LAPF

LAPF
LAPF

Jumanne, 17 Julai 2012

Cuban Marimba Band


Salum Abdallah Yazidu


Kuanzia miaka ya 1920 mpaka 1940, wanamuziki na wapenzi wa muziki walifuatilia sana muziki kutoka Cuba kupitia sahani za santuri za wakati huo. Kulikuwa na vikundi kama Trio Matamoros and Sexteto Habanero, ambao walitoa santuri zikiwa na namba zinazoanzia GV1, GV2 na kuendelea na kupata upenzi mkubwa katika sehemu kubwa ya  Afrika. Ni vikundi hivi ambavyo viliingiza mitindo kama rhumba, Bolelo, Chacha na kadhalika, na muziki huu kuwa ndio mbegu ya muziki wa dansi wa Afrika mpaka leo. Kwa kweli bendi za muziki wa dansi zingepata mengi ya kimapinduzi kama zingeweza kusikiliza na kuelewa muziki wanaoupiga kiini chake ni nini.

Kutokana na hamu hiyo ya kuujua na kuupiga muziki wa kiCuba kisawasawa Marehemu Salum Abdallah aliwahi kutoroka kwao Morogoro akakimbilia Mombasa ili apande meli aende Cuba, bahati mbaya safari yake iliishia Mombasa, baada ya kuibiwa fedha zake na kulazimika kuanza kazi ya kuchoma mishkaki katika jiji hilo, ambako alianza kupata shida lakini kwa kuwa baba yake alikuwa mwarabu, Ushirika wa waarabu wa Mombasa walimtaarifu mzee huyo kuhusu alipo mwanae na alimfuata na kumrudisha Morogoro.  Salum Abdallah Yazidu aliyefahamika sana kama SAY, mwaka 1948 alianzisha bendi yake akaiita La Paloma, ambalo ni jina la wimbo maarufu ambao uliotoka Cuba ukiwa na jina hilo lenye maana Njiwa, wimbo huu unaendelea kupigwa hadi leo ukiimbwa na kurekodiwa kwa lugha mbalimbali duniani, marehemu Elvis Presley akiwa moja wapo aliyewahi kurekodi wimbo uliotokana na huo wa La Paloma, hata hapa Tanzania bendi nyingi huzisikia zikipiga wimbo huu na kuweka maneno yake ya papo kwa papo hasa kabla dansi rasmi halijaanza. Bendi ya La Paloma ndio ilikuja kuwa Cuban Marimba Band, Salum Abdallah aliiongoza bendi hiyo mpaka kifo chake 1965, kifo kilichotokana na ajali ya gari, baada ya roli lake la kubeba mchanga kuzimika taa ghafla na kuacha barabara na kugonga kidaraja nae akatupwa nje ya gari na pupasuka kibofu.

Aliyeichukua bendi na kuiendeleza alikuwa Juma Kilaza. Kilaza aliiendeleza vizuri kwa kutunga mamia ya nyimbo yaliyofurahisha sana watu miaka ya 60 na 70. Morogoro ulikuwa mji uliosifika kwa muziki, huku kukiwa na Mbaraka Mwinshehe na Morogoro Jazz, na huku Juma Kilaza na Cuban Marimba. Kuna watu walikuwa wakihamia Morogoro wikiendi na kurudi Dar siku ya Jumatatu asubuhi. Kati ya nyimbo maarufu za Cuban Marimba zinazodumu kwenye kumbukumbu ni Shemeji shemeji wazima taa, Wangu Ngaiye na wimbo Ee Mola Wangu, ambao Salum Abdallah awali aliutunga kwa mashahiri marefu lakini akachukua beti chache kutengenezea muziki akilalamika kuwa kuna walimwengu wanamtakia mabaya, lakini siku ya kufa atawashitakia maiti wenzake kuhusu ubaya huo, wimbo huu ulikuja onekana baadae kama ulikuwa ukitabiri aina ya kifo chake’


Maoni 4 :

Bila jina alisema ...

kaka kitime mimi niko nje kidogo ya mada naomba kama hutajali unisaidie kuna huu wimbo wa sina uwakika na aliyeiimba lakini huu wimbo naupenda sana ni wa zamani kidogo nitakupa mistari kidogo kama utaifahamu! inaanza kila mutu awe na kwao kwa baba na mamae ni hiyo mistari nimeweza kukumbuka kidogo lakini kwasababu wewe ni mwamuziki wa kitambo kidogo zizani kama utashindwa kuelewa huyo alieimba alikuwa kama mtu wa mzumbiji hivi pls naomba jina jina ya hiyo wimbo ili niweze kuseach ktk gogle na swali langu la pili na la mwisho ni wimbo wa talakatalaka mpaka yanitoa jasho nilipofika mpaka kipenzi akagoma mpenzi twende nyumbani ukaone wazazi nilipofika mpakani mezi kagoma ni hiyo mistari tu ndio nakumbua unaweza kunipajina ya hiyo bendi pi niweze kugogle asante sana kaka kitime ubarikiwe sana nasubiri jibu kwa hamu sana

JFK alisema ...

Wimbo unaitwa Kila munu ave na kwao....ulipigwa na bendi ya Jeshi iliyoitwa Les Mwenge, ila mtunzi wake Tongolanga alienda na kuishi Msumbiji kwa muda, nitatoa hadithi yake humu soon.
Talakatalaka Mpakani ulipigwa na Baba Gaston

Bila jina alisema ...

asante ubarikiwe sana kwa kunijibu kazi njema tunasubiri hiyo hadithi kwa hamu

Bila jina alisema ...

Ama matehemu.Salim.Abdullah alifurahisha watu wengi sana
Mungu amsamehe na amlaze pema. amin