LAPF

LAPF
LAPF

Jumanne, 14 Januari 2014

FRANKLIN BOUKAKA WA LE BUCHERON AFRIKA


FRANKLIN  alikuwa mtoto wa mwanamuziki Aubin Boukaka wa kundi la "The Gaiety ", na mkewe Yvonne Ntsatouabaka aliyekuwa MC maarufu  kwenye misiba na pia alikuwa mwanamuziki muimbaji.  François Boukaka aliyekuja julikana kama Franklin alizaliwa tarehe  10 Oktoba, 1940. Yeye ndie alikuwa mtoto wa kwanza katika familia ya watoto wanane wavulana watatu na wasichana watano. Elimu yake yote aliipata katika shule mbalimbali nchini kwake Congo Brazzaville. Franklin  alianza mambo ya muziki 1955 katika kundi lililojiita Sexy Jazz lililoongozwa na Miguel Samba, baadae akaanzisha kundi la Negro Band. Hatimae katika safari yake ya muziki akaungana na wakali wengine kama  Edo Clary Lutula, Jeannot Bombenga, Tabu Ley , Mutshipile "Casino", André Kambite " Damoiseau ",  Papa Bouanga, Charles Kibongue katika lile kundi maarufu la African Jazz, sauti ya Franklin imo katika nyimbo kama  Mwana mawa , Catalina cha cha na Marie José zilizotungwa na Tabu Ley. Mwaka 1959 kundi la African Jazz lilimeguka baada ya wanamuziki wengine walipohamia Brussels wakifuatana na wanasiasa wa Kongo kwenye mazungumzo ya awali ya uhuru wa Kongo. Wanamuziki wote waliobaki akiwemo Jeannot Bombenga,  kasoro Tabu Ley wakajiunga na kuanzisha kundi jingine lililotingisha Africa lililoitwa Vox Africa, Franklin Boukaka na Jeannot Bombenga wakiimba. Baada ya hapo Franklin akaaliacha kundi hili na kurudi kwao Brazzaville ambako  1962 akawa mmoja wa wanamuziki wa Cercul Jazz, band iliyoanza miaka ya 50 ikiwa chini ya chama cha vijana kilichokuwa kikipata ufadhili wa serikali ya Ufaransa, chama hicho kiliitwa Cercule Culturel de Bacongo.  Hatimae Boukaka alikuja kuwa kiongozi wa chama hiki na kikawa na umaarufu wa mkubwa. Wimbo wa bendi hiyo "Pont Sur le Congo" (Daraja juu ya Mto Congo), wimbo ambao ulikuwa una hamasisha kuunganika kwa Congo Kinshasa na  Kongo Brazzaville baada ya nchi hizo kupata uhuru. Wimbo uliopata umaarufu kuliko nyimbo zote za bendi hiyo. Baadaye Franklin akiwa na gitaa lake kavu akaanzisha kikundi ambacho kilikuwa na wapiga marimba wawili akaweza kufanya ziara kadhaa hata nje ya nchi yake na kundi hili. Mwaka 1970 ndipo Boukaka  alipo rekodi nyimbo 12 zilizopangwa vyombo na Manu Dibango na hapo ndipo nyimbo Nakoki na Le Bucheron zilipopatikana. Baada ya hapo Franklin alijiunga na wenzie waliotaka kuipindua serikali ya Congo Brazzaville wakati huo ikiwa chini ya Rais Marien Ngouabi(aliyetuletea suti za Ngwabi). Jaribio hilo lililofanyika tarehe 22 February 1972 lilishindwa na siku chache baadae kifo cha Boukaka kilitangazwa.