LAPF

LAPF
LAPF

Alhamisi, 28 Agosti 2014

MFAHAMU MKONGWE WA SAXOPHONE RASHID PEMBE

RASHID PEMBE


 “TUKIO la kuutumikia Umoja wa Vijana kwa muda wa miaka 18 na kulipwa mafao ya sh. Mil 1.6, baada ya kustaafu, ndilo linalosumbua kichwa changu hadi leo, ambalo kiukweli sitakaa nikalisahau,” ndivyo anavyoanza kueleza Rashid Pembe.
Pembe ni kati ya wanamuziki nguli wa miondoko ya Dansi, aliyetokea mbali hadi sasa ambapo anaonekana amepata mafanikio kiasi kupitia sanaa hiyo.
Mwaka 2005 aliomba kustaafu kuitumikia bendi ya Vijana Jazz aliyokuwa nayo tangu Aprili, 1987, baada ya kuona imeanza kuyumba na kupoteza mwelekeo na kilichomkuta ndio hicho ambacho wakati fulani aliwahi kujutia kuwa mwanamuziki wa Dansi.
Kwa sasa Pembe anamiliki bendi yake binafsi, inayojulikana kama Mark Band, ambayo chanzo cha jina ‘MARK’ ni herufi moja moja za majina ya mwanzo ya wanamuziki wanne wanzilishi wa bendi hiyo.
Wanamuziki hao na nafasi zao kwenye mabano, ni pamoja na Mgazija (Bass), Alex (Solo), Rashid (Saxophone) na Karamazoo (Saxophone).
Mark Band iliasisiwa rasmi mwaka 2006, ambapo baada ya kuiunda, waliamua kuwaongeza wanamuziki wengine kama Said Majivu (Drums), Said Makelele (Tarumbeta) pamoja na Noel Minja na Balusi Kitembo ambao ni waimbaji.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Pembe anasema kuwa, kama ilivyo kwa bendi nyingine nyingi, walipoanzisha bendi hiyo walikumbana na changamoto kemkemu, ikiwa ni pamoja na kukodi vyombo kwa gharama kubwa.
“Hata hivyo, Mungu alitujalia kwani baadaye tulipata mkataba wa kutumbuiza siku tatu katika wiki, kwenye Hoteli ya See Criff, jijini Dar es Salaam, tukaanza kujipanga kwa ununuzi wa vyombo vyetu wenyewe,” anasema Pembe.
Anamtaja Waziri wa zamani wa Mambo ya Ndani, Mheshimiwa Mohammed Seif Khatibu kuwa ni kati ya watu waliochangia kuwakwamua ndani ya Mark Band kwa kuwaombea mkopo wa sh. Mil 3, kwenye Hoteli ya See Criff walioilipa polepole kwa kufanya shoo hapo.
Waliitumia pesa hiyo kwa kuchanganya na nyingine walizipata kupitia maonesho yao mengine na kununua vyombo kidogo kidogo hadi sasa wanapomiliki vyombo vyenye thamani zaidi ya sh. Mil 50.
Mwaka 2010 waliingia mkataba na Kampuni ya Kijerumani iitwayo ‘Mother Africa’ wa kutumbuiza nchi mbalimbali kama vile; Misri, Sweden, na nchi za Amerika ya Kusini kama vile Chile na Peru na pia  Ufaransa pamoja na Ujerumani yenyewe.
“Tumekuwa na maisha ya namna hiyo kwa muda mrefu sasa, ya kutumbuiza nje, huku hapa nchini tukifanya shoo nyakati za likizo zetu tu,” anasema Pembe.
Pembe anasema, tayari kwa upande wa nyimbo, Mark Band imeshafyatua albamu nzima, ambapo ni kibao kimoja tu kiitwacho ‘Matukio’ ndicho walichokisambaza kwenye vituo mbalimbali vya radio na runinga hapa nchini.
Vibao vingine kwenye albamu hiyo waliyoirekodia katika Studio za Bakunde Production, jijini Dar es Salaam, ni ‘The Girl From Tanzania’, ‘Baba Kaleta Panya Remix’, ‘Amani’, ‘Anjela’ na ‘Pombe’.
Pembe anasema, mafanikio ndani ya Mark Band ni kumiliki vyombo vya thamani, kuwa na akaunti nono na kujulikana duniani kote, huku mafanikio kwa upande wake ikiwa ni kuwasomesha wanawe na kuanza kuwanunulia viwanja kila mmoja na chake.
Akielezea namna alivyojifunza muziki, Pembe anasema kuwa mwaka 1981 alijiunga na Jeshi la Polisi kama fundi ujenzi, baada ya kumaliza masomo yake ya Sekondari.
“Nikiwa Polisi, wakati najiandaa kupelekwa chuo cha ufundi, Marehemu Tx Moshi William aliyekuwa kwenye bendi ya jeshi hilo wakati huo, alinishauri kuachana na ufundi na kujiunga na kitengo cha Bendi,” anafahamisha Pembe.
Pembe anasema, Tx Moshi alimshauri hivyo kwasababu waliishi mtaa mmoja kabla hawajawa polisi, ambapo alikuwa akimuona namna alivyokuwa ‘mtundu’ kwenye gitaa la Solo.
Kiongozi wa polisi wakati huo, Mzee Mayagilo akamuombea Pembe uhamisho, lakini pia wakati anasubiri kwenda kuendelezwa ujuzi wa kupiga gitaa, mpigaji Saxophone wao, Abdul Mwalugembe akastaafu.
“Tukio hilo lilimfanya Mayagilo kunibadilisha na nikaanza kusomea upulizaji Saxophone, ambapo nilisoma nadharia mwezi mmoja na nusu na vitendo pia muda kama huo, nikawa fiti kabisa,” anasema Pembe.
Anasema kuwa, alirekodi nyimbo nyingi Polisi Jazz, baada ya zile zilizoambatana na ‘Mwaka wa Watoto’, ambazo hata hivyo hazikuchukua chati.
Mwaka 1987 alistaafu ligwaride akiwa askari mwenye cheo cha Koplo, kwa kununua mkataba, baada ya kuvunjika ghafla kwa ahadi aliyopewa na Jeshi, ya kupelekwa nchini Korea kuendelezwa kimasomo, kwa sababu alihisi ndoto zake za kufika mbali kielimu zilishagonga ukuta wa zege.
Akiwa na Vijana Jazz aliyojiunga nayo wakati imetoka kuipua vibao kama ‘Mari Maria’, ‘Ambha’ na ‘Bujumbura’, Pembe anasema kuwa, kibao chake cha kwanza kurekodi kilikuwa ni kile kinachokwenda kwa jina la ‘Miaka 10 ya Umoja wa Vijana’.
“Hadi nafungasha virago Vijana Jazz, niliyoitumikia na kushika nyadhifa mbalimbali za Kiuongozi, nilikuwa nimetunga vibao vinne ambavyo ni ‘Siri ya Ndani’, ‘Baba Sammy’, ‘Mwanamke Salo’ na ‘Dar es Salaam’,” anasema Pembe.
Pembe asiyependa kuona bendi haina maendeleo na ambaye katika muziki anawakubali King Enock na Elias Nyoni, anasema hajapata mafanikio wakati wa Vijana Jazz, zaidi ya kusafiri nchini Zambia pekee.
Kwa mtazamo wake, Pembe anaona biashara huria na udhamini katika vipindi, kwenye vituo mbalimbali vya radio na runinga ndivyo vinavyochangia kwa kiasi kikubwa kuliua Dansi.
Anasema mfumuko wa vituo vingi vya radio na runinga umefanya kuwapo na upendeleo binafsi kwa badhi ya mitindo ya muziki, huku mingine ikididimizwa kwa makusudi kwa manufaa ya watu wachache kama si mtu mmoja.
“Watoto wangu wanaoonekana kufuata kwa karibu zaidi nyayo zangu baba yao, ni Omary (21) ambaye yuko Kisiwani Zanzibar hivi sasa akijishughulisha na muziki wa Hoteli na Mwajuma (15), ambaye bado ni mwanafunzi wa darasa la saba,” anasema Pembe.
Tayari Pembe aliye mbioni kufungua chuo cha Saxophone, ameshawaambukiza wengi kipaji cha upulizaji chombo hicho, badhi yao wakiwa ni wanamuziki wa Dansi, Injili pamoja na miondoko mingine.
Aidha, badhi ya wasanii wa miondoko ya muziki wa Bongofleva waliomshirikisha kupuliza Saxophone kwenye vibao vyao, ni pamoja na Q Chillah, Kikosi cha Mizinga na Cindi katika nyimbo ya pamoja na Ommy Dimpoz.
Huyo ndiye Rashid Pembe, baba wa familia mwenye mke na watoto sita ambao ni Rehema, Pembe, Amina, Omary, Khalid na Mwajuma.
Alizaliwa mwaka 1957, Kisarawe Pwani na kupata elimu ya msingi katika shule nne tofauti ambazo ni Kisarawe, Vikindu, Sotele na Kisiju zote za mkoani Pwani, kuanzia mwaka 1966 hadi mwaka 1972

Hakuna maoni: