LAPF

LAPF
LAPF

Jumapili, 4 Machi 2012

Wanamuziki wa Tanzania na utamaduni wa kuiga nyimbo

Si jambo la ajabu kukuta mwanamuziki wa Tanzania kachukua wimbo wa mwanamuziki kutoka nje ya nchi hii na kuweka maneno ya Kiswahili na kuutambulisha kama wake. Katika siku za karibuni msanii anayejulikana kwa jina la Timbulo alikiri katika radio kuwa ni kweli amechukua nyimbo Domo Langu na Waleo wakesho, kutoka kundi la X Maleya  la huko Cameroon. Japo aliwahi kukataa kabla jambo hilo na kudai alikuwa kazitunga nyimbo hizo zamani ila kachelewa kuzitoa. Swala kama hili liliwahi kumkumba mwanamuziki TID miaka michache iliyopita. 
Lakini ni ukweli wenye ushahidi  kuwa matukio kama haya si mageni hata kidogo katika historia ya muziki wa Tanzania.  Katika miaka ya sitini,  nchi hii ilikuwa na vikundi vingi sana vya muziki, karibu kila wilaya ilikuwa na bendi ya muziki, Tanu Youth League ambayo ilikuwa jumuiya ya vijana ya chama cha TANU ilikuwa moja wapo ya vyanzo vikubwa vya bendi kwani matawi mengi ya wilaya ya TANU yalikuwa na vyombo vya muziki, na hivyo kuwa na bendi. Jambo moja lililokuwa wazi ni kuwa bendi zilikuwa zimekithiri kwa kunakili nyimbo za bendi kutoka Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Kongo. Kati ya bendi zilizokuwa maarufu kwa hili zilikuwa Dar es Salaam Jazz Band na Kilwa Jazz Band, nyimbo zao za kuiga bado zinapigwa sana hadi siku hizi na wengi hudhani ni tungo za bendi hizo. Wengi tunaufahamu wimbo wa  Ahmad Kipande na Kilwa Jazz ‘Moyoni naumia’, huu ulikuwa utunzi wa Tabu Ley na aliuita ‘Mokolo na kokufa’, nyimbo nyingine kama  Mapenzi yanani vunja mgongo, Pesa nyingi nimepoteza, Na kadhalika zilikuwa moja kwa moja tungo za OK Jazz.  Hali ilikuwa mbaya mpaka serikali ililazimika kuingilia kati na kikao cha wanamuziki kilifanyika pale Lumumba kwenye ofisi za TANU ambapo Waziri husika aliwaomba wanamuziki waanze kutunga nyimbo zao. Baada ya hapo Kilwa jazz walitunga wimbo wenye mashahiri yakisema.’Koma koma koma kaka we tunga zako’.
Hata bendi uinayosikia kama Afro 70, pia iliingia katika mtego huu wa kunakili nyimbo, wimbo, Umoja wa Kinamama, ulikuwa moja kwa moja kutokana na wimbo Georgette wa TP OK Jazz. Vijana jazz Band nayo inaingia katika orodha hii kwa wimbo wao uliotumika katika kusherehekea miaka kumi ya Umoja wa Vijana  wa CCM, ambao nao ulikuwa wimbo wa TP OK Jazz.
Wote tunakifahamu kibwagizo kilichokuwa kikitumika na band ya African Stars, kikisema, Twanga Pepeta hatutaki shari Tunatesa’ ambacho ilitoholewa toka kwa kibwagizo alichokuwa akitumia Defao wakati wa staili ile ya Kiwanzenza.
Bila kubisha hali ya kutohoa nyimbo ni kubwa sana kwa zile bendi ambazo hupiga moja  kwa moja muziki kutoka Kongo. Kwa siku hizi kuanzia uvaaji, uchezaji, na hata kutembea vinaigwa. Vibwagizo huwekwa maneno ya Kiswahili, melody au vipande vya magitaa  au madaraja katika nyimbo hurudiwa vilevile ambavyo vimepigwa na Kofie, au wanamuziki mahiri wa vikundi vya Wenge. 
Wanamuziki wa nyimbo za enjili ni mabingwa mno wa wizi wa namna hii, wengi wamepata umaarufu hata kupata tuzo kwa nyimbo ambazo si zao, katika upande wa nyimbo za enjili muziki kutoka Afrika ya Kusini ndio umekuwa ghala la kuchota melody na uchezaji.
 Muda umefika na kupita wa wanamuziki wetu kuacha kuiba nyimbo au vipande vya nyimbo za wanamuziki wengine. Na muda muafaka wa serikali hii kufanya lile lilifanywa na serikali ya miaka ile mwishoni mwa miaka ya 60

Maoni 9 :

Bila jina alisema ...

suala la kuiga au kunakili kipande au wimbo wote si geni dunia nzima. wapo wanamuziki mashuhuri tena wenye sifa lukuki duniani ambao wanapiga au hata kurekodi nyimbo zilizotungwa na kupigwa na wengine na hakuna kelele wala nini. jambo la msingi tu ni kuzingatia masharti ya haki miliki ya wimbo...mtu aweza kupiga kipande au wimbo wote kwa ruhusa ya mmiliki wa wimbo.

Bila jina alisema ...

Mfano mwingine mzuri ambao Kitime umesahau kuutaja hapa ni wimbo wa Orchestra Safari Sound uliorekodiwa mwaka 1982. Jina kidogo limenitoka lakini ni ule unaomzungumzia mwanaume aliyemwomba mwanamke wacheze halafu baadaye akafanya ‘upuuzi’ wa kumfinyia jicho na kusababisha mwanamke huyo kung’aka. Nachelea kusema wimbo huu ulitungwa na marehemu Ndala Kasheba kwa sababu sehemu kubwa ni tafsiri ya Kiswahili neno kwa neno ya kibao cha TP OK Jazz ‘Bina na Ngai na Respect’ utunzi wake Ntesa Dalienst uliorekodiwa 1981. Sikiliza ‘Bina na Ngai na Respect’ kupitia YouTube www.youtube.com/watch?v=E0GHFbmPpOM

Bila jina alisema ...

Ni kweli ila naona hawa wanamuziki wa kizazi kipya ndiyo noma. Ukiondoa ubovu wa tungo zao, wao kila kitu ni kuiga tu yaani mpaka inakera. Cha kusikitisha utakuta mtu anapiga mapigo ya africa kusini ama magharibu halafu anaitwa mfalme/malkia wa huo muziki wakati amekopi kila kitu, si ujinga huu jamani?

Perez alisema ...

umemsahau Zahir Ali Zoro

" Awali niliomba uniponze moyoo, Sakiinaa...
...Nangoja siku yangu ya mwisho,
nirudi kwenye makazi yangu, mbona natesekaa..."

nae aliuiga pia lakini sikumbuki kwa nani.

Bila jina alisema ...

Kweli mdau March 6, 2012 9:53 AM. Wimbo huo wa Safari Sound Dukuduku sehemu kubwa ni tafsiri ya Kiswahili ya Bina na Ngai na Respect (cheza nami kwa heshima) uliotungwa na kuimbwa na mkali wa vocals Zitani Dalienst Ya Ntesa (RIP) akiwa na TP OK Jazz. Wimbo huu wa Dukuduku ulivyotoka 1982 mara moja nilitambua kuwa Kasheba (RIP) 'ameazima' maneno na staili ya uimbaji kutoka Bina na Ngai na Respect kwa kuwa nilishausikia wimbo huo wa OK Jazz na kwa bahati nzuri naelewa vizuri Kilingala. Nashukuru kuwa nimepata ukumbi wa kutoa dukuduku langu miaka 30 baadae.

Bila jina alisema ...

Mimi sina tatizo na wanamuziki wanaopiga upya nyimbo za wanamuziki wengine na ikajulikana wazi kuwa wamerudia nyimbo hizo baada kupata ruhusa kutoka kwa watunzi au wamiliki wake. Tatizo langu ni wanamuziki wanaoiga nyimbo za wengine na kutaka watu waamini kuwa ni zao. Zamani watu walikuwa wakijihusisha na wizi wa aina hii bila kuwepo uwezekano mkubwa wa wao kujulikana, lakini teknolojia ya habari na mawasiliano hivi sasa imerahisisha wezi wa nyimbo kujulikana. Siku hizi karibu kila wimbo unarekodiwa unaweza kusikilizwa katika internet kwa hiyo siku za mwizi zinakuwa kweli ni arobaini.

Bila jina alisema ...

Mzee Kitime naomba tafadhali nitoke kidogo kwenye mada. Kwa muda mrefu nimekua nikililia vipaji Tanzania vya uimbaji. Watu wanaunguruma nguruma tu hakuna jipya mpaka nimeona bwana mdogo mmoja nimechka mwenyewe. Tafadhali naomba watanzania wenye moyo wa upendo wamsikilize na kumsaidia mtoto anaitwa DOGO ASLAY. Kile jamani ni kipaji. Kama anaweza kutoa vocal aliyonayo kwenye umri alionao, akikua itakuwa balaa. Katika kipindi cha zaidi ya mlongo mmoja, sijaona kipaji kama hiki. DOGO ASLAY yupo juu jamani. Naomba Mungu bongofleva isimuharibie kipaji chake maana wale sijui wanaimba au wanaongea?

emu-three alisema ...

Mkuu kuna wimbo wa nafikiri OSS, `takadiri...'unaweza kuuweka hewani, unanikumbusha mbali...Tupo pamoja

SENETA MSONDO alisema ...

kuiga sio issue ila basi wawe wanasema kwamba huu wimbo ni wa fulani inatosha.

Maana hata marehemu witney houston nyimbo zake zote zilikua za kuiga na zilimpatia pesa tuzo kibao huku zikimfanya awe international icon kuwazidi hata wenye nyimbo,so thas not a big deal,but kuonyesha heshma kwa mtunzi jambo zuri.

Tuliona wimbo shoga wa benno villa uliigwa na yule dada alikua mtangazaji wa redio clouds nimesahau jina lake lakini nadhani alimuona benno badae ingawa mwanzo hakufuata taratibu kwa mujibu wa benno mwenyewe siku moja nilipanda nae daladala hapo dar nilimuuliza.

seneta wa msondo-Revere massachisetts,usa.