LAPF

LAPF
LAPF

Jumatatu, 31 Oktoba 2011

Tabu Ley Rochereau mwanamuziki wa Afrika


Tabu Ley

 
Mbilia Bel
 Tabu Ley Rochereau, alizaliwa mwaka 1940 huko Bandundu katika Jamhuri ya Demokrasi ya Kongo. Alianza maisha akiitwa Pascal Tabu. Tabu Ley alianza maisha yake ya muziki mapema sana na 1954 akiwa na umri wa miaka 14 tu aliandika wimbo wake wa kwanza Bessama Muchacha,  ambao akaurekodi na kundi maarufu la African Jazz lililokuwa chini ya Joseph ‘Grande Kalle’ Kasebele, (asichanganywe na Pepe Kalle). Aliendelea na shule na hatimae alipomaliza High School 1959, ndipo alipojiunga rasmi na African Jazz. Alikuwa mmoj awapo wa walioimba ule wimbo utunzi wa Grande Kalle, na uliotikisa anga la Afrika miaka ya 60, Independence Cha Cha. Uliogeuka na kuwa wimbo rasmi wa kusherehekea uhuru wa kongo.
African Jazz ya Joseph Grande Kalle Kabasele
Baada ya kiasi kama miaka minne alijiengua bendi hii na akiwa na mpiga gitaa mahiri Nicholaus Kassanda aka Dr Nico, wakaanzisha African Fiesta, ambapo alikuweko hadi 1965, wakati Kongo imewaka moto kimuziki na ushindani kuwa mkali sana, akaachana na Dr Nico na kuanzisha African Fiesta National au mara nyingine ikiitwa Africa Fiesta Flash, na kutoa kile kibao maarufu Afrika Mokili Mobimba, ambacho kilivuka mauzo ya nakala milioni moja miaka ya sabini, na kuiingiza bendi hii kuwa kati ya bendi zilizopata mafanikio ya juu katika Afrika kwa wakati huo. Wanamuziki kama Papa Wemba na Sam Mangwana ni kati ya wakongwe waliowahi kupitia katika kundi hili tishio.
 Kufikia mwaka wa 70, Tabu Ley alianzisha Orchestre Afrisa International wakati huo Afrisa na TPOK Jazz ndizo zilikuwa bendi maarufu zaidi Afrika. Afrisa waliteremsha vibao kama Sorozo, Kaful Mayay, Aon Aon, na Mose Konzo na  Tabu Ley
Faya Tess
 aliweza hata kupata tuzo toka serikali za nchi kama Chad iliyompa heshima ya Officer of The National Order, wakati Senegal ilimpa heshima ya Knight of Senegal, na akawa sasa anaitwa Siegneur Rochereau. Katikati ya miaka ya 80 Tabu Ley aligundua kipaji cha mwanamama aliyekuja kutikisa anga za Afrika naye si mwingine ila Mbilia Bel, baadae Tabu alimuoa Mbilia a wakapata mtoto mmoja. Nyimbo kama Nadina, Nakei Nairobi zinaonyesha kipaji gani alikuwa nacho binti huyu aliyekuwa mzuri kwa sura, aliyejua pia kucheza na kutawala jukwaa vizuri. 1988 Tabu akamgundua muimbaji wa kike mwingine Faya Tess. Hapo Mbilia akaacha bendi na kuendelea na maisha yake ya muziki peke yake. Kipindi hiki, mtindo wa Soukus uliokuwa na mapigo yenye mwendokasi zaidi ya lile rumba la Afrisa na TPOK Jazz ulianza kuzishika nyoyo za vijana, bendi hizi kubwa zikaanza kufifia.
Mwanzoni mwa miaka ya 90 Tabu Ley alihamia Marekani akaishi Kusini mwa California, akabadili muziki wake katika kujaribu kujikita zaidi katika soko la ‘Kimataifa’, akatunga nyimbo kama Muzina, Exil Ley, Babeti Soukous. 1996 Tabu Ley alishiriki katika album ya kundi la Africando na kushiriki katika wimbo Paquita wimbo aliyokuwa ameurekodi miaka ya 60 akiwa na African Fiesta. Tabu alipata cheo cha Uwaziri katika utawala wa Laurent Kabila baada ya kuondolewa kwa Mobutu. Hata baada ya kifo cha Laurent Kabila November  2005 Tabu alipewa cheo cha
Vice-Governor in charge of political, administrative, and socio-cultural questions, kwenye jiji la Kinshasa.
Mwaka 2006  Tabu Ley  akashirikiana na rafiki yake wa  muda mrefu Maika munah na kutoa album yake ya mwisho iliyoitwa Tempelo, katika album hiyo binti yake Melodie aliimba nyimbo kadhaa katika album hiyo.

Maoni 6 :

mugo alisema ...

Kaka Kitime ni vizuri umefungua hii blog ili sisi vijana wa leo tunaopenda muziki(wa sasa na ule wa enzi zenu mlivyokuwa vijana)tuweze kupata historia na kusikiliza muziki uliopangika...kaka hii blog ni hazina kubwa ktk masuala ya muziki sio tu wa bongo bali hata wa Afrika yote tafadhali usiache hii blog ifee

Bila jina alisema ...

Afya ya Tabu Ley ilitetereka mwaka 2009 baada ya mkongwe huyu kupata kiharusi (stroke). Bado anaendelea na matibabu.

Bila jina alisema ...

Jana jioni wakati natoka kazini nilikuwa nasikiliza muziki ikaingia ile nyimbo ya Ngugi waliyopiga Franco na Tabu Ley. Ilikuwa kama naisikiliza kwa mara ya kwanza! Nilisikia melody nzuri mno ya muziki wa Ngugi na uimbaji na vyombo vilivyopangwa kwa mpangilio mzuri sana. Ngugi ni kati ya miziki ambayo Franco na Tabu Ley waliitunga kwa ustadi wa hali ya juu sana.

Miaka mingi iliyopita nilisoma kutoka katika waraka fulani siukumbuki upi chronology ya matumbuizo ya Tabu Ley katika aidha kuapishwa kwa Marais au kwenye sikukuu na dhifa za kiserikali duniani. Nakumbuka waraka ule ulisema kwamba Tabu Ley ni moja kati ya wanamuziki ambao wamewahi kutumbuiza katika sherehe za viongozi na dhifa nyingi za serikali mbali mbali duniani.

Nimebahatika kuhudhuria moja ya maonyesho ya Tabu Ley. Onyesho lilikuwa katika ukumbi ambao hupiga wanamuziki maarufu na tiketi zake huwa ni za bei ya juu sana. Bahati mbaya kwenye onyesho lile Tabu Ley hakuwa mchangamfu na pia alichelewa sana kuingia jukwaani na alipoingia aliimba nyimbo chache sana sidhani kama zilizidi nyimbo tano na alikuwa anaimba kama anajiimbia mwenyewe.

Mdau Sokomoko Damu, Helsinki, Finland.

seneta wa msondo alisema ...

Huu hapa wimbo MA'ZE WA MZEE TABU LEY,HAPA UKIWA UMEROKODIWA UPYA NA KUIMBWA NA AWILO LONGOMBA IKIWA NI KATIKA KUENZI KAZI ILIYOTUKUKA YA MZEE HUYO,WIMBO UNAPATIKANA KWENYE ALBUM SUPERMAN YA AWILO

http://www.youtube.com/watch?v=iDs6i_351qQ

dunny jonathan alisema ...

Kaka kitime, kwanza nikupongeze kwa kazi nzuri ambayo inarithisha kizazi hadi kizazi hasa kwa wapenzi wa muziki wa Dansi,naomba nikusumbue kwa manufaa ya wasomaji wa blog yako na Wapenzi wa Muziki wa Dansi kwa ujumla,wako wapi wanamuziki wafuatao na wanajishughulisha na nini kwa sasa
1.christian kazinduki aliyekuwa mpiga besi wa safari trippers.2.mwimbaji wa mazoea yananikondesha uliopigwa na mzinga troops.3.said vinyama mpiga solo wa jkt kimbunga,4.shoo hassan shoo mpiga kinanda wa Vijana jazz enzi hizo.5.chibanga sonny mwimbaji wa ndekule/magereza jazz.6.mwimbaji wa sauti ya kwanza sikinde maalim unyasi.7.mpiga solo wa matimila batt osenga.8.gotagota mwimbaji wa vijana jazz enzi hizo.mwimbaji wa mwenge jazz farahani mzee(acha kulia mwanangu zena)kwa leo ni hao tu.

Bila jina alisema ...

Kwa kweli story ya Tabu ley ni nzuri sana ila nasikitika bwana kitime hukuimaliza yaani kwa kifute mimi sijui huyo tabu ley yupo wapi na anafanya nini kwa sasa,
wako
James Biboze
Holland