LAPF

LAPF
LAPF

Alhamisi, 11 Oktoba 2012

KASSIM “RHYTHM” KALUONA WA SEGERE MATATA, NYOTA YA MAGHARIBI ILIYOZIMIKA GHAFLA


KASSIM KARUONA
MAKALA HII ILIYOANDIKWA, NA NYINGINE NYINGI KUHUSU TABORA UTAWEZA KUZISOMA-uyui.wordpress.com/
  Aliwashangaza wengi kwa Gita lake la Rythm lililo ongoza baadhi ya nyimbo kama dada Helena, chakula kwa jirani na nyinginezo
Watu wengi Tabora walimfahamu kwa jina la Kassim rhythm hata wasisumbuke kujua jina la baba yake
Tabora, Dar na Kigoma vyakumbwa na wingu zito la simanzi.. kifo chake chatonesha donda la marehemu Hanzuruni, Wema Abdalla, Msafiri Haroub, Issa Ramadhani na Halfani Juma
________________________________________________________________________
 Kifo mara zote huja kwa kushitukiza, ndivyo zilivyokuja taarifa za kifo cha marehemu mwamamuziki mkongwe Kassim Hassani Kaluona maarufu kama Kassim Rythm aliyefariki dunia siku ya Jumatano ya novemba 22, 2006 Jijini. Marehemu alikuwa ni mwanamuziki wa Tabora Srar  zamani Tabora Jazz au Segere matata iliyokuwa na makazi yake kule Tabora Lumumba kwenye makutano ya mitaa ya Rufita na mtaa wa Fundi. Kwa sasa Bendi hiyo inaitwa Tabora Star.  
Taarifa za kustua za msiba
 Ingawa taarifa hizo zilikuwa zimeenea Jijini tangu siku iliyofuatia ya Alhamis majira ya mchana wengi walizipata taarifa za kifo cha Kassim rythm katika vipindi vya michezo na kwenye taarifa za habari za televisheni.Ilishitua. Nilimuangalia Mzee Shem Ibrahim Karenga alipokuwa akitoa taarifa za msiba  kwenye Luninga, alikuwa amekosa ile nuru yake. Hilo lilitegemewa kama ambavyo imewatokea watu waliokuwa wakimjua marehemu Kassim walipopata taarifa za kifo chake. Kwa Mzee Shem Karenga hili ni pigo kubwa na ni zaidi, alikuwa na marehemu katika kazi na walikuwa maswahiba wakubwa kwa zaidi ya miaka 30. Umri wa mtu mwenye familia.
 Wasifu
  Sikumfahamu sana marehemu zaidi ya kuzifahamu kazi zake.  Siwezi kujinadi  kuwa nilifahamu. Tulimfahamu marehemu Kassim kwa kumuona kama ni mwanamuziki mtanashati, au mfua uji kwa lugha za enzi hizo. Jukwaani hata nje ya jukwaa hakuwa muongeaji kama marehemu Msafiri haroob aliyekuwa  Hakuwa mzungumzaji sana. Zamani wakati nasoma Tabora enzi zile za miaka ya sabini tulikuwa tunakwenda kuangalia  mazoezi ya Segere Matata. Wakati ule watoto au  wanafunzi hatukuruhusiwa kuingia Dansini hivyo mara nyingi kama kulikuwa na  dansi tuliishia nje . tuliusikiliza muziki kwa nje na mara nyingi tulikaa katika baraza ya mama mmoja maarufu sana Tabora mama Adeni. Mama yake (Ismail Aden Rage huyu wa Moro star). Mama huyu alikuwa na Hoteli iliyoitwa Tanzania Hotel iliyokuwa mtaa wa Rufita. kwa wale wanaojua Tabora na hulka zake, katika hoteli ile kulikuwa na Baraza kubwa sana ya kahawa. Tanzania hoteli ilikuwa pua na mdomo kutoka  Lumumba uliokuwa ukumbi wa Tabora Jazz.
 Hamu ya kwanza enzi hizo ilikuwa ni kuwajua wanamuziki. Hao ndio walikuwa nyota wetu stars. Vijana wa sasa nyota wao ni kina Eminem. Basi hapo ndipo nilimfahamu marehemu Kaka Kassimu na tangu enzi zile mpaka wakati nilipokuwa namuona alikuwa unaweza kusema hazeeki. Baada ya miaka 20 alibaki kuwa na umbo lile lile na sisi wengine tutaanza kuonekana kama tunalingana naye umri.
 Kassimu alibaki marehemu Issa Ramadhani na Mzee Kitambi walipoenda Msondo na Msafiri alipoenda Paselepa
 Nakumbuka mwaka 1978  Bendi ya Msondo walikuja Tabora walipoondoka baada ya kumaliza ziara yao  baadaye zikaja habari kuwa Marehemu Issa Ramadhani (Baba Isaya) na Mzee Hamisi Kitambi walikuwa wamekuja Dar na kwamba wamejiunga na Msondo. Kuna watu walilia kama kafa mtu kwa kuhama kwa wanamuziki hao.wakati ule hakikuwa kitu cha kawaida. Nakumbuka kuna rafiki yangu mmoja Mohammedi Hassan Kaombwe aliuliza kwani na Kassimu naye kaondoka! Alipojibiwa kuwa Kassimu yupo hajaondoka watu wote wakatuliza mioyo. Huyo ndio marehemu kassimu. Msondo Ngoma katika miaka ya 1980 ilinuniwa na wakazi wengi wa Tabora kwa kuwachukua wanamuziki Issa na Mzee Kitambi.
 Kazi zake
Hapa ndipo niliposema kuwa nimezifahamu na kuzisikiliza sana kazi zake hii ni kwa sababu niliipenda sana Segere matata, segua segua. Niliupenda pia muziki wake wa uliokuwa na mahadhi ya kimanyema na kisonge. Mahadhi ambayo hata marehemu Marijan alikuwa anapiga.
 Alishiriki kupiga gita la rythms katika nyimbo karibu zote huku Shemu  Karenga akipiga gita la solo na kuimba pamoja na kina marehemu Msafiri Habob aliyehamia Paselepa bbadaye miaka 1980. Marehemu Kassimu alipiga gita la rythm jinsi anavyotaka. Kwa wale wataobahatika kusikiliza wimbo wa dada helena uliopigwa na Tabora Jazz wanaweza kuelewa ninachozungumzia, gita lake ndio lilikuwa kiongozi katika wimbo huo. Nyimbo nyingine ni pamoja na Halima, Kilimo, Chakula kwa Jirani, Alhamdulilah, kazi ya kulima ndio maisha ya watu wote, samba yasika, dada Remi, dada Asha na 1 na na 2, dada zena, dada Helena jitulize,  Ruth, belaombwe, hasira hasara,  uliopigwa kwa staili ya kavasha na nyingi nyinginezo nyingi ukiwemo merina nihurumie. Zainab,   akasema kuwa

Kiigizo  kwa wanamuziki chipukizi
Moja kati ya sifa za wanamuziki wa zamani aliwemo marehemu Kassimu ni kuwa kiigizo. Wakati ule Tabora na hata mikoa ya jirani kama Kigoma , Rukwa na Shinyanga kila kijana alipenda awe kama Kassim, Shemu, Athuman Tembo au Salum Luzila.
 Wapo vijana wengi waliofuatia ambao muziki wa kaka zao kina Kasimu uliwavutia. Orodha ni ndefu, kina Juma Banduki aliyekuwa mpiga kinanda wa Mkote Ngoma na hatimaye Sikinde, kina  Madaraka Moris (kiwembe), Kibonge, kina Fransis aliyeanza kupiga gita akiwa na sare za shule ya  Kazima sekondari lakini akaweza kumudu masomo na muziki, yupo  kaka yangu Rehani Juma (Profesa wa munisa ndesa) na wengineo wengi ambao walivutiwa na kazi za wanamuziki hawa wakongwe kina kasimu.
 Buriani Kassim
Kassim umetangulia mbele ya haki ambako sisi sote tunakuja huko. Kwa kiasi nilichofahamu kazi yako isingekuwa haki kuacha kukuandikia taazia hii ewe kassim rythm. Kuna siku nilishawahi kumuambia komredi wangu mmoja anayeandikia Gazeti moja maarufu la wiki hapa nchini kuwa itafika siku watu watauliza hivi Shaaban Robert, Hukwe Zawose, Athuman Khalfan, Mathias Mnyapala, Abbas Mzee, Juma Kilaza, Salim Abdalla,  Patrick Balisidya au Marijan Rajab na Saleh Ramadhan Mwinamila ndio kina nani?
 Kassim kama mashujaa wenzako mmelifanyia kazi kubwa Taifa hili kupitia sanaa na ubunifu wenu, mkaitangaza nchi hii (njii hii)  ndani na nje ya mipaka yake. Mmefanya kazi kubwa lakini kama wenzako mmeondoka kimya kimya. Ndivyo walivyo watu wenye matendo makuu. Tuliwakumbuka kwa siku mbili tatu baadaye tukashika hamsini zetu. Tunayajua zaidi mashairi ya shake Spear ya mwaka 1600 kuliko mashairi ya Saadan Kandoro. Haya ni makosa makubwa. Tunapaswa tuwakumbuke mashujaa wetu ninyi  kama kielelezo cha shukurani. Wakati wengine waliopo Marekani sasa hivi wanatafuta asili zao root.  Sisi angalau tunaijua asili yetu basi tuanzie hapa. Buriani kassim, Msiba wako nimeutumia kama jukwaa la kuelezea kile kilichiokuwa kinaniganda kwa siku nyingi. Nisamehe kwa hilo. Tunakuombea duaa wakati huu tunauanza mwaka 2009.Buriani.. 

Maoni 1 :

Bila jina alisema ...

Nayathamini sana unayotuasa sisi wanamuziki wapya,yatubidi tuyatafakari na kuyafanyia kazi kwani ni mara chate sana kumpata mtu kama wewe kitime kutuelimisha.Hivi sasa vyombo vya habari kama magazeti,TV,Radio kuna rushwa tupu,ambayo na yenyewe kwa kiasi kikubwa inaumaliza mziki wa dansi kwani hela za kuhonga uwe nazo ili usikike hili nitakuomba uianzishe mada hii kwa mapana na uwazi,Enzi za wakongwe ulowataja kulikua hanuna Rushwa kwenye yombo vya habari kama ilivyo sasa!!Nakuomba tusaidiane maana jamaa watatumaliza kabisa sisi wasanii wa Ukweli!!Muziki wa Dansi tunaupenda na ndio maana tukaichagua kuwa kazi sasa hawa watu wanaomiliki hivi vyombo vya habari na wafanya kazi wao mtazamo wao uko kinyume na maadili kwa kupenda Rushwa ili kazi za wanamuziki zisikike!!