LAPF

LAPF
LAPF

Jumanne, 10 Aprili 2012

Kifo cha Les Wanyika

Simba wa Nyika ya mwanzo.

Ni bahati mbaya kuwa wanamuziki waliohamia Les Wanyika hawakutaka kuondoka na George Peter kwa kosa waliloona ni la ndugu yake Wilson Peter, maana George alikuwa mfanya kazi mzuri aliweza kuimba na kupiga vyombo vingi, sijui kingetokea kitu gani bora zaidi kama George angejiunga na Les Wanyika lakini hayo ni mawazo yangu tu. Wakati mambo yakishamiri kwa Les Wanyika, hali ilikuwa mbaya kwa Simba wa Nyika, maana walikuwa wamebakia ndugu watatu Wilson, George na William ambaye wakati huu hali yake haikuwa inaweza kutegemewa katika kazi kutokana na maradhi yake ya kichwa. Wilson hakuamini kilichotokea kwamba bendi yake ambayo ilikuwa maarufu ikawa haiwezi tena kupiga kwa kukosa wanamuziki na hata walipojaribu kupiga walikosa wapenzi. Baada ya kipindi cha miezi kadhaa ya kushindwa kufanya maonyesho kwa kukosa wanamuziki na hata washabiki, bahati kubwa ikatokea kwa Simba wa Nyika. Wanamuziki watatu kutoka Kurugenzi Jazz band ya Arusha, George Madrago mpiga bezi, Joseph Tito mpiga rhythm, na Mzee Maneno Shaaban aliyekuwa anapiga drums na Tumba wakaja kuungana na Wilson na George kujaribu kufufua Simba wa Nyika. Walifanikiwa kupiga muziki mzuri tu lakini bahati haikuwa yao wakakosa wapenzi. Haukuchukua muda mrefu, Wilson na George walianza kutofautiana tena, safari hii kukatokea mpasuko ulioanzisha Orchestra Jobiso. Orchestra Jobiso ilianza vizuri ikiwa na wanamuziki wafuatao, George Peter-Kiongozi, mwimbaji na mpigaji gitaa la solo, George Madrago- Bezi gitaa, Joseph Tito- rhythm guitar, Said  Makelele na Mambi Juma wakiwa kwenye trumpet, katika recording ya kwanza ya Jobiso pia walikuwa na mpiga saxaphone aliyeitwa George Kalombo na wakatoa vibao kama Christmas imefika, Mwana wa kambo, Pole Jobiso, Karibu, Chunga heshima, Visa vyako, nakadhalika.  Mwaka huu wa 1981 George na Wilson Peter tena kujaribu kufufua Simba wa Nyika. Wakati huo mdudu wa matatizo tayari aliingia katika bendi ya Les Wanyika, pamoja na kwamba Profesa Omary ndie aliyekuwa Kiongozi, taratibu akawa ameanza tabia ya ulevi na hivyo kutokuwa na mahudhurio mazuri kazini, usukani kwa kweli ukawa unashikwa na John Ngereza. Hali ilikuwa mbaya kiasi cha Profesa Omary kusimamishwa kazi mara kwa mara na bendi ya Les Wanyika, bendi aliyoanzisha yeye mwenyewe. Kutokana na tabia hiyo mwanamuziki Stanley Mtambo akakaribishwa ili kupiga rythm, na hata aliyetupatia habari hizi mwanamuziki Abbu Omar, ambaye baadae alikuja pia kurithi jina la  Profesa Jnr alipitia bendi hiyo tena kwa mualiko wa Profesa Omary mwenyewe. Hali hii  ya kuwa na matatizo na uongozi usioeleweka ikaanza kuleta matatizo kwa wanamuziki hasa katika malipo. Ndipo hapo basi wanamuziki Issa Juma na Mohamed Tika wakaamua kutafuta njia nyingine ya maisha, jambo lililoleta kuanzishwa bendi nyingine hii wakaiita Super Wanyika. Bendi hii ikawa na mchanganyiko wa wanamuziki kutoka Les Wanyika na Jobiso chini ya kiongozi Issa Juma. Huyu Issa Juma ndiye aliyekuwa muimbaji mkuu wa Les Wanyika sauti yake inatambulika dunia nzima kutokana na wimbo Sina Makosa. Mwezi june 1981 ndipo alipoacha Les Wanyika ili kuanzisha Super Wanyika. Alikuwa maarufu sana kiasi cha kufanyiwa hila na wanamuziki wenyeji akafungwa miezi kadhaa huko Kenya kwa kufanya kazi bila Work Permit. Mwaka 1988 alipata ugonjwa wa kupooza na hivyo kupata taabu ya kutembea na hata kuongea na hatimae akafariki mwanzoni mwa mwaka 1990. Je Super Wanyika ilianzaje?........itaendelea

Maoni 2 :

Bila jina alisema ...

Sad story but very interesting....looking foward
Mike

Kinyerezi alisema ...

Wapi naweza kupata huu wimbo wa "Christmas imefika"?