LAPF

LAPF
LAPF

Jumatatu, 1 Aprili 2013

STEEL BEAUTAH, SLIM ALLY WAKALI WA FUNKY MUSIC

Hodi Boys

Slim Ally


Sal Davis

Steel Beautah

-->
Kama ulikuwa kijana miaka ya 70 lazima ulikuwa unaifahamu ile miamba ya muziki wa funk iliyokuwa ikiwika nchini Kenya. Steele Beauttah, Kelly Brown, Slim Ali, Ishmael Jingo na wengine wengi. Katika ukumbi wa Starlight Club katikati ya jiji la Nairobi uliofunguliwa rasmi May 15 1965, mwenye ukumbi huo Robbie Armstrong aliwezesha ukumbi kuingiza kasi cha watu 12,000 kila mwezi kwa kuzikaribisha bendi zilizokuwa kali kama The Ashantis, Air Fiesta Matata, The Cavaliers, kufanya maonyesho katika klabu hiyo. Wanamuziki wa bendi hizi waliiga ‘swaga’ za mwenyewe Godfather of Soul marehemu James Brown, uvaaji utanashati na hatimae uimbaji, kati ya wanamuziki wa kwanza kuwa wafuasi wa JB alikuwa ni Salim Abdullah Salim ambaye tunamfahamu kwa jina la Sal Davis ambaye vibao vyake kama Unchain my heart, Makini akili vilitikisa sana anga za Afrika mashariki miaka ya 60. Huwezi kuacha kumtaja Kelly Brown mwanamuziki mwingine wa Kenya ambaye alihamia Ujerumani na kuishi huko mpaka kifo chake 1989.  Muziki wa Boogie ndio ulitawala kwa vijana huu ulikuwa muziki uliopigwa mchana kuanzia saa nane hadi saa 12 jioni. Viongozi wengi hawakupenda Boogie kwa madai kuwa linaharibu vijana, na pia mitindo ya mavazi na swaga za wakati huo ziliongeza wasiwasi wa  viongozi hawa, vijana wakiwa na viatu vya raizon, nywele kwa mtindo wa Afro, suruali za bell bottom , na mashati ya kubana mtindo wa slim fit vilikosesha sana usingizi wazee. Lakini muziki uliopigwa wakati huo ulikuwa ni wa hali ya juu sana, kibao kama You can do it cha Slim Ally au Fever iliyotungwa na Ishmael Jingo ni ushahidi tosha. Bahati mbaya wanamuziki wake walipotea mmoja mmoja na wengine kufa vifo vya kudhalilika katika umasikini.
Steele alikuwa bandleader wa kundi la Air Fiesta Matata. Kundi hili lililokuwa na wanamuziki 10, lilikuwa bingwa wa muziki wa funk kiasi cha kuweza kupiga na Miles Davis 1969, na alilipenda mpaka alilialika kundi zima kwenda kupiga nae Marekani. Mwaka 1971 BBC World service ililitaja kama bendi bora Afrika. Steele alianza madawa ya kulevya kama walivyoanza wanabendi wenzie baada ya kupata tour ya kuzunguka ulimwengu 1974. Bendi ilianza kwa kwenda Hong Kong, kasha Uswisi na Uingereza. Wakati wakiwa tayari kwa  safari ya kurudi Kenya wakiwa na vyombo vipya na vizuri meneja wao Mogosti akawaambia ana tatizo la viza kwa hiyo watangulie yeye atawafuata Kenya kwa ndege iliyokuwa inafuata. Hakuonekana tena, naye ndie alikuwa na fedha na vyombo, ilisemekana alihamia Jamaica, Air Fiesta Matata ikavunjika baada ya hapo. Tatizo la madawa ya kulevya lilimuandama Steele kiasi cha kuamua kufa kwenye mtaro wa maji machafu lakini wanae walimuokota na kumsaidia baada ya muda akaokoka. Mpiga gitaa wa Matata Sammy Kagenda naye pia alidhurika na madawa aina ya heroine kiasi cha kutokukumbuka hata nyimbo alizotunga mwenyewe, na hata alipoonyeshwa picha zake akiwa kwenye maonyesho alikana kuwa hakumbuki kuweko katika shughuli hiyo.

YOU CAN DO IT FEVER MAKINI

Hakuna maoni: