LAPF

LAPF
LAPF

Jumanne, 14 Agosti 2012

Mark Manji mpiga rythm wa Orchestra MkwawaORCHESTRA MKWAWA-Waliosimama  Mungure(Saxophone),Tanganyika(Saxophonist),Mark Manji(Rythm),Waliokaa  Kakoko(Solo),Simon Sewando(Solo),John Mkamwa(Bass)
Mkwawa Secondary
Mark Manji alianza kupenda sana kusikiliza  wapigaji wa magitaa makavu(accoustic) maarufu kama magalaton, kutoka kwa wapigaji waliokuwa kijiji kwao Chitare, Musoma. Kutokana na kupakana na Kenye ambako kulikuwa na wapigaji maarufu kama akina George Mukabi, John Mwale na kadhalika, upigaji wa aina hiyo ulikuwa maarufu katika eneo la Musoma. Anakumbuka toka yuko darasa la tatu alianza kuwa  na  hamu sana ya kuwa mwanamuziki. Hamu hii iliongezeka alipoingia kidato cha kwanza Alliance Secondary pale Musoma  ambako kila Jumamosi alianza kwenda kuchungulia wakati  bendi ikipiga  Musoma mjini. Bendi aliyokuwa maarufu wakati huo ilikuwa inaitwa Eleven Stars Band, pamoja na kuwa bendi ilikuwa na watu sita iliitwa Eleven Stars kwa kuwa mwenye bendi pia alikuwa anaendesha club ya mpira iliyokuwa na jina hilo. Bendi hiyo iliyokuwa na mpiga solo kutoka Kigoma, mpiga bezi Mkongo, mwimbaji Mkongo na waTanzania wengine wawili, mmoja wa waimbaji alikuwa akiitwa Dode ambaye kwake ndiko vyombo  vya bendi vilikuwa vinatunzwa.  Huyu Dode, ambaye baadae sana Mark aligundua ni kifupi cha Deusdedit alikuwa akiishi karibu na kaka yake mmoja, hivyo akaomba kujifunza gitaa na taratibu akajifunza gitaa la rhythm. Hizi juhudi zake za kujifunza muziki ziliwahi hata kusababisha kufukuzwa shule wakati akiwa form II, lakini hatimae alimaliza form IV.  Mwaka 1970  akawa amechaguliwa kujiunga na shule ya sekondari ya Mkwawa,  katika kumbukumbu zake hakuwahi kusikia kuwa Iringa kulikuwa na bendi kwa hiyo alikataa kwenda kuendelea na shule kwa kuwa alitaka kuwa mwanamuziki. Akawa na ndoto za aidha kwenda kusoma Tanga, Morogoro, au Tabora maana huko alijua kulikuwa na bendi. Pamoja na baba yake kujitahidi kumshawishi kwenda kusoma Mkwawa alikataa katakata akitaka kujiunga  na muziki au aende kusoma kwenye mji wenye bendi. Alijitahidi hata kubadilishana na mwenzie aliyechaguliwa kusoma Galanos Tanga lakini ikashindikana. Baada ya kama wiki tatu toka shule zimefunguliwa akakutana na mtu aliyemshangaa kwanini hajaenda shule, na alipomwambia kuwa hana mpango wa kwenda Iringa kwa kuwa hakuna bendi, yule mtu alimtaarifu kuwa katika shule ya Mkwawa kuna bendi, na tena ndio inayopiga Iringa mjini. Baada ya kusikia hayo moja kwa moja akaenda kwa baba yake na kumwambia kuwa ameamua kwenda shule, tena kesho yake. Baba yake hakuongeza neno, akampa fedha haraka sana nae  haraka akenda ofisi  za wilaya na kupewa warrant ya kwenda kusafiri kuelekea Iringa. Ikiwa ni mara ya kwanza kusafiri nje ya Musoma, lakini alifanikisha safari yake ndefu ya meli hadi Mwanza, treni Mwanza mpaka Dodoma na bus Dodoma hadi Iringa. Alifika shuleni Mkwawa kama saa kumi na moja jioni, akakuta taratibu ziko nzuri maana akakuta orodha iliyoeleza bweni na chumba alichopangiwa, alipangiwa bweni la Magembe West. Haraka akaweka mizigo tu kwenye chumba alichopangiwa na kuulizia bendi iko wapi, akaelekezwa na kukuta mazoezi yanaendelea, akakaa hapo kwa saa nzima na kujua kweli amefika alipotaka. Pamoja na masomo akaendelea na bendi ambayo kweli iliendelea kupiga Iringa mjini, kila wikiendi katika dansi lililojulikana kama bugi. Lilianza saa nane mchana na kuisha saa kumi na mbili jioni.Bendi ilikuwa na wanamuziki wafuatao, yeye Mark Manji rhythm, Kakonko solo, Tanganyika mpuliza Sax, John Mkamwa kwenye bass, Makange, Sewando solo, Masanja rythm, Danford Mpumilwa muimbaji, Semboni, Zacharia Kakobe na Norman Hiza. Mwaka 1972 baada ya kumaliza mitihani ya mwisho bendi ilisafiri hadi Dar es salaam kwenda kurekodi,bendi ya  Vijana Jazz ndio walikuwa wenyeji wao na wakawaazima hata vyombo walivyoenda kurekodia. Baada ya kumaliza shule ya Mkwawa kama ilivyokuwa ada wakati huo akaenda kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa, mwaka 1973 baada ya kumaliza JKT akaingia Dar es Salaam akiwa na nia ya kujiunga aidha na Dar es Salaam Jazz au Western Jazz bendi alizozipenda sana, lakini anasema hali ya wanamuziki aliyoikuta ilimkatisha tamaa kuwa mwanamuziki na kuamua kuendelea na masomo, na kufanya muziki kuwa ni shughuli yake ya ziada, jambo ambalo ameweza kulifanya na wakati huu ambapo amekwisha staafu kazi ameanzisha kituo kikubwa cha kufundisha taaluma mbalimbali za muziki. Kati ya bendi ambazo Orchestra Mkwawa iliwa kupiga nazo katika jukwaa moja ni Cuban Marimba ya  Kilaza, Butiama Jazz Band, The Jets wakati huo  Marijani Rajabu na wanamuziki wengine mahiri kama Raphael Sabuni, Belino, na kadhalika.
Mkwawa kulikuwa na bendi mbili, bendi ya pili ilikuwa ikipiga muziki  wa  kizungu, wakati huo muziki ulioigwa sana na bendi za aina hiyo  ulikuwa ni wa soul, na blues. Hivyo bendi hii ya pili ilipiga muziki wa akina James Brown, Wilson Picket, Otis Redding, Jimi Hendrix na kadhalika, baadhi ya wanamuziki waliokuwemo katika bendi hii walikuwa ni Bijoux, Deo Ishengoma na Shaba katika drums. Deo aliyekuwa mwimbaji mmoja wapo alikuwa na mvuto wa pekee kutokana na Afro yake kubwa na uvaaji uliomfanya ajulikane mji mzima wa Iringa.     

Hakuna maoni: