LAPF

LAPF
LAPF

Jumapili, 9 Oktoba 2011

Women Jazz Band, bendi ya akina mama 1966

Kijakazi Mbegu kwenye solo gitaa
Mwaka 1965 kundi jipya la muziki la aina yake lilianzishwa Tanzania. Lilikuwa ni bendi ya akina mama watupu. Akina mama hawa, wengine wakiwa wafanya kazi wa Government Press walijichagua na kuanza kuhudhuria mafunzo ya muziki chini ya yule mwanamuziki mahiri Mzee Mayagilo aliyekuwa kiongozi wa shughuli za muziki katika Jeshi la Polisi. Akina mama hawa wakawa chini ya kitengo cha Polisi Jazz Band, wakaanza kufanya mazoezi ya nguvu. Bendi hiyo ya akina mama ilikuwa chini ya TANU Youth League. Wakati wakianza shughuli hii walikuwa hawana ujuzi wowote wa muziki. Kutokana na jitihada waliyofanya taratibu wakaanza kufanya maonyesho yao hasa kwenye hafla za serikali na Chama tawala wakati huo.
Tarehe 31 Mei 1966 Women Jazz band iliingia katika studio za RTD na kurekodi nyimbo sita.
1. Tumsifu Mheshimiwa
2. Leo Tunafuraha
3.Mwalimu Kasema
4.Women Jazz
5.Sifa nyingi tuwasifu viongozi
6.TANU yajenge nchi. 
Washiriki katika bendi hiyo walikuwa;
1.Mary Kilima- Mwimbaji
2.Juanita Mwegoha-Mwimbaji
3.Siwema Salum- Mwimbaji
4.Rukia Hassan- Mwimbaji
5. Kijakazi Mbegu- Solo Guitar
6.Mwanjaa Ramadhan-Bass Guitar
7.Chano Mohammed-Rhythm Guitar
8.Tatu Ally-Alto Sax
9.Mina Tumaini-Tenor Sax
10. Anna Stewart-Alto Sax
11. Rukia Mbaraka-Tenor Sax
12.Lea Samweli-Bongos
13. Josephine James-Drums
14. Zainab Mbwana-Maracass
15. Tale Mgongo-Timing.
Women Jazz ilipata umaarufu kiasi cha kuanza kufanya safari nje ya Tanzania, na kuweza kufanya maonyesho Nairobi na Mombasa, baada ya kutembelea miji kadhaa hapa nchini. Wakati wa matayarisho ya kwenda China kundi lilisambaratika. Kikubwa kilichosababisha hili ilikuwa ni wanamuziki kuona hawapati chochote kutokana na mapato yaliyotokana na muziki.


Maoni 4 :

Mija Shija Sayi alisema ...

Kwa kweli inatia moyo sana.. Asante anko Kitime kwa hii.

Perez alisema ...

Kaka,

Yule Pauline Zongo alikwendaga wapi yule?
Alikuwa anaimba na kupiga gitaa yule naamini angeweza kuwakusanya wenzie na kuwa kitu kama hiki tena.

Haebu jaribu kumgusia kama unajua aliko

seneta wa msondo-usa alisema ...

yap kweli mdau umenena juu ya mamaa poulin zongo,yule mtoto amekulia kinshasa drc nilivosikia sasa sijui alirudi congo ama la..kitime atajua kirahisi akitaka,yuko na network kutuliko..

JFK alisema ...

Pauline aliletwa nchini na Mzee king kiki baada ya kutumwa Kongo kwenda kuleta wanamuziki wanawake ili iundwe bendi ya wanawake watupu. Na kweli bendi hiyo iliundwa iikiwa na mabinti toka Kongo na Tanzania. Akiwemo Modesta Nyoni dada mkubwa wa Luiza Mbutu wa Twanga Pepeta. Kundi hilo halikudumu muda mrefu likavunjika na ndipo Pauline alipoanza kujulikana baada ya kufanya recording zake na baadae kujiunga na TOT.