LAPF

LAPF
LAPF

Jumatatu, 30 Mei 2016

BENDI ZA SHULE ZA SEKONDARI


Leo nimeamka na wimbo uliopigwa mwaka 1969, na Mkwawa Jazz Band katika mtindo wao wa Ligija. Maneno ya wimbo huo yalikuwa kama ifuatavyo;
Huenda hasa utaijua shida niliyopata nilipokupenda
Ulisema hali yangu duni leo wanipendaje na wewe almasi,
Kwa kweli sina msamaha na sasa sahau kuwa bado naishi
Wamekwisha kuacha walo bora
Ohh uliniona chura ondoka
Usinijue sana nishaponda  ohh niseme lugha gani changanya
Tafadhali jifiche nisikuone, naenda ita konstebo kimbia
Utapendaje chura na wewe lulu
Na mimi sasa ghali ohh
Bendi hii ilikuwa moja ya bendi mbili za wanafunzi waliokuwa wakisoma Mkwawa High School kati ya mwaka 1969 na 1971. Kila Jumapili mchana bendi hizi mbili ziliporomosha muziki katika mfumo uliojulikana kama bugi, katika ukumbi wa Community Center pale Iringa. Bugi lilikuwa dansi lililoruhusu wanafunzi na watoto wadogo kufaidi dansi. Dansi lilianza saa nane mchana na kibali cha bugi kiliisha saa kumi na mbili kamili, pombe zilikuwa marufuku wakati wa bugi. Katika miaka hiyo shule za sekondari nyingi zilikuwa na bendi na bendi hizi nyingine zilikuja kuwa maarufu na hata kuja kutoa wanamuziki maarufu sana. Na kwa kuwa kulikuwa na utaratibu mzuri wanafunzi wengi waliokuwa wanamuziki wakati huo walikuja kuendelea na kuwa watu muhimu katika nyanja mbalimbali kitaifa. Kwa mfano katika bendi hiyo ya Mkwawa iliyoimba na hata baadae kurekodi wimbo wangu wa leo, wanamuziki wake woye walikuja kuwa watu wenye nafasi muhimu Kitaifa. Mpiga solo Sewando alikuja kuwa mwalimu  wa ‘electronics’ chuo kikuu cha Dar es Salaam, na pia ndie alikuja kuwa mwanzilishi wa bendi ya TZ Brothers. Sewando ambaye mwanae sasa ni producer maarufu wa muziki wa ‘kizazi kipya’, alianza muziki akiwa Kwiro Secondary ambako nako kulikuwa na bendi iliyowahi kurekodi nyimbo maarufu wakati huo, na hata kuwa chanzo cha baadhi ya mitindo iliyotumiwa na Morogoro Jazz band. Sewando alianza kupenda electronics wakati huo, na kuwa fundi wa vyombo vya bendi yake ya shule kiasi cha kupata jina la ‘The Mad Scientist’. Masanja alikuwa mpiga rhythm wakati huo na hatimae alikuja kuwa rubani wa ndege. John Mkama aliyepiga bezi alikuja kuwa mwandishi wa habari mahiri. Manji aliyepiga rhythm pia alikuja kuwa mhandisi wa ndege, na miaka mchache iliyopita alianzisha bendi iliyoitwa Chikoike Sound, na kwa sasa ana shule nzuri ya muziki Tabata, Dar es Salaam wakati muimbaji Danford Mpumilwa ni mwandishi maarufu, nae pia ndie alikuwa mwanzilishi wa bendi ya Serengeti ya Arusha. Mpiga tumba katika wimbo huo ni kiongozi maarufu wa dini mwenye wadhifa wa Askofu Mkuu. Hivyo kushiriki katika muziki hakukuwafanya wanamuziki hawa waishie kuwa wahuni au walevi walioharibikiwa kimaisha au kushindwa kuendelea ma masomo. Bendi ya pili ya Mkwawa Secondary ilikuwa ikipiga muziki wa kizungu na hasa wa mtindo wa soul. Bendi hii iliitwa  ‘The Midnight Movers’ ikiwa na wanamuziki kama Kafumba, Martin Mhando. Hans Poppe, Deo Ishengoma, amboa waliohai ni watu wenye nyadhifa muhimu katika jamii. Kuwa mwanamuziki hakukuwa tiketi ya kuwa muhuni. Kama nilivyosema shule nyingi za sekondari zilikuwa na bendi, pale Dodoma Secondary kulikuwa na bendi kiongozi wa bendi hii alikuwa Patrick Balisidya aliyekuja kuwa mwanamuziki maarufu alipokuja kuanzisha Afro 70.
Pale Azania Secondary School, kati ya mwaka 1966 hadi 1969, kulikuwa na kundi lililoitwa ‘The Blues’ ambalo lilikuwa likifundishwa na mwalimu wa muziki Martin Longfellow Mugalula ambaye baadae alihamia Finland na huko kutoa nyimbo kadhaa. Kundi hili lilikuwa likienda kupiga sehemu ambazo Kilwa Jazz walikuwa wakipiga hasa kutegea wakati Kilwa Jazz wamepumzika. Bendi kubwa zamani zilikuwa na kawaida ya kupumziki nusu saa katikati ya onyesho na wakati huo bendi ndogo zilipztz nafasi nafasi ya kupanda na kupiga muziki wao. Utaratibu huu ulijulikana kama kupara ‘kijiko’. Kati ya wanamuziki wa bendi hii ya The Blues, mmoja alikuja kuwa mwalimu shule ya Al Muntazir Upanga Dar es Salaam. Mazengo High School huko Dodoma nako kulikuwa na bendi, Jengo kwenye Microphone, marehemu Profesa  Wagao akipiga bezi Kime kwenye solo na  Balozi Tsere akipiga gitaa la rythm. Bendi hii ilichukua vyombo vibovu vya Central Jazz Band ambayo wakati huo ilikuwa imekufa na kuvikarabati katika maabara ya shule na kuanza kuvitumia. Shule zilikuwa na utaratibu ulioitwa Social Evening, katika utaratibu huu shule moja hualika shule nyingine mara nyingi shule ya wavulana ilialika shule ya wasichana kwa ajili ya dansi, na wakati huo record player zilizotumia sahani za santuri ndizo zilizotumika kutoa muziki. Katika social evening moja hapo Mazengo Secondary, Social Prefect hakupenda bendi hiyo ya wanafunzi ipige muziki, wanabendi walibembeleza na kuomba kupiga wimbo mmoja tu, kwa shingo upande wakaruhusiwa, baada ya kupiga wimbo huo, wasichana wa Msalato waliokuwa wageni na wanafunzi wengine wa Mazengo hawakutaka tena kucheza muziki kutoka kwenye player. Bendi ikachukua nafasi yake. Moshi Secondary nako kulikuwa na bendi wakiwemo wanamuziki kama Joseph Mkwawa, mfamasia mashuhuri kule Arusha, Peregreen ambae anawadhifa mkubwa jeshini nao walikuwa wakipiga kwenye sherehe za pale shuleni na mara nyingine kushirikiana na bendi kama Bana Afrika Kituli na Zaire Success kwenye maonyesho ya bendi hizo, bendi zilizokuwa na masikani mjini Moshi zama hizo. Hakika kupiga muziki si uhuni, ikiwa mazingira mazuri ya kazi hiyo yameandaliwa. Kuna ushahidi wa kisayansi kuwa kupiga muziki husaidia kuchamngamsha matumizi ya ubongo na hivyo kumfanya mwanafunzi kuwa na maendeleo mazuri shuleni   

Maoni 2 :

mirriam ndunge alisema ...

vizuri kusikia mziki

mc moise mugembe alisema ...

Kweli kabisa