LAPF

LAPF
LAPF

Alhamisi, 7 Juni 2012

Pepe Ndombe afariki dunia


Pepe Ndombe


Mwanamuziki muimbaji  aliyekuwa bendi ya OK Jazz na baadaye Bana OK, Ndombe Opetum aliyejulikana kwa jina la Pepe Ndombe  amefariki kwa ugonjwa wa moyo, mjini Kinshasa, Jamhuri ya Demokrasi ya Kongo.
Pepe alikuwa mwimbaji wa Afrisa International ya Mzee Tabu Ley na kuiacha bendi hiyo na kujiunga na TP OK Jazz baada ya Sam Mangwana kuondoka OK Jazz. Aljiunga na Ok Jazz akiwa na Empopo Loway mwanamuziki mpulizaji, na aliitumikia OK Jazz mpaka iliposambaratika mwaka 1993. Baadhi ya nyimbo alizotunga Pepe ni:
  • Voyage ya Bandundu
  • Mawe
  • Mabe Yo Mabe - In 1977
  • Coupe du Monde - 1979
  • Youyou - In 1980
  • Nayebi Ndenge Bakolela Ngai - 1982
  • Angela - In 1989
  • Tawaba - In 1989
Baada ya kifo cha Franco mwaka 1989, TP OK Jazz iliendelea katika mfumo ambao Mzee Simarro aliendelea kuwa kiongozi wa bendi na kusimamia mambo ya wanamuziki,wakati familia ya Franco iliendelea kusimamia upande wa wanasheria wa bendi, label za bendi na mambo mengine ya kiufundi , wanamuziki wakigawana asilimia 70 ya mapato wakati familia ikipata asilimia 30 ya mapato. Tofauti zikajitokeza na miaka minne baadae, na Desemba 1993 ukawa mwisho wa TP OK Jazz. 
January 1994 Pepe alikuwa mmoja wa wanamuziki waanzilishi wa kundi la Bana OK, na hakuliacha kundi hili mpaka kifo kilipomkuta May 24, 2012.
Wizara ya Utamaduni na Sanaa ya Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo inatayarisha maziko ya heshima mwanamuziki huyo.
Pepe Ndombe Opetum alizaliwa jimbo la Bandundu mwaka 1944, alisoma katika jiji la Kinshasa, alioa na akapata watoto 9. Mtoto wake wa 5 aliyezaliwa tarehe 3 March 1974 ni mwimbaji ambaye hujiita Baby Ndombe au mara nyingine Black Ndombe, nae anafanya vizuri katika ulimwengu wa muziki.

Maoni 2 :

Kisondella, A.A alisema ...

Inaniwia vigumu kuamini kuwa mwanamuziki Paul Ndombe Opetum "Pepe Ndombe" amefariki dunia.
Nikiwa mmoja ya wafuasi na mpenzi mkubwa wa bendi ya TP OK Jazz pamoja na iliyoyotokana nayo - Bana Ok inaleta simanzi ya hali ya juu.

Kama ilivyo kwa bendi za Msondo na Sikinde, ndiyo iliyokuwa kwa bendi ya Afrisa International ya Tabuley na TP OK Jazz ya Franco - yaani kuchukuliana wanamuziki. Ndombe pamoja na marehemu wengine Empopo Loway, Ndiembu Kiesse Ya Ntesa kwa nyakati tofauti walikuwa wanamuziki wa Afrisa International ya Tabuley na walichukuliwa na Franco kulipa nguvu kundi la TP OK Jazz.

Kwa picha ninayoiona sasa kwa iliyokuwa TP OK Jazz hakuna tofauti na ninachokiona katika Bendi ya Msondo Ngoma; takribani waimbaji wote wa iliyokuwa TP OK Jazz wamefariki, ukianzia Jean Bialu Madilu "System", Aime Kiwanaka Kiala, Djo Mpoy Kaninda, Dalienst Zitani Ya Ntesa, Ndiembu Kiesse Ya Ntesa, Bonyeme, Lola Checain Djang, hawa mbali ya waasisi wa Ok Jazz kama Vicky Longomba,Philippe Lando Rossignol, Edo nganga, Kwamy Munsi, Mulamba Joseph Mujos, na Franco mwenyewe.

Nashindwa kupata picha wanamuziki ambao walikuwa sambamba wakiimba na Ndombe kama Josky Kiambukuta, Wuta mayi, Michael Boyibanda, Sam Mangwana.

Hii ndiyo ninayosema nalinganisha na ninachokiona Msondo Ngoma ambapo vocal line hatunayo tena ukiachia mbali Shaaban Dede na Maalimu Gurumo waliobaki, yuko wapo Ally Akida, Tx Moshi William, Athumani Momba, Suleman Mbwembwe, Joseph Maina, Nico Zengekala, Tino Masenge.

Mungu aiweke mahali pema roho ya Marehemu Paul Ndombe Opetum na wengine wote waliotangulia hapa kwetu Tanzania na huko Zaire.

Nitaendelea kumuenzi Paul Ndombe Opetum kwa kusikiliza nyimbo zake akiwa na Afrisa International, TP OK Jazz na Bana Ok

Kisondella - (Mafinga) - Iringa

emu-three alisema ...

Ndio maisha tena hayo, kuzaliwa na kufa..RIP Pepe