LAPF

LAPF
LAPF

Jumatatu, 2 Julai 2012

PAUL DANIEL GAMA mwanamuziki wa Central Jazz na Dodoma Jazz-Part 1


Paul Daniel Gama
Paul Daniel Gama alizaliwa Barabara ya 11 Dodoma (1947). Baba yake alikuwa ni mwanajeshi wa KAR mwenye asili ya Songea na mama yake alikuwa na asili ya Usangu alikuwa anafanya kazi  katika 
Spokes Mashiyane na filimbi yake
hospitali ya Mirembe ambayo wakati huo ilikuwa ni hospitali kubwa ya majeruhi wa vita ya pili ya dunia. Aliingia shule na alipofika darasa la nne alijikuta akiwa na kipaji kukubwa cha kupiga filimbi, wakati huo wapiga filimbi walipenda sana kumuiga mpiga filimbi maarufu kutoka Africa ya Kusini Spokes Mashiyane. Akiwa na wenzie walianzisha kikundi ambacho kilikuwa na maskani eneo la Mji Mpya pale Dodoma. Vijana hao pia walikuwa wakiiga  nyimbo za wanamuziki maarufu wa wakati huo, kama Salum Abdallah na  Cuban Marimba, pia Salum Zahor na Kiko Kids. Katika kufanya fani yao hiyo kama kitu cha kujipa burudani waliligusa sikio la  aliyekuwa mwalimu wa Elimu ya Watu Wazima katika Community Center ya pale Dodoma. Mwalimu huyu aliwasaidia kuwaazimia amplifaya moja kutoka kwenye bendi nyingine ilikuweko Dodoma wakati huo, The Jolly Sextet Band. Band iliyokuwa ikimilikiwa na Mkenya mmoja ambaye alifika Dodoma kama mfanya kazi wa East African Postal and Telecommunication Services, huyu bwana alikuja na vyombo vingi akaanzisha bendi ambayo mmoja wa wapigaji wake alikuwa Mzee Mnenge ambaye hatimaye alitua NUTA Jazz Band.
Bongos
Hiki kikundi cha Gama na wenzie kilikuwa katika mfumo wa Jazz Band za zamani ambapo walikuwa na ngoma na filimbi tu,ikisindikizwa na kuimba, lakini waliweza kukonga nyoyo hata za wanamuziki wengine, na Gama akawa anasakwa na bendi kubwa iliyokuweko wakati ule Central Jazz band. Alipomaliza darasa la saba tu ndugu yake aliyeitwa Titus Olaf Gama alimshawishi aingie Central Jazz lakini hakuwa tena mpiga filimbi bali mpiga Bongos, fani aliyoiweza sana hata  kuipenda na hasa baada ya kuwaona wanamuziki wa NUTA akiwemo Muhidin Gurumo  ambaye wakati huo alikuwa akipiga Bongos na kuimba. Bongos no ngoma ndogo zilizokuwa muhimu katika kundi wakati huo ambapo hakukuweko na drums wala tumba. Taratibu akaanza kupata hamu ya kupiga bass, wanamuziki wenzie walimkatisha sana tamaa kwa kuambiwa kuwa vidole vyake vilifaa sana kwa kupiga bongos na si kupiga gitaa.

Hakuna maoni: