LAPF

LAPF
LAPF

Ijumaa, 8 Machi 2013

MWANAMUZIKI WA AFRO70, SALIM JAMES WILLIS =PART 1


TheDynamites..Salim wa kwanza kushoto

Salim wa pili kushoto, Paul Muhuto wa tatu toka kushoto. Seaview Hotel

Salim Willis ni mmoja wa wanamuziki waliowahi kupigia bendi ya Afro70, alianza kupata hamu ya kuwa mwanamuziki baada ya kuwa mpenzi mkubwa wa filamu za Elvis Presley, mwanamuziki mahiri wa muziki wa rock'n'roll aliyetawala anga za muziki wa dunia kwa muda mrefu, na hata baada ya kifo chake santuri zake bado zinauza kwa wingi zaidi ya wanamuziki wengi walio hai  mpaka leo. Moto huu wa kutaka kuwa mwanamuziki ulimfanya aanze kuhudhuria maonyesho ya bendi ya Wagoa iliyotengenezwa na wanafunzi wenzie wakati akisoma shule ya St Xavier(Kibasila). Hapo akawa kila bendi ikipiga yeye alianza kupiga marakasi, pamoja na ugomvi mwingi aliozua wakati akipiga chombo hicho kutoka kwa wanamuziki wa bendi hiyo aling’ang’ania na hatimae akawa mahiri kiasi cha kutakiwa kutokosa wakati wa maonyesho ya bendi hiyo ambayo yote yalifanyika pale shuleni. Kutoka shule ya St Xavier akahamia St Joseph ambako huko akakutana wapenzi wa muziki  wenzie na kuanzisha kundi la Dynamites akiwa mpiga drums. Kundi lake la Dynamites lilikuwa na wanamuziki   wafuatao; Abdallah Boja, Bashir Farahani, Mohamed Manyika, Salha, na  yeye Salim katika drums. Kwa kadri ya mfumo uliokuwa wakati ule kulikuwa na vikundi vingi vikiwa na majina lakini havikuwa na vyombo, kwa hiyo vijana wa vikundi hivi walifanya mazoezi kwa kutumia magitaa baridi na hatimae kuzunguka kufuata bendi kubwa na kupata nafasi ya kutumia vyombo vya umeme pale bendi hizi zinapokuwa katika mapumziko. Kulikuwa na kawaida ya bendi kupumzika nusu saa katika kila onyesho. Hivyo Salim alikuwa katika  kikundi cha Dynamites na kuzunguka kwenye mabendi kutafuta nafasi ya kuachiwa kupiga vyombo vya moto.
Alipohamia St Joseph ndipo wakati huohuo alipoanza kufuatilia bendi ya Sparks ambayo ilikuwa ikipiga Gateways, na yeye kwa kuwa alikuwa akiishi Gerezani aliweza kusikia muziki wa bendi hiyo na kuanza kuhakikisha hakosi kwenye maonyesho ya bendi hiyo. Nako huko akakimbilia chombo chake cha maracas, hapa wakamtambua kuwa anaweza japo alikuwa mfupi sana akawa anawekewa kiti cha chuma awe anaonekana. Hapa akakutana na Paul Mhuto na urafiki wao wakaanzisha kundi la Gypsies. Huu ukoo wa akina Mhuto walikuwa wanamuziki wazuri wote wakijua kupiga kwa umahiri vyombo mbalimbali,  na Salim nae akaanza kuwa na hamu ya kujifunza gitaa hasa kwa ajili ya kuupenda sana wimbo maarufu wa Besame mucho. Akafikia mpaka akaweza kupiga wimbo huo kwa kidole kimoja, bila hasa hata kujua ni chord gani hupigwa wimbo huo, lakini hii ilikuwa hatua kubwa katika kuonyesha nia ya kuweza kupiga wimbo huo. Mmoja wa wanamuziki wa Sparks akampa kitabu cha kujifunzia chords za gitaa, akampa pia na gitaa aende nalo nyumbani akajifunze. Wakati huo huo akawa anajiendeleza katika drums chini ya mwalimu wake George Muhuto, ambaye alikuwa akimuelekeza beats fulani na kumpa homework kuwa lazima ajue hizo beat kufikia kesho yake. Na kwa juhudi zake mwenyewe za kuanza kufuatisha mapigo ya santuri za vikundi mbalimbali kama The Famous Flames ya James Brown akawa mpigaji mahiri. Akawa anaruhusiwa kupiga nyimbo za polepole na kuruhusiwa kuwa kwenye jukwaa mapema kwani ilikuwa lazima arudi kwao kabla ya saa nne. Wakati wote huo alikuwa akitoroka tu nyumbani kwao kwa kupitia tundu alilolitengeneza kwa kufumua vigae vya nyumba yao ambayo ilikuwa moja ya kota za relwe. Baba yake alipogundua akamtuma mfanya kazi wao mmoja amfuatilie ajue anaishia wapi , mfanya kazi akarudi na jibu kuwa jamaa anaishia kwenye muziki na anapiga sana. Baba yake hakuchukia ila alimwambia awe anagonga  anapitia mlangoni. Muda si mrefu baada ya hapo bendi ya Sparks ikafa ikazaliwa The Comets. Hapo ndipo likaanzishwa pia kundi la Gypsiys ambalo alikuweko yeye Salim Willis, Paul Muhuto, Charles Sabuni, Omari Sykes na Abraham Sykes na Mzanda. Kwa vile kundi lilikuwa halina vyombo, wakawa hawana mahala pa kufanyia mazoezi basi wakaamua kuwafuata Afro70 ambao wakati huu walikuwa wakipiga Princes Bar..........

Maoni 1 :

Bila jina alisema ...

Nini siri ya kifo cha mwanamuziki Gobby? Kitime umeuliza swali la msingi sana ambalo hujalijibu.