LAPF

LAPF
LAPF

Jumanne, 2 Agosti 2011

Andy Swebe mpiga bezi mahiri

Andy Brown Swebe alianza kupenda gitaa kutokana na kumsikia baba yake mzee Mwalimu  Brown Samson Swebe ambae alikuwa mpiga gitaa mzuri sana, hivyo alikuwa akipiga nyumbani kwao akisindikizana na mama yake Asha Sapi Mkwawa ambae nae alikuwa anaweza kupiga kinanda cha mdomo (mouth organ), na pia kumsikia binamu yake Prince Robert aliyekuwa akipiga na akina Twahiri Ally, Roy Bashekinako Rweyemamu, Balthazar Kunambi, Ally Hega ambao kwa pamoja walikuwa baadhi ya wanamuziki wa bendi ya BAT iliyopiga nyimbo zenye kumbukumbu kama Kumbora. Andy alianza kwa kutengeneza magitaa yake kwa kutumia makopo ya mafuta na mishipi ya kuvulia samaki kama ambavyo wapiga magitaa wengi walifanya sehemu nyingi katika Afrika. Wakati huo akizipenda bendi kama STC Jazz, Afro 70, baadae Safari Trippers. Wakati bado mdogo alikuwa akienda kuwachungulia wakati wakipiga buggy lililokuwa likiporomoshwa kila Jumapili  kwenye  ukumbi wa shule wa Tambaza Secondary. Wakati huo akiishi Upanga ambapo anakumbuka kulikuwa na bendi kadhaa zikiwemo Strokers na De Souza, Barkeys na Barlocks. 

Ili kujifunza magitaa ililazimika kutembea mpaka Chang’ombe kwa David Musa wa Safari Trippers, kwenda kufanya mazoezi, huko kulikuwa na vyombo vyote vya muziki na David alikuwa si mchoyo wa kufundisha vijana. Andy na vijana wengine wa  wa Upanga Magharibi walianzisha kikundi wakikiita BT Commandos(Boom Town Commandos ) ambapo kulikuweko na wanamuziki wenzie kama Martin Ubwe, Emmanuel, Linus Nzuguno, Madaraka Masumbigana, walilazimika kuwa wanaenda Chang'ombe kupata nafasi ya kupiga magitaa ya umeme. 1978, rafiki yake Juma Kunga akampatia gitaa na ndipo alipopata nafasi ya kuanza kufundishwa vizuri na Prince Roberts, bendi yake ya kwanza ni Oshekas ya  Brian Shaka ambapo ilikuwa inapiga mara moja kwa mwezi Yatch Club. Alipiga bendi hii mpaka alipomaliza kidato cha nne, ndipo alipopata kazi na kuhamia  Morogoro, huko akawa anafanya kazi kiwanda cha ngozi.Siku moja Orchestra Makassy ilifanya ziara Morogoro, na hapo rafiki yake aliyekuwa anapiga Keyboards katika bendi hiyo John Bosco akamuona na akakaribishwa jukwaani na akapiga nyimbo chache jambo ambalo lilifanya Mzee Makassy amwite katika bendi yake, 25 May 1983 alijiunga na Orchestra Makassy na onyesho la kwanza lilikuwa Mkirikiti Bar Msasani. Akiwa Orchestra Makassy alishiriki kurekodi nyimbo kama Olenge, Bembeya, Nono, Minachoka ya Masiya Radi, bendi wakati huo ilikuwa na wakongwe kama Mzee Aimala Mbutu(Simaro), Fan Fan Mosesengo, Kassim Mganga na Dr Remmy. Safari  ya Kenya ndiyo iliyoenda kusambaratisha bendi, safari ilipangwa iwe ya wiki mbili ikaishia kuwa tour ya mwaka, na bedni kuzunguka karibu Kenya yote katika mazingira magumu, hali hiyo iliyokuwa ngumu kiasi cha wanamuziki wengine kuamua kurudi Tanzania kila mtu kivyake. Wanamuziki Keppy Kiombile(mpiga Bass Kilimanjaro Band), Selemani Nyanga(yuko Uholanzi) na Andy walirudi zao Dar. Ambapo aliporudi akaja kujiunga na Afriso Ngoma ya Lovy Longomba, wakati huo wakiwa na Kassim Mponda, Raymond Thomas, Seif Lengwe, Sololo wa Imani, John Maida, Ramadhani Kinguti, Kalamazoo na wengine. Wakati huo MK Group, wana Ngulupa Tupatupa, wakawa wanahitaji mpiga bass na Mafumu Bilali ndie aliyemfuata kwenye bendi yake na kumtaarifu kuwa Mkurugenzi wa MK Group angependa kumwona. Baada ya kuongea na Baraka Msilwa alipewa fedha taslimu Shilingi 15,000 kama fedha ya kuhama na mshahara wa mwezi shilingi 5000, kwa wakati huo fedha hiyo ilitosha kumfanya apate chumba chake na kununua furniture. MK Group aliwakuta wanamuziki mahiri kama  Kasongo Mpinda, Mbombo wa Mbomboka, Siddy Morris, Joseph Mulenga(King Spoiler), Ally Makunguru, Abdallah Tuba, Tromblo , Green Simtowe, Paul Vitangi, Rahma Shally, Asia Darwesh na kadhalika........inaendelea

Maoni 3 :

Bila jina alisema ...

Paukwa, Pakawa,

Simulizi tamu sana kumhusu Andy Swebe ambaye a.k.a. yake ikaja kuwa Ambassador.

Natumaini sitaharibu uhondo, kwa kusema nikiwa nasoma Mazengo sekondari, nilikuwa nikihudhuria maonyesho ya Bicco Stars katika uwanja wa Jamhuri kila walipotembelea Dodoma, ndipo lipoanza kumuona akiwa anaungurumisha bass guitar huku aking'ata njiti ya kibiriti mdomomi. Akivaa nguo kama kombati za jeshi na kufunga kitambaa nusu kichwa...si mchezo. Endelea kaka Kitime

Bila jina alisema ...

Kweli David Gordon-Mussa aliwafundisha vijana wengi kupiga gitaa nk. Alikuwa generous sana na vyombo vyake vya muziki huko nyumbani kwake Chang'ombe. Long live Tall-DAVID was Safari Trippers!

HALIMA WaChang'ombe

Bila jina alisema ...

Rest in Peace DAVID GORDON...