma Sangula-Bass huyu ndie mzee kuliko wanamuziki wote waliokuwepo, ndie aliyerekodi na Salum Abdalla wa Cuban Marimba vile vibao Shemeji shemeji, Wangu Ngaiye na kadhalika-kapewa jina la utani Sharobaro. mzee huyu muda wote ye hucheka na kupenda utani.  Mabrouk Hamis maarfu kama Babu Njenje wa Kilimanjaro Band, King Kiki, Kasongo Mpinda, Waziri Ally, Kabeya badu, Adinani Ally wa Shikamoo JAzz, Juma Ubao wa enzi ya Biashara Jazz Kumbakisa, Mafumu Bilali, Mbangu Kazadi mpiga rythm wa OSS na Maquis,Andy Swebe, huyu alipiga Bass Makassy, Bicco Stars, MK Group na kadhalika, John Kitime wa enzi ya Tancut, Orchestra Mambo Bado, Vijana Jazz na kadhalika. Akuliake Salehe maarufu kama King Maluu, Bonny Kachale alikuwa mpiga trumpet aliyewahi kupitia Mzinga Troupe, Mlimani Park OSS, kwa sasa ni mchungaji katika kanisa la Efatha. Hamza Kalala Comandoo na mzee wa madongo, Maneno Uvuruge kutoka kwenye ile familia ya wanamuziki, akina Stamili, Huluka na wengineo. Matei Joseph mpiga drum,aliyepitia Uhamiaji Jazz Band, MK Group, Double O na bendi nyimngi nyingine


 . Baadhi ya nyimbo zilizopigwa ni:
1.Miaka 50 ya Uhuru
2. Tanzania Yetu nchi ya furaha-Atomic Jazz
3. Kiyongo-Maquis du Zaire
4. Georgina -Safari Trippers
5. Mali ya Mwenzio-Kilwa Jazz
6. Mtoto acha kupiga mayowe- Dar Jazz
7. Anjeluu- Maquis
8. Magie- Maquis
9. Masafa Marefu-Tancut Alimasi Orchestra
10. Tumezaliwa wote- UDA Jazz
11. Sogea Karibu -JUWATA
12. Kitambaa Cheupe-Zaita Muzika
13. Salam Nimpe nani-
14. Roza Nenda Shule-Safari Trippers

Maoni 6 :

Bila jina alisema ...

Kweli mbuzi wa maskini hazai jamani yaani kuhangaika kote na mazoezi na matayarisho mwisho wake ni matatizo,Inabidi Tanzania itafute suluhisho la kudumu kuhusu tatizo hili sugu la umeme,ni aibu sana kwa taifa zima,na viongozi wetu kazi yao kudai posho na blaa blaa nyingi.Nchi imeoza kabisa hii.

Bila jina alisema ...

John Kitime, sijui nani alikuwa mdhamini wa kazi hii lakini bora irudiwe, katika ubora unaokubalika, kwani kundi lenyewe ni bora sana. Hongereni

Bila jina alisema ...

Cha msingi mlipania kutoa burudani tosha. Ushauri wangu ni kuzipiga nyimbo hizo studio tengenezeni CD msimamie kazi yenu isiibiwe muuze faida iwekeni kwenye kikundi chenu basi, hawa Tanesco watawaangusha tu angalau burudani kila mtu aisikilizie kwenye kijiredio chake

mlawa jr alisema ...

Poleni sana.lakini tusichoke .nadhani lipangwe onesho lingine baada ya mfungo wa ramadhani.wengi tunahitaji kuwaona zaidi ya siku ile.

mlawa jr

Bila jina alisema ...

Mzee Kitime mie ombi langu mfanye onyesho lingine ila pasiwe pale Salender Bridge maana ni padogo sana.

mwacheni77 alisema ...

Poleni sana kwa matatizo yaliyokupateni mwanzo na mwisho wa onyesho lenu,tatizo naloliona mm ni mbona sijaona kina mama ktk picha zako kwani hakuna kina mama wakongwe?