LAPF

LAPF
LAPF

Jumatano, 19 Oktoba 2011

Vumbi Dekula Kahanga mpiga solo wa Maquis Original


Vumbi Dekula Kahanga

Orch. Maquis Original 1987 Wapiwapi Chang'ombe Bar,kutoka kulia ni:
Mbuya Makonga "Adios",Dekula Kahanga"Vumbi",Mpoyo Kalenga na William Maselenge.
Alie chuchumaa ni Juma Choka

Kwa wapenzi wa muziki wa enzi wa Tanzania jina la mpiga gitaa Dekula Kahanga Vumbi si geni,  lakini baba yake hakupenda kabisa apige gitaa, lakini bahati nzuri alikulia kwa bibi yake katika mji wa Uvira, mkoa wa Kivu, Jamhuri ya Kongo ambako alikuwa na uhuru zaidi na akaanza kwa kutengeneza magitaa yake, ambalo lilikuwa likivunjwa kila baba yake alipokuwa akija kumtembelea bibi yake.Jirani na alipokuwa akiishi kulikuweko na bar inaitwa Sikiya sosi ambapo palikuweko  na bendi ikiitwa Gramick Jazz, bendi iliyopitiwa na wanamuziki wengi waliokuja Tanzania akiwemo Dr Remmy. Alikuwa akisikiliza muziki ukipigwa katika hiyo bar na yeye akawa anafuatisha kwenye gitaa la kutengeza mwenyewe la nyuzi tatu, hatimae bibi yake akamnunulia gitaa dogo la nyuzi nne ambalo alikuwa naaenda nalo mpaka shule, ambapo mwalimu wake siku nyingine alikuwa akimwita awatumbuize wanafunzi wenzie. Hatimae akakutana na jamaa aliyekuwa akipiga katika bendi iliyokuwa ikimilikiwa na mapadri, akawa anamnunulia sigara huyu jamaa nae akaanza kumfundisha chords mbalimbali za kupiga gitaa. Aliendelea vizuri hatimae akajiunga na bendi hiyo ya mapadri iliyoitwa Kyalalo Band akiwa mpiga rhythm. Wanamuziki wa Kyalalo hawakuruhusiwa kujiunga na bendi zilizo kuwa zinapiga muziki kwenye bar, wala bendi yenyewe  kwenda kupiga kwenye bar, kulikuweko na ukumbi mkubwa wa kanisa na hapo ndipo walipofanya mazoezi na maonyesho, lakini baadae Vumbi akajiunga na bendi Bavy National tena kama mpiga rhythm, 
Kutoka kulia mstari wa nyuma ni Dekula (Rythm),Packot(Solo na Kiongozi),Maboko(Besi),
Merry-Djo (Drums).
Kutoka kulia mstari wa mbele,Waimbaji ni Djo-Mali,Issa Nundu na Simplice Mofeza.
Mwaka wa 1983  katika "Sikia Sosi Bar" Mjini  Uvira Mkoani Kivu Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
na hapo akakutana na mwimbaji Issa Nundu ambae alikuwa anafanya hospitali na jioni kujiunga na bendi, hatimae Kyanga Songa ambaye kazi yake ilikuwa Bwana Shamba nae alijiunga nao.
Katika kipindi hicho wakazi wa Kongo ya Mashariki, ambako kunazungumzwa kiswahili, walikuwa wakisikiliza na kuzijua bendi nyingi kutoka Afrika ya Mashariki, bendi kama Tabora Jazz, Mangelepa, Simba wa Nyika, Mlimani Park zilisikilizwa sana, na nyimbo kama Kassim ilikuwa nyimbo maarufu wakati huo na hivyo ikawa ndoto ya Vumbi kuwa lazima siku moja waende huko unakotoka muziki mtamu huo ili nae aweze kushiriki. Katika kipindi hicho Kyanga Songa na Issa Nundu waliondoka  kwenye bendi yao ya Bavi National na kuelekea Tanzania. Bendi ikatetereka sana, lakini nae wakati huo akawa anahamu sana ya kuja  Afrika Mashariki. Bahati nzuri mtu mmoja Alida Shanga akamjia akiwa ametumwa na Marehemu Mzee John Luanda aliyekuwa anamiliki Chamwino Jazz kuja kutafuta wanamuziki toka Kongo, nae akawachukua na wakatua Tandale jijini Dar es Salaam, na siku waliofika tu na wakaanza mazoezi siku hiyo hiyo. Wakiwa vijana bado yeye na wenzie watatu walikuja wakiwa na staili ya  kuimba na steji show ambayo wakati huo iliitwa sarakasi, na pia wao ndo kilikuwa kikundi cha kwanza kuanza kurap katikati ya nyimbo. Waimbaji wakiwa ni   Sisko Lunanga, Fanfan Bwami, na mwenzao mmoja Baposta Kilosho ambae hatimae alirudi Kongo. Recording ya kwanza ilimuacha Julius Nyaisanga akishangaa vituko vya vijana hawa. Katika bendi ya Chamwino wakati huo wapiga magitaa walikuwa Vumbi Dekula, Kazembe wa Kazembe (huyu alikuwa Msukuma ambaye aliishi kwa muda Kongo na alikuwa mpiga gitaa hodari sana), na Mzee Albert, na hatimae wakamchukua Muhidin ambae alikuwa mpiga bezi wa Dr Remmy. Siku moja walienda kuomba kupiga na Maquis Original(lift), wakati huo wakipiga nyimbo za kopi, nyimbo kama Mario, Maze na kadhalika, hivyo wakazipiga hizo na watu wakafurahi sana na kuwatuza  fedha nyingi, wakachanganyikiwa maana bendi yao ya Chamwino ilikuwa haina mshahara na si mara moja walitembea kwa miguu toka Buguruni hadi Tandale kwa kukosa mapato. Japo wakati huo walikuwa wadogo kwa umri na hata umbo walifika mahala marehemu Kasheba alikuwa anawaita ‘Vimario’, upigaji wao ulikuwa mzuri sana. Nguza aliwashauri wawe wanakuja kupiga kabla Maquis hawajaanza kupiga. Hivyo wakaamua kuacha Chamwino, na wakawa wanasindikizana na Maquis, hili lilimuudhi aliyewaleta na siku moja wakiwa Silent Inn, maafisa wa Uhamiaji walikuja kuwachukua wakalazwa Central Police na kisha kupelekwa gereza la Keko. Wakiwa huko walimwandikia Mzee Luanda kuwa wanarudi Chamwino, basi wakaachiwa na kurudi kusuka upya Chamwino Jazz. Lakini hawakukaa muda mrefu Mzee Makassy akaja kuwaomba waingie katika bendi yake, wenzake waimbaji  wakaenda  yeye akabaki Chamwino, lakini muda si mrefu Nguza akamwambia aandike barua ajiunge na Maquis. Nae akafanya hivyo na ndio kujiunga rasmi na Maquis kama mpiga gitaa la second solo. Aliwakuta wanamuziki kama Maneno Uvuruge, Omari Makuka, Keppy kiombile, Ilunga Lubaba, William Maselenge na wengine wengi.  Aliendelea kupiga second solo hadi siku moja bendi ilikuwa inapiga maeneo ya Ukonga, kwa kawaida Mzee Lubaba alikuwa anapiga kuanzia saa tatu mpaka saa sita, na  kisha Nguza Viking akiingia na kuendelea .
Wa pili toka kulia na shati jeusi Vumbi, wapili toka kushoto na suruali nyeusi Issa Nundu
Siku hiyo Nguza hakuonekana Vumbi  akaweza kupiga nyimbo zote za Nguza, na kesho yake  akaambiwa afike ofisini akasainishwa rasmi mkataba wa kuwa mwanamuziki wa Maquis.  Baada ya muda mfupi Nguza akaacha bendi.
Na baada ya hapo walirekodi ule wimbo maarufu wa Makumbele, solo ya wimbo huu ilikuwa awali ikipigwa na Mzee Lubaba, lakini afya ya mzee Lubaba ilianza kuzorota nae akawa anawafundisha nyimbo zake wanamuziki wengine, wimbo wa Makumbele alifundishwa  Makuka na akawa anaupiga katika mahonyesho mbalimbali, lakini wakati wa kutaka kurekodi kamati ya uongozi ya Maquis iliamua Vumbi aufanyie mazoezi  na aurekodi. Kurekodi kwa album ya Makumbele ilitokana na safari ndefu ya bendi ambayo ilichukua miezi mitatu katika mikoa ya Ziwa, hivyo bendi iliporudi Dar  ilikuta sifa ya bendi imepungua, hivyo walirekodi album ya Makumbele iliyokuwa na nyimbo kama Tipwatipwa, Ngalula na Makumbele, sifa ya bendi ikarudi juu tena kwa mara nyingine. Na ni wakati huo ambapo bendi ilihamia katika ukumbi wa Lang’ata Kinondoni

Maoni 4 :

Bila jina alisema ...

Ngando Mukulu Vumbi namoni yo!

"FREEZE, KAUKA!..DEFROOOOZE,CHANGAMKA!.. Kutumbola Ngando na mayi te, mokila na ye ikubeta yo!.."

Mdau Sokomoko Damu, Helsinki, Finland.

Bila jina alisema ...

Ila Vumbi kiboko katika upigaji wa solo.

seneta wa msondo-usa alisema ...

Papaa Vumbi Dekula Kahanga.. Ndenge nini papa?ozali wapi?

seneta wa msondo-usa alisema ...

Naomba kuuliza hivi Dingituka Molay aliingia nchini mwaka gani?akajiunga na bendi gani,baada ya hapo alipitia bendi gani na gani kabla ya kutua tancut...na ni nyimbo gani alizotunga ukiacha nyama ya nyani ambao nasikia ulipigwa marufuku na kama ni kweli kwanini ulipigwa marufuku?na je marufuku hiyo bado ipo?mwisho kama haipo tena naomba ututafutie then tuusikilize tutafakari ulikua una tatizo gani mpaka kupigwa marufuku.

R.I.P.BROTHER DINGITUKA MOLAY.

seneta wa msondo-Grand Rapids,michigan city.