LAPF

LAPF
LAPF

Ijumaa, 4 Julai 2014

IJUE BEMBEYA JAZZ YA GUINEA


Bembeya Jazz, hutajwa kama ni nguzo ya historia ya muziki wa kisasa wa Afrika Magharibi. Bendi hii ilianza vipi?
Mwaka 1958 kulikuweko na kura ya maoni katika nchi zilizotawaliwa na Wafaransa Afrika Magharibi ambapo wananchi waliulizwa kama wanataka kuendelea kuwa chini ya Ufaransa, Guinea ndio nchi pekee iliyokataa. Sekou Toure akachaguliwa Rais  wa nchi hiyo, na kati ya vitu alivyoanzisha mara  moja ilikuwa ni Bendi ya Taifa iliyoitwa Syli National Orchestra. Bendi hii iliyokuwa na maskani katika jiji la Conakry iliendelea kukuwa na kuwa kubwa hatimae  mwaka 1961 ikagawanyika katika makundi mawili Bala et ses Balladins na Keletigui et ses Tambourinis. Kutokana na  upenzi wake wa sanaa Sekou Toure alitengeneza bendi za mikoani, ambazo alizifadhili kwa vyombo na fedha. Katika jiji la Beyla kusini mashariki mwa Guinea kwenye mwaka 1961 Gavana wa mkoa huo Emile Conde alianzisha kakundi kake kadogo kakiwa na gitaa moja tu kavu na bila uzoefu mwingi lakini taratibu kakanza kujitokeza. Kabendi haka toka mikoani kalishinda mashindano mengi na kakajulikana sana Conakry, hatimae chama tawala kiliitaka Bembeya ihamie Conakry mwaka 1965, na kakataifishwa na kufanywa bendi ya Taifa kama zile nyingine mbili. Bendi hii ilianza kwa kuitwa Beyla Jazz, lakini siku moja April 1961, katika mkutano wa bendi wakaamua kujiita Mbembeya Jazz
 Wakati huo Guinea kulikuwa na aina mbili za wanamuziki wale waliopiga muziki kutumia muziki wao wa  asili na wale waliotoka kwenye mashule ya Kifaranza amabo walipiga muziki wa asili ya Cuba, kuna amri iliyotolewa na serikali kueleza wanamuziki wapige muziki kutokana na vionjo vya kwao kwenye katikati ya miaka ya 60. Hivyo ukisikia nyimbo za Bembeya Jazz kabla ya hapo unasikia vionjo vya Cuba kama vile Whisky Soda na Mamiwata  ni mfano wa upigaji huo, baada ya hapo na mpaka ilipokuja kurekodi mara ya mwisho bendi hiyo imekuwa na vionjo vya muziki wa asili wa  Guinea
Wakati wa uhai wa Sekou Toure, nchi hiyo ilianzisha record label iliyoitwa Syliphone, ilikuwa label ya Taifa, jambo hilo halikuwahi kufanyika popote Afrika, Tanzania ilijaribu kuiga mfumo huu na iliweza kutoa kazi chache kwa kutumia Tanzania Film Company na  kuwa na label kama TFC na Sindimba.
 Bahati mbaya hali ya uchumi wa Guinea ulipoharibika miaka ya 70 label hiyo ambayo iliyoweza kutoa album 80 ilikufa, na ndipo wanamuziki wa nchi hiyo wakaanza kuelekea Ufaransa. Sekou Toure alifanya kazi kubwa kwa nchi yake kwa upande wa sanaa na kuweza kuifanya Guinea kuwa kati ya nchi zilizoongoza Afrika katika utamaduni wa muziki. Bahati mbaya taratibu alianza udikteta na watu waliompinga wakaanza kupotea au kuuwawa, kama ilivyotokea kwa Fodeba Keita msanii aliyeanzisha kundi la kwanza la Ballet nchini Guinea na Sekou Toure akamfanya Waziri wa Mambo ya Ndani, lakini kufikia mwishoni mwa miaka ya 60, Sekou Toure akawa na wasiwasi kuwa Fodeba atampindua, basi alimfunga na hatimae mtu huyu akapotea, haijulikani alikufa vipi au lini. Pamoja na udikteta huo alikuwa tofauti na Mobutu. Alikuwa mzalendo hakuwa fisadi wa kuiba mabilioni na kuyatorosha nje kama Mobutu, bali aligeuka kuwa katili wa kulinda utawala wake. Pamoja na maelfu ya Waguinea kuikimbia nchi yao kutokana na utawala huu wanamuziki wachache walimlaani kwani wengi walifaidika na fadhila zake katika tasnia ya muziki.

Kufikia mwaka 1980 Bembeya Jazz  ilikuwa haipigi tena maonyesho ya kawaida  labda kwa kukodishwa. Kati ya mambo makubwa ya kusikitisha yaliyokikumba kikundi hiki ni kifo cha muimbaji wao Demba Camara ambaye alifariki gari lao lililokuwa likiendeshwa na dereva wa bendi kupinduka wakiwa safarini, katika gari hilo pia alikuweko Sekou 'Bembeya' Diabate (Diamond Finger). Demba alikutwa ametupwa nje ya gari walipowasili wanamuziki wengine waliokuwa katika gari jingine.
Sekou 'Bembeya' Diabate

Sekou 'Bembeya' Diabate bado anafanya maonyesho lakini hasa nje ya Guinea
Kwa wale wanaojua historia ya sanaa ya Tanzania watajua kuwa Tanzania iliiga baadhi ya taratibu za sanaa za Rais Sekou Toure wa Guinee, kuanzishwa kwa kundi la sanaa la Taifa na hata kuanzishwa kwa bendi ya wanawake,  yalitokana na ziara za Rais huyo hapa kwetu ambapo alikuja kasindikizana na kundi kubwa la wasanii wa kundi la Taifa.

Hakuna maoni: