LAPF

LAPF
LAPF

Jumatatu, 18 Agosti 2014

ALIKOPITIA MWANAMUZIKI HUSSEIN JUMBE HAKUKUWA RAHISI


Nchini Tanzania, sanaa ya muziki wa dansi ni miongoni mwa kazi kadhaa za sanaa zinazoaminika kuwa ni za kujitolea zaidi.
 Inaaminika hivyo kutokana na ugumu wa kazi yenyewe ukilinganisha na mafanikio yake.
 Hapa nchini hadi kuyafika mafanikio, wanamuziki wengi kwanza hupitia taabu, mashaka na vikwazo kemkemu kiasi ambacho kama mtu si mstamilivu atakata tamaa 'mchana mchana!'
 Tunayo mifano mingi inayoweza kuyakinisha hayo, ila mfano mmoja  wapo ambao ndio wa karibu zaidi ni mwanamuziki Hussein Suleiman Jumbe 'Mzee wa Dodo' kama anavyojulikana kwa wengi.
 Jumbe ambaye alizaliwa miaka takriban 51 iliyopita, ni mwanamuziki nguli aliyejaaliwa kipaji adhimu cha sauti ya uimbaji. Ni mtunzi hodari pia mwenye tungo zilizojaa hisia na zinazosisimua zaidi, ambazo mara nyingi hugusa kila rika la watu.
 Kwa hivi sasa, nguli huyo aliyepata elimu yake ya msingi katika Shule za Uhuru Mchanganyiko Primary na Muslimu Secondary School zote za Dar es Salaam, anamiliki bendi yake mwenyewe inayojulikana kama Talent Band.Akizungumza leo asubuhi nyumbani kwake, Temeke Mwembeyanga, jijini Dar es Salaam, Jumbe anasema aliamua kujifunza muziki baada ya kuvutiwa na nyimbo za marehemu Marijani Rajab 'Jabali la muziki'.
 "Nilikuwa natembea na radio yangu kwa ajili ya kusikiliza nyimbo za Marijani, enzi hizo akiwa na bendi ya Safari Trippers," anakumbuka Jumbe na kuongeza kuwa vibao vilivyokuwa vikimpagawisha zaidi ni 'Roza Nenda Shule', 'Mwalimu Nyerere' na 'Nani Mchokozi'.
 Anasema, kabla nyimbo hizo hazijatoka kwenye radio, alizijua na kwamba alikuwa akiziimba kila alipokaa ambapo wakati huo ndio kwanza alikuwa bado yuko shule ya msingi.
 Anakumbuka zaidi kuwa kutokana na mapenzi yake kwa Marijani, mara kwa mara alikuwa anatembelea maonyesho yake na kila Jumapili alikuwa hakosi kwenda katika ukumbi uliokuwa ukijulikana kama ' Princess uliokuwa maeneo ya Mnazi Mmoja kwenye 'bugi dansi' dansi la mchana siku za Jumapili lililoisha saa kumi na mbili jioni, ambapo kiingilio chake kilikuwa shilingi tano tu.
Mnamo mwaka 1979, wakati akiwa darasa la nne alijiunga kwa siri na kundi la Orchestra Siza, ambalo maskani yake yalikuwa Mtaa Ruvuma, Temeke, jijini Dar es Salaam ambako pia ndiko alikokuwa akiishi yeye.
 Hapo katika kundi la Orchestra Siza, Jumbe anasema ndiko kwa mara ya kwanza alikokutana na mwanamuziki Roshi Mselela waliyepatana nae kupita kiasi, akawa bado anaendelea na muziki kwa siri.
 Lakini kwa vile dunia haina siri, mwaka mmoja tu baadaye wazazi wake wakagundua janja yake ya kujiingiza katika muziki na kuzembea masomo shuleni, wakamgombeza na kumpiga marufuku kufanya muziki.
 Hata hivyo, mwenyewe Jumbe anakiri kwamba kuishi bila kujihusisha na masuala ya muziki ilikuwa ngumu kwake, mwaka 1981 akajiunga tena kwa siri na kundi lingine la muziki wa dansi, Asilia Jazz ambalo lilikuwa likimilikiwa na Baraza la Muziki Tanzania (BAMUTA).
 "Safari hii, baba alipokuja kugundua kuwa naendelea kujishughulisha na muziki, alinichukua na kunipeleka kufanyakazi katika kiwanda cha plastiki," anasimulia Jumbe na kufafanua kuwa hapo aliajiliwa  kama Msimamizi wa Uzalishaji (Production Foremen).
 Huku akicheka, Jumbe anasema kuwa aliacha kazi kiwandani hapo mara moja baada ya kuona anakosa muda wa mazoezi ya muziki, ambapo kilichofuata ni familia yao yote kumtenga na kumsusa kabisa.
 "Nakumbuka katika kipindi hicho nilichosuswa na familia, nilitaabika kwa dhiki mpaka nilifikia hatua ya kuvaa viraka," anasema Jumbe.
 Anasema kuwa, katika jitihada zake za kuhakikisha hautupi mkono muziki, mwaka 1983 alilikimbia jiji la Dar es Salaam na kwenda Tabora kutafuta bendi atakayoitumikia kwa kujinafasi. Huko akapokewa na mkongwe Shem Kalenga ndani ya bendi ya Tabora Jazz ambako pia alikutana na mwimbaji Mohammed Gotagota ambaye kwa sasa ni marehemu.
 Tabora Jazz alikaa kwa miaka miwili, akachomoka akatokomea Musoma, Mara. Huko alikaa mwaka mmoja tu wa 1985 na ilipofika 1986 aliamua kurejea Dar es salaam kwani alikuwa amepokea taarifa ya msiba wa baba yake mzazi.
 "Nilipowasili, nilikuta tayari baba amekwishazikwa," anasikitika Jumbe na kusema kuwa baada ya hapo hakuona haja ya kuwa mbali na familia hivyo alimfuata Gotagota aliyekuwa bendi ya Urafiki wakati huo,nae akamuunganisha na kuwa muimbaji wa bendi hiyo.
Akiwa Urafiki Jazz 'Wana Chakachua' iliyokuwa ikiongozwa na Juma Mrisho 'Ngulimba wa Ngulimba', ndipo Jumbe alipoanza kudhihirisha makali yake katika utunzi kwani aliporomosha kibao kizito kilichokwenda kwa jina la 'Usia wa Mama'.
 Oktoba 17, 1987 aliitwa na mtu asiyemfahamu ambaye alimweleza kuwa amependezwa na uimbaji wake hivyo siku hiyohiyo aende makao makuu ya Mlimani Park yaliyoko karibu na Chuo Kikuu Dar es salaam. Yule mtu alikuja kumtambua baadaye kuwa kumbe alikuwa Hassan Rehani Bichuka 'Super Stereo'.
 “Wimbo wangu ya kwanza kabisa kutunga nikiwa na Wana Mlimani Park ni ule usemao 'Hisia za Mwanadamu' ambao mwaka 1990 ulishiriki mashindano ya nyimbo kumi bora na kushika nafasi ya tatu, ambapo nafasi ya kwanza ilinyakuliwa na bendi ya MK Group 'Ngoma za Magorofani’ na ya pili ikatwaliwa na Salna Brothers.
 Alidumu Mlimani Park kwa muda mrefu na kushiriki kuimba na kutunga vibao vingi vikali ambavyo baadhi yake ni ‘Epuka No2’, ‘Nuru ya Upendo’, ‘Shamba’, ‘Mtoto wa Mitaani’, ‘Chozi la Kejeli’, ‘Nachechemea’ na ‘Isaya Mrithi Wangu’ ambazo kila moja kwa wakati wake ilitikisa vilivyo.
 Mwaka 2002, aliondoka DDC na kujiunga na TOT Plus 'Achimenengule', ambapo kama kawaida yake, akiwa na kundi hilo lililokuwa chini ya Mbunge wa Mbinga Magharibi, Capt John Damian Komba, Jumbe aliporomosha vibao viwili moto wa kuoteambali.
 Vibao hivyo ni 'Gunia la Mazoezi' na 'Nani Kaiona Kesho' ambavyo vyote viko katika albamu moja ya ‘Sarafina’ iliyofyatuliwa mwaka huohuo 2002 na ambayo ilikuwa na jumla ya nyimbo sita.
 Jumbe alidumu TOT kwa miaka miwili, akatoka na kwenda kujalibu upepo Msondo Ngoma Music alikokutana na wakongwe we dansi kama vile Muhiddin Gurumo na Tx Moshi William ambao kwa sasa wote ni marehemu.
 Akiwa na Msondo, Jumbe alifanya vitu vizito kwenye albamu iitwayo ‘Ajali’ aliposhiriki kuimba katika nyimbo zote akitumia ufundi wa njia ndogo ya sauti ujulikanao kitaalamu kama 'Minor' na kutunga vibao 'Transfer' na 'Sumu ya Ufukara'.
 Tofauti na wanamuziki wengine wengi wanapohama bendi kuikashifu, Jumbe anaisifu Msondo kwa kusema kuwa ni bendi ambayo wanamuziki wake hawana majungu, fitina wala nyoyo za chikichiki.
 "Msondo wenzetu wanapendana halafu lao moja, hawana majungu hata kidogo," anasema Jumbe anapoulizwa kuhusu bendi hiyo inayotumia mtindo wa 'Mambo Hadharani'.
 Hivi sasa, Jumbe ambaye ni baba wa familia mwenye watoto wanane na mkewe Zakhia Jumbe, anayekiri kuwa maendeleo katika muziki ni 'matokeo', amepata mafanikio makubwa hasa baada ya kuanzisha bendi yake.
Tayari Talent Band ina albamu tatu ambazo ni ‘Kwangu ni Wapi’, ‘Subiri Kidogo’ na ‘Kiapo Mara Tatu’, huku hivi sasa akiwa anapika albamu nyingine itakayokusanya vibao vikali kama ‘Nyumba ya Urithi’, ‘Kaolewa Ramadhani Kaachika Ramadhani’ na ‘Ukienda Kuomba Mboga’.  Ndani ya vibao vyote kwenye albamu zilizotangulia za Talent Band, Jumbe ameonyesha ukomavu mkubwa kisanii kuanzia ujumbe hadi ala na kumfanya afanikiwe kupata maendeleo makubwa zaidi ya alipokuwa mwajiriwa.

 

Hakuna maoni: