LAPF

LAPF
LAPF

Jumapili, 18 Agosti 2013

AHMAD KIPANDE WA KILWA JAZZ BAND


 
AHMED KIPANDE

Ahmed Kipande alizaliwa Kilwa Kivinje mwaka 1937, huko Kilwa Kivinje. Na baada ya  mama yake kufariki baba yake akahamia Dar es salaam na Ahmed akajiunga na masomo katika shule ya Wavulana ya Uhuru maeneo ya Kariakoo, Dar es Salaam ambapo alisoma hadi darasa la nne. katika makuzi yake aliweza kusikia muziki wa aina mbalimbali na pia akapata nafasi ya kusikiliza muziki kutoka santuri zilizofahamika sana kama GV ambazo zilikuwa na muziki toka Cuba na pia kuanza kuwasikia wanamuziki wa Afrika mashariki kama Fundi Konde. na kuanza kuwa na hamu ya  kuwa wanamuziki.
Santuri hizi za GV zilipata umaarufu katika sehemu kubwa Afrika na kusaidia kupanda mizizi ya muziki wa kisasa wa Afrika mpaka leo. Na hata leo nyimbo za GV zinaendelea kujitokeza katika muziki wa kizazi hiki. Na kuendelea kupata umaarufu, kwa mfano wimbo wa Sawa Sawa Saware ni kutoka mmoja ya wimbo wa GV uliojulikaa pia kama Peanut Vendor. 
Kwa msisimko alioupata Kipande akaanza kujifunza mwenyewe vyombo mbalimbali likiwemo gitaa, ukulele, banjo na violin na hatimae saxaphone ambayo ndio ilikuja kumpa umaarufu mkubwa.  Mwaka 1953 Kipande alijiunga na  Tanganyika Jazz akiwa mpiga violin. Tanganyika jazz lilikuwa kundi la mtu binafsi na wakati huo muziki ulikuwa ukipigwa kama kitu cha kujiburudisha na kuendeleza fani kwa wanamuziki, haikuwa ajira wala njia ya kupata fedha. Bendi hiyo ilikuwa na vidhaa vifuatavyo magitaa, violin, ngoma, trumpet na saxaphone.
VIOLIN

KUSHOTO BANJO, KULIA MANDOLIN

UKULELE
Bendi ilikuwa ikiongozwa na Zimbe Kidasi,makao yake makuu yakiwa katika mtaa wa New Street, mtaa ujulikanao sasa kama mtaa wa  Lumumba.
Mwaka 1958 aliamua nae kuwa na bendi, na ndipo Kilwa Jazz Band ikazaliwa. Hivyo akanunua saxaphone , magitaa, na kutengeneza ngoma zake, wakati huo ngoma zilikuwa zikitengezwa kwa kutumia mapipa.  Kipindi hicho bendi ambazo tayari zilikuwepo katika jiji la Dar zilikuwa Homeboys Jazz band, Dar es Salaam Jazz band, na Cuban Marimba Branch, hili lilikuwa tawi la Cuban Marimba ya Morogoro, ambayo inaonekana ilikuwa na matawi mengi kwa karibuni nimepata taarifa ya Cuban Marimba Branch ya Kilosa (taarifa ya bendi hii inakusanywa). Kati ya wanamuziki wake wa kwanza alikuweko mzee Zuberi Makata ambaye alifundishwa na Kipande upigaji wa sax. Bendi ilikuwa ikipiga mitindo ya aina nyingi kama vile rumba, samba bolelo  na chacha. Na kupata umaarufu kutokana na tungo zake nzuri ambazo nyingine zilihamasisha kudai Uhuru. Kwa heshima hii bendi ilikuweko kwenye kilele cha sherehe za kupata Uhuru 1961 pale Uwanja wa Taifa.
KILWA JAZZ BAND
makao makuu ya Kilwa jazz Band yalikuwa katika kona ya mtaa ya Jangwani na Mhoro. Baadhi ya wanamuziki waliopitia bendi hii katika miaka ya sitini na sabini ni;
Ahmed Kipande, kiongozi wa bendi, mwimbaji, mtunzi wa nyimbo, na mpuliza saxophone.
Zuberi Makata, Juma Town, Kisi Rajabu saxophone
Duncan Njilima na Hassan Shabani ‘Kichwa’(kaka yake Ahmed Kipande) walipiga solo.  
 Juma Mrisho aka Ngulimba wa ngulimba, Kassim Mapili na Ahmed Kipande waimbaji.
Rythm Gitaa lilipigwa na Abdull Ngatwa, Abdallah Kanjo alipiga tumba. Kwa kipindi kirefu bendi ilipata mchango mkubwa toka kwa Waziri wa enzi hizo Mzee  Nangwanda Lawi Sijaona, ambaye alifanya mengi katika muziki wakati huo kwani hata wanamuziki wa bendi ya wanawake Women Jazz na hata Vijana Jazz wote wanahistoria ya ufadhili wa Mzee huyu.
  Ahmedi Mohammed Kipande afariki dunia  Aprili 27, 1987 a kuzikwa kesho yake kwenye  makaburi ya Tandika Maguruwe.

Hakuna maoni: